Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya mji wa Bunda mkoani Mara, Bibi. Janeth Mayanja akiwa ofisini kwake. (Picha na Ofisi ya Mkurugenzi Bunda)
|
Na. Immaculate Makilika
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya mji wa Bunda mkoani Mara, Bibi. Janeth Mayanja amemsimamisha kazi mtumishi wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji kwa kosa la kujipatia fedha kinyume na taratibu za utumishi wa umma.
Akizungumza leo mjini Bunda wakati wa tukio hilo, Bibi. Mayanja alisema kuwa ameamua kumsimamisha kazi kwa muda, Bw.Eliudi Haonga ambaye ni mtumishi wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji pia ni Mthamini wa Halmashauri hiyo ili kupisha uchunguzi kwa kosa la kujipatia fedha kinyume na taratibu za utumishi wa umma.
“Tarehe 28 mwezi Juni mwaka huu Bw.Eliudi Haonga alipokea fedha kiasi cha shilingi milioni saba kutoka kiwanda cha Olam ikiwa ni kodi ya pango kwa mwaka kodi 2015/2016, lakini mtumishi huyo alihifadhi kwenye akaunti ya Halmashauri ya mji yaani ‘own source’ fedha kiasi cha shilingi milioni mbili tu, na kiasi kilichobaki yaani milioni tano alizitumia kwa masuala binafsi kinyume na taratibu za utumishi wa umma” alisema Bibi Mayanja
Aliongeza kuwa Bw. Haonga aligushi risiti ya Halmashauri ya Mji na ambayo aliikabidhi katika kiwanda cha Olam baada ya kupokea fedha hizo.
Alisisitiza kuwa mtumishi huyo amesimamishwa kazi kwa mujibu wa kifungu namba 38 (1) cha kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2003.
Aidha, Bibi Mayanja amewaasa watumishi wa umma wanaofanyakazi katika Halmashauri hiyo kuwa waadilifu kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi. Vile vile ameonya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269