TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUTENGUA NAFASI YA MKURUGENZI WA HUDUMA ZA TIBA SHIRIKISHI NA MKUU WA KITENGO CHA KUHIFADHI MAITI
Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence
Museru ametengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Shirikishi Dkt.
Praxeda Ogweyo kuanzia leo Juni 23,
2016 ili kupisha uchunguzi kutokana na kushindwa kusimamia vizuri
wafanyakazi walioko chini yake na kusababisha Kitengo cha Kuhifadhi
Maiti kuchanganya maiti wakati wa kuzitoa kwa ndugu mara mbili katika
kipindi kisichozidi miezi mitatu na kusababisha usumbufu
mkubwa kwa wafiwa na Hospitali kwa ujumla. Ikumbukwe kuwa tarehe 9,
Aprili 2016 tukio kama hili lilitokea na kusababisha usumbufu mkubwa kwa
ndugu, jamii na Hospitali kwa ujumla. Aidha tukio hili tena
limejitokeza tarehe 20 Juni, 2016.
Prof.
Museru amemteua Dkt. Flora Lwakatare Mkuu wa Idara ya Radiolojia
kukaimu nafasi hiyo. Kurugenzi ya Tiba Shirikishi inasimamia Idara ya
Mionzi na Idara ya Maabara ambapo Kitengo
cha Kuhifadhi Maiti kipo chini ya maabara. Vilevile Prof. Museru
ametengua uteuzi wa Mkuu wa Kitengo cha Kuhifadhi Maiti Hospitali ya
Taifa Muhimbili Dkt. Innocent Mosha na kumteua Dkt Herbert Nguvumali
kukaimu nafasi hiyo.
Aidha,
wahudumu waliohusika katika matukio haya wameondolewa katika chumba cha
kuhifadhi maiti kuanzia leo tarehe 23 Juni, 2016 ili kupisha uchunguzi.
Katika uchunguzi huu, kamati
maalumu imeundwa kuchunguza kwa kina utendaji wa Kitengo cha Kuhifadhi
Maiti ili kutoa mapendekezo ya jinsi ya kurekebisha utendaji wa kitengo
hicho ili matukio kama haya yasitokeze tena.
Imetolewa na;
Aminiel Buberwa Aligaesha,
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano,
Hospitali ya Taifa Muhimbili,
JUNI 23, 2016.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269