Breaking News

Your Ad Spot

Sep 27, 2016

TANZANIA YAITANGAZIA DUNIA VIPAUMBELE VYAKE, YATAKA USHIRIKIANO KATIKA VITA DHIDI YA RUSHWA NA UKWEPAJI KODI

Waziri Dk. Mahiga akitoahotuba
ya Tanzania kwenye Mkutano wa
Baraza Kuu la 71 la UN jana
Na Mwandishi Maalum, New York 
Tanzania jana iliitangazia Dunia vipaumbele vyake na kuiomba Jumuia ya Kimataifa kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya  Tano za kukabiliana na  vitendo vya rushwa ili  zifanikiwe.

Katika kuunga mkono juhudi hizo, Tanzania, inazitaka nchi zilizoendelea kuhakikisha wawekezaji na kampuni hawakwepi kulipa kodi na wanapojaribu kukwepa nchi hizo ziwawajibishe.

Hayo yamesemwa jana  Jumatatu na   Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa  Afrika Mashariki, Dk. Agustine Mahiga,  alipolihutubia  Baraza Kuu la 71 la Umoja wa Mataifa na kutumia  fursa hiyo kuelezea vipaumbele vya Serikali ya Tanzania.

Waziri Mahinga alifafanua kwamba, lengo namba 16 la  maendeleo endelevu linatambua kuwa,  rushwa inakandamiza juhudi za kumbana na  umaskini na   usawa wa jinsia,  inazuia  fursa na inakuwa na kama kodi kwa familia maskini pale wanapotafuta  haki.

Ni katika muktadha  huo,   akasema, serikali  ya  Tanzania imeamua kuanzisha vita dhidi ya rushwa  kwa kuhuisha uwazi, uwajibikani  na usahihi katika utoaji wa huduma  kwenye taasisi za  umma.

Akasisitiza kwamba serikali  imeweka misingi mizuri ya  uwajibikaji inayomtaka mtumishi wa umma kutambua kwamba  wajibu wake wa kwanza ni  kutoa huduma bora na kwa wakati kwa umma.

“Juhudi hizi za serikali za kupambana na rushwa  hazitaweza kuzaa matunda bila ya  kuungwa mkono wa jumuiya ya kimataifa. Nchi zilizoendelea zinatakiwa  kuwawajibisha wawekezaji wao  pamoja na makampuni yao ili  waweze kulipa kodi stahiki.” Akaeleza zaidi  Waziri  Mahinga

Na  kuongeza. “Ni lazima wawe tayari kurudisha mali na fedha  zilizoibwa kutoka nchi zinazoendelea na kuzificha katika nchi zao ili mali  na fedha hizo ziweze kusaidia maendeleo  yetu”.

Kuhusu fursa za jinsia na uwezeshwaji wa wanawake,  Waziri  Mahinga ameelezea juhudi mbalimbali ambazo zimefanywa na serikali katika  kuwawezesha  wawanake ikiwamo kushika ngazi za juu za maamuzi kuanzia serikali kuu  hadi bunge na uwezeshwaji wa  kiuchumi.

katika kudhibitisha kuwa Tanzania  inazingatia usawa wa jinsia katika uteuzi wa ngazi  mbalimbali za maamuzi,  Waziri Mahinga  ameeleza kwamba kwa mara ya kwanza  wakati wa  uchaguzi mkuu wa mwaka 2015,  Rais Dk. John Magufuli  alimchangua mwanamke  kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Uteuzi  huu  unathibitisha nia ya nchi yangu ya kuona wanawake  wengi zaidi wanakuwa katika   nafasi za ngazi za  juu  za maamuzi. Na ajenda hii ya uwezeshwaji wa wanawake wa Tanzania sasa inamilikiwa na wanawake wenyewe” akasisitiza  Waziri.

 Kwa upande wa vijana, Kiongozi huyu wa Ujumbe wa Tanzania ambaye amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  amesema.  Vijana ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya taifa lolote lile, siyo tu kwamba ni viongozi wa kesho lakini pia ni viongozi wa sasa.

Akatahadharisha kwamba kwa  kutowapa kiupaumbele vijana  ni kujitafutia  matatizo makubwa kutokana na kile alichosema ni rahisi  kurubuniwa na makundi ambayo ni hatari kwa ustawi wa jamii na taifa .

