Breaking News

Your Ad Spot

Apr 11, 2016

OBAMA : KOSA BAYA ZAIDI NILILOWAHI KUFANYA NI KUHUSU LIBYA

Obama: Kosa baya zaidi nililowahi kufanya ni kuhusu Libya
Rais Barack Obama wa Marekani amesema: "Kosa baya zaidi katika urais wangu ni kukosa mpango wowote kwa ajili ya zama za baada ya kumuangusha Muammar Gaddafi nchini Libya."
Kwa mujibu wa kanali ya CNN, Barack Obama ametoa kauli hiyo katika mahojiano na Fox News akijibu swali kuhusu kosa kubwa alilowahi kufanya katika kipindi chake cha urais.
Ingawa rais wa Marekani ametetea uingiliaji wa mgogoro wa Libya, lakini ameitaja hali ya hivi sasa nchini humo kuwa ni 'fedheha'.
Hii si mara ya kwanza kwa rais wa Marekani kuzungumza kuhusu uingiliaji nchini Libya chini ya uongozi wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO.
Mwezi Septemba mwaka jana, Obama, katika hotuba yake katika Umoja wa Mataifa alikosoa uingiliaji wa kijeshi Libya kwa kusema: "Muungano wetu ungeweza na ungepaswa kupanga njia ya kujaza pengo lililoibuka Libya."
Kukiri Obama kuhusu makosa ya Marekani Libya kunajiri katika hali ambayo nchi hiyo imekumbwa na mgogoro kiasi cha kukaribia kusambaratika vipande vipande.
Weledi wa mambo ya kisiasa wanasema, si tu kuwa Marekani haikufikia malengo yake Libya bali hujuma ya kijeshi nchini humo, sawa na Iraq na Afghanistan ni katika mambo yanayoashiria kufeli serikali ya Obama.
Mwaka 2011, maandamano ya watu wa Libya kufuatia mapinduzi ya watu wa Tunisia hatimaye yalimalizika kwa kuondolewa madarakani dikteta wa muda mrefu Muammar Gaddafi kufuatia uingiliaji wa kijeshi wa NATO. Uingiliaji huo uligeuza mkondo wa mapinduzi ya watu wa Libya ambapo Marekani na waitifaki wake Ulaya walipanda katika wimbi la wanamapinduzi ili kufikia malengo yao haramu.
Weledi wa mambo wanasema, hujuma ya NATO Libya ilikuwa na malengo kadhaa muhimu zaidi ikiwa ni kupora utajiri mkubwa wa nchi hiyo hasa wa mafuta ya petroli na pia kujipeneyeza katika eneo la Kaskazini mwa Afrika kufuatia mabadiliko yaloyoanzia Tunisia.
Libya ni moja ya nchi muhimu zaidi zenye kuzalisha mafuta ghafi ya petroli duniani kwani kabla ya 2011 ilikuwa ikizalisha mapima milioni moja na laki nane kwa siku.
Mafuta ya Libya ni hafifu na mazuri na hivyo huwa na nafasi muhimu katika kuleta mlingano wa soko la mafuta duniani kwa manufaa ya nchi za Maghairbi.
Kwa hivyo moja ya sababu muhimu za uingiliaji nchi za Magharibi Libya ni maslahi ya mafuta ya petroli au kwa jina jingine dhahabu nyeusi.
Sababu nyingine ya kuvamiwa Libya ni kuwa inapakana na nchi mbili muhimu za Kiarabu yaani Misri na Tunisia, nchi ambazo zilikuwa chimbuko la mapinduzi ya wananchi yaliyopeleka kuangushwa madikteta kaktika eneo. Kwa hivyo Libya ilikuwa muhimu kwa Marekani na waifitaki wake kwa matazamo wa kistratijia.
Baadhi ya weledi wanaamini hujuma ya NATO nchini Libya ni jambo lililobadilisha mkondo wa kisiasa wa nchi hiyo. Makundi mbali mbali ya kisiasa ambayo yalijitokeza mitaani yalikuwa na malengo ya pamoja lakini yalipopata silaha yakaanza mapigano baina yao.
Hivi sasa hali ya Libya inasikitisha. Mgogoro wa kisiasa unaendelea sambamba na kuharibu vituo vya kuzalisha mafuta na pia kuingia kundi la kigaidi la ISIS au Daesh nchini humo. Magaidi hao wamechukua udhibiti wa maeneo muhimu na ya kistratijia Libya.
Ingawa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya imeundwa baada ya mazungumzo magumu, lakini bado usalama haujaweza kurejeswa nchini humo na makundi ya kigaidi yangali yanaeneza ukatili. Kwa msingi huo bado kuna muda mrefu kabla ya nchi hiyo kufikia uthabiti.
Gazeti moja la Kimarekani hivi karibuni lilisema nchi za Magharibi zilichukua hatua ya hamaki wakati zilipoingilia kijeshi Libya.
Kukiri Obama kuhusu kosa alilofanya Libya ni jambo linaloipa nguvu dhana hiyo.
Kadhia ya vita dhidi ya ugaidi hivi sasa ni suala gumu sana kwa nchi za Magharibi kwani uingiliaji katika nchi mbali mbali duniani ndiyo sababu kuu ya kuibuka na kuenea ugaidi.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages