Ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na
Serikali ya Saudi Arabia umeendelea kukosolewa vikali katika duru
mbalimbali za kikanda na kimataifa.
Saudi Arabia inayotambuliwa kuwa husuni na ngome ya udikteta ni
miongoni mwa wakiukaji wakubwa wa haki za binadamu duniani. Watawala
wa kifalme wa nchi hiyo hawaheshimu haki za binadamu si ndani ya Saudia
pekee bali hata katika kanda hii ya Asia.
Ndani ya Saudi Arabia kwenyewe wanawake na Waislamu wa madhehebu ya
Shia ndio wahanga wakubwa zaidi siasa za kikandamizaji wa Aal Saud.
Wanawake nchini humo hawana hata haki ya kuendesha magari yao wenyewe na
hata haki ya kupiga kura waliyopewa hivi karibuni bado haijaanza
kutekelezwa.
Vyombo vyote vya habari vya Saudi Arabia vinamilikiwa na watu wa
kizazi tawala na ni kosa la jinai kukosoa wanamfalme na viongozi wa nchi
hiyo. Ubaguzi wa kijamii hususan dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia
unaonekana kila mahala. Nchini Saudi Arabia wananchi hawana haki yoyote
isipokuwa kutii amri za utawala wa kifalme.
Watawala wa kizazi cha Aal Saud hususan katika kipindi cha miaka
mitano ya hivi karibuni wamekuwa miongoni mwa wakiukaji wakubwa wa haki
za binadamu katika nchi nyingine. Serikali ya nchi hiyo inawaunga mkono
na kuwafadhili kwa hali na mali magaidi nchini Syria ambako maelfu ya
raia wasio na hatia wanauawa kila siku.
Machi mwaka 2015 utawala wa kifalme wa Saudi Arabia ulianzisha
mashambulizi ya kinyama dhidi ya nchi maskini zaidi ya Kiarabu katika
eneo la Mashariki ya Kati yaani Yemen, na mashambulizi hayo bado
yanaendelea. Matokeo ya mashambulizi hayo ni kuuawa maelfu ya Waislamu
wasio na hatia, kuharibiwa asilimia 80 ya miundombinu ya nchi hiyo,
kuwafanya Wayemeni milioni 3 kuwa wakimbizi, kuharibu umoja wa kitaifa
wa nchi hiyo na kuwapa magaidi fursa ya kudhibiti baadhi ya maeneo ya
Yemen.
Huko Iraq pia watawala wa Saudi Arabia wanawaunga mkono magaidi wa
kundi la kiwahabi la Daesh na wanafanya kila wawezalo kudhoofisha
serikali ya nchi hiyo kupitia njia ya kuzusha mivutano ya kikaumu na
kimadhehebu.
Licha ya hayo yote lakini tawala zinazodai kutetea demokrasia na haki
za binadamu za Magharibi hususan Marekani si tu kwamba hazijachukua
hatua yoyote dhidi ya Saudia bali zinaiunga mkono na kuisaidia. Miongoni
mwa vielelezo vya uungaji mkono wa nchi za Magharibi kwa utawala katili
wa Saudi Arabia ni kuchaguliwa nchi hiyo kama Mwenyeliti wa Baraza la
Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, suala ambalo limetambuliwa na
wachambuzi wengi wa mambo kuwa ni sawa na nchezo mchungu wa kuigiza wa
kisiasa. Suala hilo linakosolewa sana na taasisi za kiraia na jumuiya za
kimataifa za kutetea haki za binadamu.
Katika uwanja huo jana Ijumaa katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa
ya Ubinadamu wanaharakati wa masuala ya kiraia nchini Uingereza
walimtaka Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Theresa May kupinga suala la
kuchaguliwa tena Saudi Arabia kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Haki za
Binadamu.
Wakati huo huo Belkis Wille ambaye ni mhakiki mkuu wa shirika la
kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) ametoa taarifa
akilitaka Bunge la Marekani kupinga mauzo ya silaha zenye thamani ya
dola bilioni 1.15 kwa serikali ya Saudi Arabia. Sababu ya ombi hilo ni
kwamba HRW inaamini Saudia inatumia silaha hizo kuua watu wa Yemen.
Awali shirika hilo la kutetea haki za binadamu lilitoa wito wa kufanyika
uchunguzi huru kuhusu jinai za kivita zilizofanywa na Saudi Arabia
nchini Yemen.
Nchi na mashirika mengine ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu
kama Amnesty International pia yametaka kufanyike uchunguzi kuhusu
ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, mauaji na jinai zinazoendelea
kufanywa na Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya raia wa Yemen.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269