“ Kutoka na  kwamba idadi ya vijana ni kubwa,  serikali inachukua hatua mbalimbali za  kuliwezesha kundi hili la jamii ambalo ni muhimu katika utekelezaji wa ajenda 2030. Na ili  vijana   waweze kutekeleza  jukumu hilo  serikali imeanzisha  mfuko wa maendeleo wa  vijana mfuko ambao hadi mwezi March mwaka huu jumla ya  shiling 1.6 bilioni zilipelekwa  kwa vikundi 284 ya  vijana”.

 Kuhusu elimu,  eneo ambalo ni kipaumbele kingine cha Tanzania,   Waziri ameeleza kuwa   upatikanaji wa elimu jumuishi  na ya viwango ndicho kipaumbele cha serikali kwa  kuwa    Serikali inaamini kuwa, elimu ni  ni nyenzo muhimu   kwa maendeleo endelevu.

Akafafanua  kwamba  serikali  inatekeleza bila kuchoka kuhakikisha kwamba  watoto wote wa kike na wa kiume wanapata  elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari. Pamoja na kutoka   elimu bure, serikali imeboresha mitaala yake kwa kuzingatia mahitaji ya karne ya 21.

“Alipoingia madarakani,  Dk.  John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitangaza kwamba   kuanzia elimu ya msingi  hadi sekondari itakuwa bure. Serikali  imetenga zaidi ya  shilingi 263 bilioni ili kuhakikisha elimu  inakuwa bure kwa wote.

Vipaumbele vingine vya  Tanzania ambavyo Mhe. Waziri amevianisha katika  hotuba  yake ni pamoja na  mikakati ambayo  serikali imejiwekea  katika utekelezaji wa mkataba wa mabadiliano ya tabia nchi ( Paris Agreement),  utekelezaji wa   malengo ya maendeleo endelevu ( agenda 2030), mapambano dhidi ya  dawa haramu za kulevya,  na  kukabiliana na  ugaidi ambao  amesema  ni  tatizo ambalo linaendelea kukua na kuwa tishio  hata kwa  nchi za Afrika Mashariki.

Kwa upande wa utekelezaji wa  agenda 2030, Waziri amesema agenda hiyo imeanishwa  katika mipango ya kitaifa ya  miaka  mitano ya  maendeleo  kwa pande zote za muungano.  Hata hivyo  amesema kuwa Tanzania  imebaini kwamba haitaweza kukamilisha kwa  wakati agenda 2030 pasipo kushirikiana na wadau  mbalimbali  wa maendeleo.

Kuhusu  migogoro inayoendelea katika nchi za Burundi na  Sudani ya Kusini, Waziri Mahiga amezitaka pande zote zinazopingana  nchi Burundi kutambua kwamba majadiliano ambayo ni jumuishi kwa pande zote ndiyo  njia sahihi ya kutatua matatizo ya nchi yao.

Kwa upande wa Sudani ya Kusini,  Waziri  amesema Tanzania inaungana na   nchi nyingine kulaani matukio ya hivi karibuni ya kujirudia kwa machafuko nchini humo.

Na kuongeza,  Tanzania ambaye ni  Mwenye -Kiti wa sasa wa  Jumuiya ya  Afrika Mashariki,  iliitisha kikao kisicho cha kawaida ili  kuzungumzia hali ya kisiasa ya Burundi na Sudani ya Kusini. “  Tunatumaini kwamba nchi  zote mbili  zitaweka maslahi  ya wananchi wao mbele ili kumaliza machafuko”.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa  Afrika Mashariki pia aligusia kuhusu marekebisho ya mfumo wa   Baraza  Usalama la Umoja wa Mataifa,  ili liwe jumuishi.

Kwa upande wa   Uchaguzi wa Katibu Mkuu, Waziri amesema, Tanzania  inaunga mkono  hoja ya kuendelea  kuheshimu utaratibu wa kupokezana nafasi ya  Katibu Mkuu kwa kuzingatia mzugunko wa   kijiographia.
 Balozi wa Tanzania nchi Marekani  Wilson  Masilingi, akimpa  mkono wa pongezi Waziri  Mahiga  baada kumaliza hotuba yake mbele ya   wajumbe wa  mkutano wa  71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Anna Lupembe akimpongeza Waziri Mahiga kwa hotuba yake iliyopokelewa vizuri
 Mkurugenzi  Mtendaji wa  ESRF Dk. Tausi Kida,  akimpongeza  Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania  katika Mkutano wa  71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages