Viongozi wa Ulaya wameonyesha radiamali zao
kufuatia ushindi wa Donald Trump wa chama cha Republican katika uchaguzi
wa Rais uliofanyika jana.
Baada ya Donald Trump kutangazwa kuwa mshindi wa kiti cha urais
nchini Marekani baada ya kutangazwa matokeo ya kura za uchaguzi, Rais
Vladimir Putin wa Russia amemtumia ujumbe Trump akisistiza umuhimu wa
kuhuishwa uhusiano wa nchi yake na Marekani katika kipindi cha uongozi
wa Donald Trump.
Huko nyuma pia Rais Putin alisema kuwa Moscow itashirikiana na
mgombea yoyote ambaye atachaguliwa kuwa Rais wa Marekani. Trump pia
aliahidi kwamba atafanya jitihada kupunguza au kuondoa vikwazo vya miaka
mitatu vilivyowekwa na Marekani na Umoja wa Ulaya dhidi ya Russia
kuhusiana na hali ya mambo ya Ukraine. Wakati huo huo Bi Federica
Mogherini Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa umoja huo
utaendelea kushirikiana na Marekani. Mogherini ametuma ujumbe kwa njia
ya twitter unaoeleza kuwa, uhusiano kati ya Umoja wa Ulaya na Marekani
ni mkubwa zaidi kuliko badiliko lolote la kisiasa. Nao wanachama wa
ngazi ya juu wa chama cha Kihafidhina cha Ujerumani wameutaja uchaguzi
wa Marekani kuwa ulioshtua.
Naye
Jean- Pierre Rafarrin Seneta wa mrengo wa kulia wa Ufaransa ametoa
radiamali yake kufuatia ushindi wa Trump na uungaji mkono wa mwanasiasa
Marine Le Pen kwa ushindi wa mgombea huyo wa chama cha Republican kwa
kusema, 'katika mazingira kama haya tutaraji pia ushindi wa mrengo wa
kulia wenye misimamo mikali katika uchaguzi wa Rais wa Ufaransa wa mwaka
kesho.'
Donald
Trump amesema leo baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa Rais wa
Marekani kuwa, hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa ili kuijenga upya
Marekani na kwamba ushirikiano wa wananchi pia unahitajika ili kupambana
na matatizo ya kiuchumi nchini humo. Rais mteule wa Marekani ameongeza
kuwa wanawake na wanaume waliosahaulika nchini humo, hivi sasa
hawatasahaulika tena.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269