RAIS YOWERI MUSEVENI |
DAR ES SALAAM
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 17
Septemba, 2016 amepokea taarifa ya maafa yaliyosababishwa na tetemoko la ardhi
lililotokea katika Mkoa wa Kagera na mikoa jirani ya Mwanza, Geita na Mara
kutoka kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa,
Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Pamoja
na kupokea taarifa hiyo Rais Magufuli amepokea mchango wa fedha taslimu kiasi
cha Dola za Kimarekani laki mbili (USD-200,000/-) sawa na takribani Shilingi za
Kitanzania Milioni Mia nne na therathini na saba (Tshs-437,000,000/-) kutoka
kwa Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni na pia amepokea
taarifa ya mchango wa mabati, blanketi na magodoro vyenye thamani ya Shilingi
za Kitanzania milioni 115 kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru
Kenyatta kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi Mkoani Kagera.
Katika
taarifa yake Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amesema tetemeko hilo
limesababisha vifo vya watu 17, majeruhi 440, nyumba 2063 zimeanguka, nyumba
14,081 zipo katika hali hatarishi na nyumba 9,471 zimepata uharibifu mdogo,
huku watu 126,315 wakihitaji misaada mbalimbali.
"Mhe.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali zikiwemo
kupeleka chakula, huduma za matibabu na hifadhi za dharura kwa waathirika na
pia inaratibu ukusanyaji wa michango kutoka sehemu mbalimbali ambapo mpaka sasa
kiasi cha Shilingi za Kitanzania Bilioni tatu nukta sita (Tshs Bilioni 3.6)
zimepatikana", imesema taarifa ya Ikulu.
Akizungumza
baada ya kupokea taarifa ya maafa na michango kwa ajili ya waathirika wa maafa
hayo, Rais Magufuli amewashukuru wote waliojitoa kusaidia waathirika wakiwemo
Marais Mhe. Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, Mhe. Uhuru Kenyatta wa Kenya na
Paul Kagame wa Rwanda ambao wamempigia simu za kumpa pole na tayari wametoa
misaada yao, na pia nchi mbalimbali, mashirika, wafanyabiashara, watumishi wa
umma na watu binafsi na amesema michango hiyo ina umuhimu mkubwa katika
kukabiliana na athari za maafa haya.
Dkt.
Magufuli ametoa wito kwa Watanzania na wote walioguswa na maafa haya kuendelea
kutoa misaada kwa waathirika kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, huku akionya na
kuvitaka vyombo vya dola kuwafuatilia watu wanaotaka kutumia maafa haya
kukusanya michango kwa lengo la kujinufaisha.
Rais
Magufuli amebainisha kuwa Serikali itahakikisha inarekebisha miundombinu
iliyoharibika zikiwemo shule, vituo vya matibabu, barabara na huduma nyingine
za kijamii na pia ametaka wananchi waliokumbwa na madhara ya tetemeko hususani
nyumba zilizobomoka, wajipange kurekebisha nyumba zao kwa kuwa Serikali pekee
yake haitaweza kujenga nyumba zote zilizobomoka.
Aidha,
Rais Magufuli amewasihi Watanzania kuwapuuza watu wanaotaka kutumia maafa haya
kueneza uchonganishi na chuki dhidi ya Serikali na ameweka wazi kuwa mpaka sasa
hakuna teknolojia ya kutabiri kutokea kwa tetemeko la ardhi na kwamba tetemeko
hili halikuletwa na Serikali.
Dkt.
Magufuli amesema hata mataifa makubwa yenye maendeleo makubwa ya uchumi na
teknolojia yanakumbwa na tetemeko la ardhi na kusababisha vifo vya idadi kubwa
ya wananchi na uharibifu mkubwa wa mali.
"Nilikuwa
najaribu kuangalia kwa mfano nchi kama China kwenye mwaka 2014 watu 617
walipoteza maisha, Mwaka 2013 walipoteza watu 193, Mwaka 2010 walipoteza watu
2,998 Mwaka 2008 China ilipoteza watu 98,712.
Ukijaribu
kuangalia Japan, nchi ambayo imeendelea na ina utaalamu wa hali ya juu sana,
kwenye mwaka 2016 tarehe 14 mwezi wa nne ilipoteza watu 6, baada ya siku mbili
tarehe 16 mwezi wa nne 2016 tetemeko likatokea tena na likaua watu 35, mwaka
2012 likaua watu 3, mwaka 2011 likaua watu 15,904 mwaka 2008 likaua watu 12,
mwaka 2007 likaua watu 11, mwaka 2004 likaua watu 40, mwaka 1923 liliua watu
142,800 na hiyo ni Japan. Taarifa imesema ikimkariri Rais Magufuli.
Imesema, shughuli
ya kupokea taarifa ya Waziri Mkuu na michango kwa ajili ya waathirika wa
tetemeko la ardhi lililotokea Mkoani Kagera na Mikoa jirani imehudhuriwa na
viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Balozi Dkt. Augustine Mahiga, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt Suzan Kolimba, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi
John Kijazi, Balozi wa Uganda nchini Tanzania Mhe. Dorothy Hyuha na Naibu
Balozi wa Kenya nchini Tanzania Mhe. Boniface Muhia.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269