Breaking News

Your Ad Spot

Oct 1, 2016

RAIS DK MAGUFULI AWAPA KAZI JESHINI VIJANA 70 WA MGAMBO BAADA YA KUONYESHA UZALENDO

Na Frank Shija, MAELEZO
UZALENDO umewapatia ajira takribani vijana 70 baada ya Amiri Jeshi Mkuu,na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kufurahishwa na namna ambavyo washiriki wa zoezi la Amphibia Landing walivyoonyesha umahiri wao.

Hayo yamebainika jana katika fukwe za kijiji cha Baatani, wilayani Bagamoyo, wakati wa hafla kufunga mazoezi hayo ambapo Mhe. Rais Magufuli alisema kuwa kutokana na alivyojionea mazoezi hayo na amearifiwa kuwa kati ya washiriki wa mazoezi hayo wamo mgambo 30 na JKT 40 aliagiza wote waingizwe kwenye orodha ya waajiriwa wapya wa JWTZ.

“Katibu Mkuu Kiongozi nakuagiza ufanya utaratibu wakuwaingiza kwenye ajira hawa vijana 30 wa mgambo na 40 wa JKT kwani wameonyesha moyo wa uzalendo kwelikweli, tena ikiwezekana ata kesho waingie kwenye orodha ya waajiriwa wapya”. Alisema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli amemuagiza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Davis Mwamunyange kuangalia namna ya kuwapa motishi wote walioshiriki kufanikisha zoezi hilo ili kuwaongezea morali ya kuwajibika.

Katika hatua nyingine ametoa wito kwa Majeshi kushirikia hususan katika eneo la unzanzishaji wa viwanda ili kutoa mchango wao katika hasma ya Tanzania kuwa nchi ya Viwanda.

“Ni lazima sasa tujipange nataka Majeshi yetu muwekeze katika viwanda iwe kwa kuunganishwa nguvu pamoja ama mmoja mmoja naamini hatushindwi, leteni mpango Serikali itasaidia”. Alisema Rais Magufuli.

Alitolea mfano wa Jeshi la Magereza kuwa na kiwanda cha viatu katika Gereza la Karanga mkoani Kilimanjaro, kushangaa kuona majeshi mengine yananunua viatu kutoka nje ya nchini. Aliwaagiza washirikiane katika kuhakikisha wanafikia malengo ya kuwa na viwanda.

Alisema kuwa Jeshi letu limekuwa na mafanikio makubwa katika kutekeleza majukumu yake ambayo aliyataja kuwa ni ulinzi wa mipaka ya nchi, kulinda katiba ya nchi, kufundisha wananchi masuala ya ulinzi wa Taifa, uokoaji na utoaji wa misaada katika maafa, kutoa elimu ya kujitegemea pamoja na ulinzi wa amani na ukumbozi.

Nakuongeza kuwa limeweza  kulinda mipaka ya nchi, na kulinda amani iliyopo pamoja na kushirikiana na Umoja wa Mataifa katika kulinda amani katika baadhi ya maeneo ikiwemo Sudan Kusini na DRC Congo.

Septemba Mosi mwaka huu JWTZ walitimiza miaka 52 ya uhai wake,ambapo ilianza kuadhimsha miaka hiyo kwa kufanya shughuli mbalimbali kama vile usafi, huduma za upimaji wa Afya Bure na zoezi hili la Amphibia Landing ni muendelezo wa maadhimisho hayo.

Ambapo katika zoezi hilo vifaa kama Meli Vita, Vifaru vinavyo tembea nchi kavu na majini, milipuko pamoja na Ndege vita vilitumika.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages