Wanamgambo wa ash Shabab wa Somalia
Watu wasiopungua sita wameuawa baada ya watu
wenye silaha kuyamiminia risasi mabasi mawili hii leo katika kaunti ya
Mandera nchini Kenya kwenye mpaka wa nchi hiyo na Somalia.
Fredrick Shisia, Kamishna wa Kaunti ya Mandera amesema kuwa,
tukio hilo limetokea leo saa tatu na nusu asubuhi kwa majira ya eneo
hilo wakati mabasi mawili hayo yalipokuwa yanaelekea katika mji wa
Mandera kutokea jijini Nairobi.
Kamishna Shisia ameongeza kuwa, hadi tunaandika habari hii watu sita
wamethibitishwa kuuawa katika ufyatuaji risasi huo. Ripoti zinasema kuwa
basi la kwanza lilipigwa risasi na watu wwenye silaha likiwa kati ya
miji ya Elwak na Wargadud na basi la pili lijulikano kwa jina la E-Coach
lilishindwa kuendelea na safari baada ya kupigwa risasi. Wengi wa
waliouliwa walikuwa katika basi la pili. Abiria waliojeruhiwa
wanaendelea kupatiwa matibabu katika kituo cha Afya cha Wargadud. Polisi
mmoja wa Kenya ni miongoni mwa watu waliouawa kwenye shambulio hilo na
polisi mwingine mmoja amejeruhiwa. Polisi hao walikuwa wakiyasindikiza
mabasi hayo. Polisi ya kaunti ya Mandera jana ilitahadharisha kuhusu
safari za mabasi katika eneo hilo hadi utakapomalizika mwezi mtukufu wa
Ramadhani kutokana na vitisho vya usalama vilivyotolewa na wanamgambo wa
kundi la al Shabab wenye makao yao makuu nchini Somalia. Tayari polisi
imeanzisha oparesheni ya kuwasaka wahusika wa jinai hiyo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269