Muungano mkuu wa upinzani nchini Burundi
unaoitwa CNARED umesema uko tayari kushiriki duru mpya ya mazungumzo ya
amani iwapo utaalikwa rasmi.
Pancrace Cimpaye, Msemaji wa muungano huo unaovileta pamoja
vyama kadhaa vya upinzani pamoja na wakuu wa zamani wa serikali amesema
wako tayari kushiriki mazungumzo yajayo ya kuutafutia ufumbuzi mzozo wa
kisiasa nchini Burundi na kusisitiza kuwa mazungumzo yaliyoanza Jumamosi
mjini Arusha nchini Tanzania na kumalizika jana, ni ya upande mmoja na
hayatakuwa na tija. Amesema duru mpya ya mazungumzo yanafaa kuvileta
pamoja vyama vyote vya siasa vikiwemo vya upinzani, mashirika ya kiraia
na asasi za kijamii zinazopinga muhula wa tatu kwa Rais Pierre
Nkurunziza wa nchi hiyo.
Benjamin William Mkapa, rais wa zamani wa Tanzania na mpatanishi wa
jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki anayesimamia mazungumzo hayo, jana
Jumanne katika siku ya mwisho ya vikao hivyo alisema kuwa mazungumzo
hayo yamefanyika katika ngazi za kidiplomasia, wawakilishi wa serikali,
wajumbe wa chama tawala nchini Burundi CNDD-FDD na kadhalika wawakilishi
wa jumuiya za kiraia ndani ya nchi hiyo, na kwamba wanashauriana na
viongozi wa kisiasa ambao hawakuhudhuria kikao cha Arusha, kuwashawishi
washiriki duru ijayo ya mazungumzo.
Machafuko nchini Burundi yaliibuka mwezi Aprili mwaka jana, baada ya
chama tawala kuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo kugombea
kwa mara ya tatu mfululizo kwenye uchaguzi mkuu uliopita.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269