Viongozi wa ngazi ya juu wa kidunia, wanadiplomasia na
maafisa wa masuala ya ulinzi wanakutana kwa mara ya kwanza na maafisa wa
utawala mpya wa Marekani chini ya Rais Donald Trump mjini Munich.
Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence, waziri wa ulinzi Jim Mattis na
waziri wa nchi hiyo wa mambo ya ndani John Kelly wanaoongoza ujumbe wa
Marekani katika mkutano unaohusu masuala ya ulinzi unaoanza leo mjini
Munich, Ujerumani.
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, Rais wa Baraza la Ulaya,
Donald Tusk, na Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg, ni miongoni mwa
viongozi wanaotarajiwa kushiriki mkutano huo ambao unatarajiwa
kuhudhuriwa na viongozi wa nchi zaidi ya 30 pamoja na mawaziri 80 wa
wizara ya mambo ya nje na ulinzi pamoja na maafisa kadhaa.
Mkutano
huo unafanyika mnamo wakati Rais Trump akiwa tayari ametoa kauli kadhaa
kuhusiana na Jumuiya hiyo ya kujihami ya nchi za magharibi na hivi
karibuni akitoa kauli inayooonyesha kukubaliana na umuhimu wa
ushirikiano huo wa kijeshi. Hata hivyo, amesisitiza juu ya haja ya kila
nchi mwanachama wa ushirikiano huo kulipa gharama sawa zinazohusiana
na masuala ya ulinzi jambo ambalo viongozi wa NATO wamekuwa
wakilipigania kwa muda mrefu.
Marekani yaunga mkono ushirikiano wa NATO
Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence
Waziri
wa Ulinzi wa Marekani, Jim Mattis, aliawaeleza mawaziri wa ulinzi wa
nchi nyingine 27 zinazounda Jumuiya ya NATO jumatano wiki hii mjini
Brussels kuwa Rais Trump anaunga mkono kwa kiwango cha juu NATO na
Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg, juu ya umuhimu wa ushirikiano huo
wa NATO kwa Marekani.
Aidha waziri huyo wa ulinzi wa Marekani
aliwaeleza washirika wenzake katika NATO kuwa wanapaswa kuongeza gharama
za matumizi yao kijeshi kufikia mwishoni mwa mwaka huu vinginevyo
huenda Marekani ikapunguza mchango wake kifedha katika NATO.
Masuala
mengine ambayo yanaibua maswali mengi ni kuhusiana na hatua ya Rais
Trump kuunga mkono hatua ya Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya,
ukaribu wake na Urusi na ahadi yake ya Marekanani kwanza. Alisema
muandaaji wa mkutano huo Wolfgang Ischinger ambaye ni balozi wa zamani
wa Ujerumani nchini Marekani.
Ischinger amesema matarajio ya
Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence, kuzungumza hapo kesho katika
mkutano huo ni makubwa sana. Washiriki wa mkutano huo wamesema
wanatarajia kupata ufafanuzi kutoka kwa makamu huyo wa Rais wa Marekani
kuhusiana na msimamo wa Marekani juu ya uhusiano wake na Urusi, suala
la NATO, Umoja wa Ulaya, biashara huru, masuala ya haki za binadamu na
makubaliano ya nyukilia kuhusu Iran.
Masuala mengine ni pamoja na
suala linalohusu ushirikiano kati ya Marekani na China na pia mgogoro
wa Syria ambayo washiriki wa mkutano huo wanatarajia kupata majibu
kuhusiana na maswali yaliyoibuka kuhusiana na msimamo wa Marekani katika
masuala hayo.
Kansela Merkel ambaye anatofautiana kwa hoja na
msimamo wa Rais Trump katika masuala hayo anatarajiwa pia kuhutubia
mkutano huo hapo kesho.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269