Picha: Kikao cha Bunge la Burundi
------------------
BURUNDI
Wabunge wa Burundi wamepinga azimio nambari 2303 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kukataa kabisa suala la kutumwa nchini humo askari polisi 228 wa kimataifa.
------------------
BURUNDI
Wabunge wa Burundi wamepinga azimio nambari 2303 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kukataa kabisa suala la kutumwa nchini humo askari polisi 228 wa kimataifa.
Katika kikao chake cha jana, Bunge la Burundi lilipinga azimio
hilo la Baraza la Usalama na kutangaza kuwa uamuzi huo wa Umoja wa
Mataifa hauendani na mtazamo wa serikali ya Bujumbura.
Wabunge wameeleza kuwa uamuzi wa kutaka kutuma kikosi cha askari
polisi nchini Burundi umechukuliwa bila ya kushauriana na serikali ya
nchi hiyo.
Taarifa ya Bunge la Burundi inasema, katika mpango huo haikuzingatiwa
na kutiliwa maanani hali ya kisiasa na kiusalama ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa azimio hilo ambalo lilipendekezwa na Ufaransa, askari
polisi 228 wa Umoja wa Mataifa watatumwa nchini Burundi kwa shabaha ya
kurejesha amani na kulinda haki za binadamu nchini humo kwa kipindi cha
mwaka mmoja. Muda wa huduma za kikosi hicho utaongezwa iwapo hali
itakuwa mbaya zaidi.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia limeihimiza serikali ya
Burundi kufanya mazungumzo na makundi yote ya upinzani wakiwemo
wapinzani walioko nje ya nchi kwa lengo la kukomesha mgogoro wa ndani ya
nchi hiyo.
Azimio hilo la Baraza la Usalama limekabiliwa na upinzani mkubwa wa
wananchi huko Burundi na ripoti zinasema kuwa, maandamano dhidi ya
Ufaransa ambayo ndiyo iliyopendekeza muswada wa azimio hilo, bado
yanaendelea.
Msemaji wa serikali ya Burundi, Philippe Nzobonariba ametangaza kuwa,
suala la kutumwa askari polisi wa Umoja wa Mataifa nchini humo ni
kinyume na sheria za kimataifa zinazolinda mamlaka ya kujitawala nchi
wanachama.
Kabla ya hapo Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi alikuwa amesema
kwamba, kutumwa askari wa kimataifa nchini humo ni kuingilia masuala ya
ndani ya Burundi na kwamba nchi yake itakabiliana nao kama wavamizi.
Mgogoro wa ndani nchini Burundi unaendelea kwa zaidi ya mwaka mmoja
sasa na juhudi za kikanda na kimataifa za kujaribu kukomesha machafuko
na ghasia nchini humo bado hazijazaa matunda. Machafuko hayo yalishika
kasi baada ya kiongozi wa sasa wa nchi hiyo kutangaza kuwa atagombea
kiti cha rais kwa mara ya tatu hapo mwaka jana. Suala hilo lilipingwa na
vyama vya kisiasa vya upinzani vikisema ni ukiukaji wa katiba na
makubaliano ya amani ya Arusha.
Hali hiyo imezidisha machafuko ya ndani kwa kadiri kwamba, Umoja wa
Mataifa umetangaza kuwa, serikali ya Bujumbura imezidisha mateso na
unyanyasaji dhidi ya wakosoaji na wapinzani wake. Vilevile ripoti
zinasema kuwa askari wa Burundi wanahusika na visa vingi vya kuwabaka na
kuwanajisi wanawake wanaoshikiliwa na vyombo vya usalama.
Mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Mateso, Jens Modvig ameeleza wasiwasi wake kuhusu machafuko ya kikabila nchini Burundi na kusema: Ripoti mbalimbali zinaonesha kuwa, manyanyaso na mateso nchini Burundi yanafanyika kwa sababu za kisiasa na kwamba ukatili unaofanyika dhidi ya makundi ya kisiasa na kikabila unapinga kengele ya hatari ya kuanza mauaji ya kimbari nchini humo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269