Na Lydia Churi- Mwanza
Mahakama ya Tanzania inakusudia
kuongeza idadi ya Majaji katika kanda yake ya Mwanza ili kuongeza
msukumo wa kumaliza kesi za mauaji kutokana na kanda hiyo kuongoza kwa
kuwa na kesi nyingi za mauaji nchi nzima.
Akizungumza wakati wa ziara yake
ya kukagua shughuli za kimahakama katika kanda ya Mwanza, Jaji Mkuu wa
Tanzania Mheshimiwa Mohamed Chande Othman amesema ataongeza idadi ya
majaji katika kanda hiyo ili kesi hizo za mauaji zimalizike kwa wakati.
Jaji Mkuu pia ameiagiza Mahakama
Kuu kanda ya Mwanza kuzipa msukumo maalum kesi za mauaji ili kuhakikisha
zinamalizika mapema na kupunguza mlundikano wa kesi katika mahakama za
Tanzania.
Awali akisoma taaarifa ya hali
halisi ya kesi katika Mahakama Kuu kanda ya Mwanza, Jaji Mfawidhi wa
kanda hiyo Mheshimiwa Robert Makaramba alisema kanda ya Mwanza ndiyo
inayoongoza kwa kuwa na kesi nyingi za mauaji nchini ambapo hadi kufikia
Aprili mwaka huu kuna jumla ya kesi 512 za mauaji.
Pamoja na mkakati wa Jaji Mkuu
kuongeza idadi ya Majaji ili kumaliza kesi hizo, Jaji Mfawidhi wa kanda
ya Mwanza alisema wameshachambua kesi hizo za mauaji ambapo Jaji
Kiongozi pia aliahidi kuwaongezea jumla ya Majaji 11 ili waweze kusaidia
kusukuma kesi hizo.
Jaji Makaramba alisema kati ya
mwezi Juni na Julai jumla ya vikao 11 vinatarajiwa kukaa ili kusikiliza
kesi 123 zilizopangwa kusikilizwa. Alisema kati ya kesi hizo, 35 ni zile
zitakazosikilizwa kwa mara ya kwanza na kesi 88 ni zile
zitakazosikilizwa mpaka mwisho.
Alisema endapo vikao hivyo vitafanyika kama ilivyokusudiwa vitasaidia kupunguza kesi zilizopo mahakamani kwa miaka mingi.
Hadi kufikia mwezi April mwaka
huu, Mahakama Kuu kanda ya Mwanza ina jumla ya kesi 2771 za aina zote
zikiwemo zile za Madai ya kawaida, Madai ya Ardhi na za jinai. Ili
kuongeza kasi ya usikilizwaji wa kesi hizo, kila Jaji amepangiwa
kusikiliza kesi 346. Kanda hiyo ina Majaji nane (8).
Jaji Mkuu wa Tanzania ameanza
ziara katika kanda ya Mwanza inayohusisha mikoa ya Geita, Mwanza na Mara
ambapo atakagua shughuli mbalimbali za kimahakama katika kanda hiyo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269