Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari
(hawako pichani) kuhusu utekelezaji wa agizo la kuondoa watumishi hewa
katika orodha ya malipo ya mishahara Serikalini ofisini kwake mapema
jana.
Baadhi ya
waandishi wa habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J.
Kairuki (Mb) alipozungumza leo ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Hussein Makame-MAELEZO
Waajiri
264 kati ya waajiri wote 409 Serikalini wamewasilisha taarifa zao kuhusu
kuwepo kwa watumishi hewa ambapo kati ya waajiri hao waajiri 63
wamethibitisha kwamba hawana watumishi hewa katika Taasisi zao.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi Wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Angellah Kairuki (MB), amebainisha hayo wakati alipozungumzia na
waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa
waajiri 201 wana watumishi hewa kuanzia mmoja na kuendelea.
“Waajiri
264 kati ya waajiri wote 409 wamewasilisha taarifa zao kuhusu uwepo wa
watumishi hewa. Kati ya waajiri 264 waliowasilisha taarifa zao, waajiri
63 wamethibitisha kwamba hawana watumishi hewa katika Taasisi zao na
waajiri 201 wana watumishi hewa mmoja (1) na kuendelea.” Alisema Waziri
Kairuki.
Hata
hivyo, alisema zipo taasisi 145 ambazo hazijawasilisha taarifa iwapo
zina watumishi hewa au la ikiwemo Mabaraza 11, Bodi 10, Vyuo Vikuu 25,
Hospitali 3 na Ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa 12.
Alizitaja
taasisi nyingine kuwa ni Mamlaka 6, Tume 10, Mamlaka za Serikali za
Mitaa 38, Taasisi za Umma na Wakala 30 ambapo aliziagiza Taasisi
zote ambazo hazijawasilisha taarifa za watumishi hewa kufanya hivyo
kabla au ifikapo tarehe 26 Agosti mwaka huu.
Waziri
Kairuki alieleza kuwa kuanzia Agosti 15 mwaka huu, ofisi yake ilianza
zoezi la uhakiki wa kushtukiza katika taasisi sabini za Serikali
zikiwepo Wizara, Idara za Serikali Zinazojitegemea na kwamba zoezi hilo
linaendelea.
Aliongeza
kuwa uhakiki wa kustukiza utafanyika pia kwenye Sekretarieti za Mikoa,
Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi za Umma kwa madhumuni ya
kujiridhisha kwamba taarifa za watumishi hewa zilizowasilishwa na
waajiri ni sahihi.
Alibainisha
kuwa katika kufanikisha uhakiki huo, Ofisi yake imechukua hatua kadhaa
ikiwemo kuendelea kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa Maafisa Utumishi
wenye dhamana ya kutumia mfumo wa malipo ya mshahara kukuza uwajibikaji
kwa maafisa wanaosimamia malipo ya mishahara kwa kuwachukulia hatua za
kinidhamu au kisheria wanaobainika kusababisha watumishi hewa.
“Aidha
ofisi yangu pia inafanya uhakiki wa kushtukiza na kuanza safari ya
kuunganisha Mfumo wa Malipo ya Mishahara na mifumo mingine mikubwa kama
ya NIDA, RITA na Baraza la Mitihani la Taifa, na kuwezesha mfumo
kuwaondoa moja kwa moja (automatically) watumishi waliofikisha umri wa
kustaafu kwa lazima.” alisema.
Waziri
Kairuki atatoa taarifa kamili ya watumishi hewa baada ya kupata taarifa
hizo kutoka kwa waajiri ambao hawajawasilisha taarifa hizo na kukamilika
kwa zoezi la uhakiki wa Taasisi sabini (70) linaloendelea sasa.
“Hivyo
naagiza Taasisi zote ambazo hazijawasilisha Taarifa za Watumishi Hewa
kufanya hivyo kabla au ifikapo tarehe 26 Agosti, 2016.” Alisema Waziri
Kairuki.
Alisema
kuwa ofisi yake itawasilisha taarifa rasmi ya watumishi hewa kwa
Mheshimiwa Rais ikiwa na orodha na majina ya Taasisi ambazo
zimewasilisha taarifa ya watumishi hewa na na zile ambazo
hazijawasilisha taarifa hizo.
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli mnamo Machi 15
mwaka huu aliwaagiza Wakuu wa Mikoa na Waajiri wote kwa ujumla kuchukua
hatua ya kuhakikisha katika Mikoa au Taasisi zao hakuna watumishi hewa
ifikapo tarehe 30 Machi, 2016.
Katika
kutekeleza agizo hilo Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora imekuwa ikifuatilia utekelezaji wa agizo hilo na mnamo Mei
26 mwaka huu waajiri wote waliagizwa kuwasilisha taarifa za mwisho za
zoezi la kuwabaini na kuwaondoa watumishi hewa katika orodha za malipo
ya mshahara (payroll) ifikapo mwisho wa Mwezi Juni, 2016.
Waajiri
walitakiwa kutuma jina la Taasisi, Fungu la Taasisi (Vote), namba ya
Utambulisho ya Mtumishi wa Umma (Cheki Namba), jina kamili la mtumishi;
cheo cha mtumishi, jina la tawi la Benki ambalo mshahara wa mtumishi
umekuwa ukipitishwa au ukilipwa.
Taarifa
nyingine zinazotakiwa kutumwa ni hatua zilizochukuliwa na mwajiri dhidi
ya watumishi hewa waliobainika kama kurejesha fedha, na Maafisa wengine
wa Taasisi husika waliosababisha uwepo wa Watumishi hao kuwachukulia
wahusika hatua za kinidhamu au kisheria.
Nyingine
ni namba ya akaunti ya Benki ya mtumishi, tarehe ambayo mtumishi
aliondolewa kwenye mfumo wa taarifa ya Kiutumishi na Mshahara, kiasi cha
fedha zilizolipwa kwa mtumishi husika tangu alipotakiwa kuondolewa hadi
tarehe aliyoondolewa kwenye mfumo na sababu ya kuondolewa kama utoro,
kufariki dunia, kuacha kazi, kustaafu na sababu nyingine.(P.T)
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269