Huku timu za uokoaji zikiendelea na kazi ya
kuwatafuta majeruhi na manusura wa tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 6.2
kwa kipimo cha rishta lililotokea katikati mwa Italia, hadi sasa
imethibitishwa kuwa watu wasiopungua 247 wamepoteza maisha katika janga
hilo la kimaumbile.
Hadi kufikia asubuhi ya leo, idadi ya majeruhi imeripotiwa kuwa
ni watu 368, baadhi yao wakiwa katika hali mahututi huku idadi ya vifo
ikitazamiwa kuongezeka.
Kwa muda wote wa usiku wa kuamkia leo, timu za uokozi zimekuwa
zikijaribu bila matumaini kuwatafuta majeruhi na manusura wa tetemeko
hilo chini ya vifusi vya majengo yaliyoporomoka.
Tetemeko la ardhi la jana karibu na mji wa Norcia ulioko kwenye eneo
la Umbria katikakati mwa Italia lililotokea kabla ya mapambazuko
lilisomba nyumba na kubomoa barabara katika eneo la milimani kilomita
140 mashariki mwa mji mkuu wa Italia, Rome.
Mamia ya watu walipitisha usiku wa baridi jana kwenye mahema nje ya
nyumba zao kwa kuhofia hatari ya athari za baada ya tetemeko kuu.
"Usiku huu utakuwa usiku wetu wa kwanza wa jinamizi" alisema
Alessandro Gabrielli, mmoja wa mamia ya watu waliokuwa wakijiandaa
kulala nje kwenye mahema jana usiku na kwenye bustani za mji wa
Amatrice, ambao nyumba zao zimebomolewa na zilzala.
Sergio Pirozzi, Meya wa mji huo wa Amatrice ulioathriwa vibaya zaidi
na tetemeko la ardhi amesema, viwiliwili saba tu vimepatikana kwenye
hoteli moja ya mji huo iliyoporomoka ikiwa imepokea wageni wapatao 70.
"Nusu ya mji imetoweka", ameeleza Meya Pirozzi.
Mbali na mji huo, miji mingine iliyoathiriwa vibaya na zilzala ya alfajiri ya jana ni Accumoli, Posta na Arquata del Tronto.
Tetemeko kubwa la ardhi na la mwisho kutokea nchini Italia lilikuwa
la mwaka 2009 lililoukumba mji wa katikati mwa nchi hiyo wa L'Aquila na
kuua watu zaidi ya 300.../
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269