Hatua ya Jeshi la Yemen ya kuvurumisha kwa
mara ya kwanza kombora la balistiki katika kituo cha kijeshi katika mji
mkuu wa Saudia Arabia, Riyadh ni jambo ambalo limeibua mshtuko mkubwa
katika ukoo wa Aal Saud unaotawala ufalme huo.
Usiku wa kuamkia Jumatatu ya jana, kombora la kisasa la
balistiki la Jeshi la Yemen lililenga kituo cha kijeshi katika eneo la
al-Mazahamiah mjini Riyadh. Shambulizi hilo la kwanza la aina yake
limeibua mshtuko, hofu na wahka katika Ufalme wa Saudia. Kwa mujibu wa
tovuti ya Al-Najmul Thaqib, Mwanamfalme Mohammad bin Salman, Naibu
Mrithi wa Kiti cha Ufalme na Waziri wa Vita wa Saudia ameitisha kikao
cha dharura na rais aliyejizulu wa Yemen Abdu Rabuh Mansour Hadi
kufuatia hujuma hiyo iliyolenga Riyadh.
Ni karibu miaka miwili sasa tokea Saudia inazishe hujuma ya kidhalimu
dhidi ya Yemen ambapo karibu Wayemen 12,000 wameuawa na makumi ya
maelfu ya wengine kujeruhiwa. Hivi sasa inaelekea kuwa mlingano wa vita
vya Yemen unabadilika na moja ya ishara hizi ni hujuma hiyo ya Jeshi la
Yemen dhidi ya kituo cha kijeshi katika vitongoji vya mji mkuu wa
Saudia, Riyadh.
Shambulizi hilo lililofanikiwa lina ujumbe muhimu sana. Kombora hilo
la balistiki ambalo lililenga kituo cha kijeshi cha al-Mazahamiah lina
uwezo wa kuruka umbali wa kilomita 800 sambamba na kuwa na uwezo mkubwa
wa kuharibu eneo linalolengwa. Kombora hilo ambalo limetajwa kuwa Borkan
1 linaliwezesha Jeshi la Yemen kulenga kwa urahisi Riyadh, mji mkuu wa
Saudia.
Taarifa ya pamoja iliyotolewa na Kitengo cha Makombora katika Jeshi
la Yemen na Kamati za Kujihami za Wananchi wa Yemen imesema kombora
hilo limevurumishwa Riyadh kama njia ya kujibu na kulipiza kisasi hujuma
na jinai zisizo na kikomo za utawala wa Aal Saud dhidi ya watu wa
Yemen. Taarifa hiyo imetahadharisha kuwa shambulizi lijalo litakuwa kali
zaidi. Kwa maneno mengine ni kuwa, kuanzia sasa Saudi Arabia haitakuwa
mvamizi tu bali pia italazimika kujilinda kutokana na mashambulizi ya
Wayemen wanaolipiza kisasi.
Hali kadhalika taarifa hiyo ya vikosi vya ulinzi Yemen imesema kujihami ni haki ya kisheria ya Wayemen.
Hujuma ya Saudia dhidi ya Yemen imesababisha vifo vya Wayemen zaidi
ya 12,000 wengi wao wakiwa ni raia wa kawaida hasa wanawake na watoto,
huku wengine zaidi ya 35,000 wakijeruhiwa vibaya na asilimia 80 ya
miundomsingi ya nchi hiyo kuharibiwa sambamba na mamilioni ya watu kuwa
wakimbizi. Ukatili na unyama huo wa Saudia dhidi ya Yemen kwa hakika ni
jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu na kwa msingi huo hatua ya
Jeshi la Yemen na Kamati za Kujihami za Wananchi ya kuvurumisha kombora
la balistiki mjini Riyadh ni mfano wa wazi wa 'haki ya kisheria ya
kujihami'. Hii ni haki ambayo imebainishwa wazi katika kipengee cha 51
cha Hati ya Umoja wa Mataifa.
Jambo lenye umuhimu mwingine hapa ni hili kuwa, Mansour Hadi, rais wa
Yemen aliyejiuzulu na kutoroka nchi kwa mara nyingine ameonyesha
usaliti wake kwa watu na nchi ya Yemen.
Katika hali ambayo ndege za kivita za Saudia zimedondosha mabomu
katika maeneo mbali mbali ya Yemen kama njia ya kubainisha hasira baada
ya kushambuliwa mji wa Riyadh, Mansour Hadi anayeishi uhamishoni mjini
humo amekutana na Mohammad Bin Salman na kuishukuru Saudia kwa kuendelea
kuunga mkono serikali yake iliyojiuzulu. Pamoja na uhaini wake huo,
Mansour Hadi angali anajitambua kuwa eti ndiye rais halali wa Yemen!
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269