Wizara ya usalama wa ndani ya Marekani imetangaza
sheria mpya zitakazowalenga wahamiaji wasiokuwa na vibali. Inakadiriwa
kuwa kuna watu milioni 11 nchini humo wasiokuwa na vibali.
Utawala wa rais wa Marekani Donald Trump, umetangaza amri mpya juu ya
wahamiaji haramu.Sheria hizo kali zinalenga kuwaandama wageni wanaoshi
nchini humo bila vibali rasmi, hatua ambayo itawaweka matatani watu
milioni 11 wanaoishi nchini humo bila vibali.
Amri hizo zimeibua
wasiwasi mwingi miongoni mwa mamilioni ya jamii ya wahamiaji, ambao kwa
miaka mingi wameishi nchini humo wakikuza jamii zao na kuendeleza
maisha. Lakini kwa mara ya kwanza baada ya miongo mingi, watu hao ambao
wengi wao wanatokea Mexico na America ya kati sasa wameingiwa na khofu
kutokana na uwezekano wa kufurushwa.
Sheria hizo mpya
zitawawezesha maafisa wanaoshika doria katika mipaka na maafisa wa
uhamiaji kumfurusha mhamiaji yeyote asiyekuwa na kibali.
Sheria
hizo hazitawalinda baadhi ya watu jinsi ilivyokuwa katika utawala wa
Barrack Obama, bali wote wanaokiuka sheria wanaweza kulengwa kwenye
mchakato wa kufurushwa. Kadhalika wazazi ambao walitumia wanaofanya
biashara ya kuwaingiza watu kimagendo nchini Marekani kuingiza watoto
wao pia wanaweza Kukabiliwa na sheria.
Waziri wa mambo ya ndani
anayehusika na usalama John Kelly, amesema amri hizo ni muhimu katika
kukabiliana na matatizo aliyosema yamepindukia uwezo wa rasilmali za
serikali.
Maafisa na mawakala wa mpakani katika kituo cha San Ysidro, California
Sean
Spicer ambaye ni msemaji wa Ikulu amesema sheria hizo zinaeleza
mikakati na sera za kuimarisha usalama kulingana na sheria za uhamiaji.
"Ilani kuhusu amri ya usalama wa mipaka na uimarishaji wa sheria za
uhamiaji zinaleza hatua ambazo wizara ya usalama izachukua kulinda
mipaka ya kusini mwa nchi, kuzuia uingiaji zaidi wa wahamiaji na
kuwarudisha makwao wahamiaji wasiokuwa na vibali kwa njia ya
kibinadamu."
Pingamizi dhidi ya amri hizo
Mashirika
ya kutetea haki za binadamu yametaja hatua hiyo kama uonevu na kuonya
kuwa kuwafurusha watu wengi kutaathiri familia ambazo mizizi yao
imejikita nchini Marekani. Halikadhalika kutaathiri uchumi wa nchi hiyo.
Seneta
Ben Cardin wa chama cha Democrats ameonya kuwa sheria hizo zitaathiri
usalama wan chi na umma, huku Meya wa New York Bill De Blasio akisema
hawezi kuwageuza maafisa wa polisi wa jiji kuwa mawakala wa uhamiaji
wala kuiunga mkono sera ambayo mwisho wake itaathiri umoja ambao
umesaidia kukuza usalama wa jiji hilo.
Ili kufanikisha juhudi
hizo, serikali itawaajiri maafisa 10,000 wa uhamiaji na mawakala 5,000
kushika doria mipakani. Sheria hizo ni kulingana na amri za Rais Donald
Trump punde tu baada ya kuapishwa kuwa rais, kwamba maafisa waimarishe
usalama na wawakabili wahamiaji wasiokuwa na vibali na kuamuru kujengwa
ukuta kati ya Marekani na Mexico. Katika sheria hizo, waziri Kelly
ameamuru kuwa mipango ya kujengwa kwa ukuta ianze.
Hatua hii
inajiri kabla rais wa Mexico Enrique Pena Nieto kukutana na waziri wa
nchi za nje wa Marekani Rex Tillerson na mwenzake wa mambo ya ndani John
Kelly.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269