Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetangaza kuwa, imewaachilia huru wafungwa 24 wa kisiasa.
Alexis Thambwe Mwamba, Waziri wa Sheria wa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo amesema katika mkutano wake na waandishi wa habari
kwamba, serikali ya nchi hiyo imechukua uamuzi wa kuwasamehe na
kuwaachilia huru wafungwa 24 wa kisiasa kati ya 26 waliokuwa
wakishikiliwa gerezani.
Uamuzi huo umechukuliwa na serikali ya Kinshasa kufuatia mashinikizo ya wapinzani katika nchi hiyo.
Wapinzani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo walikuwa wakishinikiza
kuachiliwa huru wafungwa 26 wa kisiasa wanaoshikiliwa katika magereza
mbalimbali ya nchi hiyo kama sharti lao la kushiriki katika mazungumzo
ya kitaifa.
Kuachiliwa wafungwa hao wa kisiasa kumetathminiwa kama juhudi za
serikali ya Kinshasa za kupunguza mivutano katika nchi hiyo kabla ya
kufanyika uchaguzi mkuu ujao.
Uchaguzi wa Rais katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umepangwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu.
Hata hivyo kumekuwa na hati hati juu ya kufanyika uchaguzi huo.
Kambi ya upinzani huko Congo imekuwa ikikataa wito wa kufanya
mazungumzo na serikali ikidai kuwa ni mbinu ya Rais Kabila ya kutaka
kurefusha kipindi cha kubakia madarakani.
Kwa mujibu wa katiba ya Congo DR, kila raia anayeshinda kiti cha rais
wa nchi anaweza kuongoza vipindi viwili mfululizo. Hata hivyo kuna
tetesi kwamba kiongozi wa sasa wa nchi hiyo ambaye alishika hatamu za
uongozi mwaka 2001 anataka kugombea kwa mara ya tatu.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269