Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Magufuli akisaini makubaliano ya kuikaribisha Sudan kusini katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Rais wa Jamhuri ya Sudan kusini, Salva Kiir akisaini hati za makubaliano ya kuikaribisha rasmi Sudan kusini kuwa Mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Magufuli akizungumza wakati wa kumkaribisha Rais wa Jamhuri ya Sudan kusini, Salva Kiir Salaam katika ziara yake ya kikazi lenye dhumuni la kujiunga rasmi na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Rais wa Jamhuri ya Sudan kusini, Salva kiir akiagana na Jaji Mkuu wa Tanzania jaji Othman Chabde mara baada ya kumaliza kutia saini ya makubaliano ya nchi yake kujiunga na jumuiya ya Afrika Mashariki.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Magufuli akiaga viongozi mbalimbali wa ikiatifa na kimataifa mara baada ya kumaliza kutia saini ya makubaliano ya nchi ya Sudan Kusini kujiunga na jumuiya ya Afrika Mashariki.
………………………………………………………………………………………………..
Na. Immaculate Makilika – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Sudani ya Kusini Salva Kiiri ametia saini makubaliano ya mkataba wa kujiunga rasmi na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki katika hafla iliyofanyika leo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kutia saini mkataba huo, Rais Salva Kiiri amesema uamuzi wa nchi yake kujiunga na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki si tu kuwa kunaimarisha ujirani ulipo kati ya nchi hizo, lakini pia kunaimarisha ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki pamoja na watu wake ikiwa ni pamoja na kuendelea kukuza utamaduni wa Afrika.
“Naishukuru Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kwa kukubali Sudani ya Kusini kuwa mwanachama wa Jumuiya, na sasa Sudani ya Kusini imepata sehemu sahihi kwa kujiunga na Jumuiya hii ambayo inalenga kuleta maendeleo kwa wananchi wake” amesema Rais Kiir.
Rais Kiir amesema “tunajua malengo makubwa ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ni kuleta maendeleo kwa wananchi wake, na tunashuhudia kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni mfani bora Afrika na duniani kwa ujumla”.
Ameongeza kuwa Sudani ya Kusini imeona fursa zilizopo katika Jumuiya hii ikiwa ni pamoja na soko la pamoja (Common markert). Tayari tumetengeneza mifumo itakayosaidia ushiriki wetu katika Jumuiya ikiwemo kuanzishwa kwa Wizara itakayoshughulikia masuala ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, ikiwa ni pamoja na kutunga sheria mbalimbali zitakazowezesha kupatikana kwa Amani ya kudumu nchini humo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, amepongeza juhudi zilizofanywa na Sudani ya Kusini na hatimaye kujiunga na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ikiwa ni muda mfupi tu tangu nchi hiyo ipate uhuru wake mnamo Julai 20, 2012.
Rais Magufuli amesema kuwa siku zote Sudani ya Kusini imekuwa sehemu ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kwa uchumi wake, utamaduni wake, lugha pamoja na historia yake na inaunganishwa na nchi za Jumiya hii kwa barabara pamoja na mto Nile.
Aidha, Rais Magufuli “amesema malengo ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ni pamoja na kukuza biashara na uwekezaji, kutoa bure huduma na uhuru wa wananchi kwenda popote ndani ya Jumuiya. Hata hivyo, Jumuiya hii inakumbwa na machafuko ya mara kwa mara na kuwa kikwazo kwa maendeleo ya uchumi wake”.
Amesema Sudani ya Kusini imekubaliwa kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kwa kuwa imetimiza makubalino yaliyowekwa na Jumuiya ikiwemo kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.
Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afika ya Mashariki, Kikanda na Kimataifa Balozi, Dkt. Augustine Mahiga, amesema kuwa Sudani ya Kusini inakuwa mwanachama wa sita wa Jumuiya hiyo, na kuwa ushirikiano wa kiuchumi uliopo katika nchi hizi utakuwa mfano wa kuigwa kwa nchi zinazoendelea.
Sudani ya Kusini iliomba kujiunga na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki mnamo Novemba 10, 2012, ikiwa ni chini ya miezi minne tangu nchi hiyo ipate uhuru wake.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269