Spika wa Bunge la Uingereza John Bercow, amesema rais wa Marekani
Donald Trump hafai kualikwa kulihutubia bunge hilo wakati atakapofanya
ziara rasmi nchini humo.
Matamshi hayo ya Spika John Bercow (pichani) yanaondoa uwezekano kwa Trump
kupewa heshima hiyo wakati wa ziara yake baadae mwaka huu. Bercow
aliwambia wabunge kwamba angepinga mwaliko huo hata kabla ya marufuku
ya Trump inayowazuwia raia kutoka mataifa saba yenye Waislamu wengi
kuingia nchini Marekani.
"Kabla ya kuwekwa marufuku ya uhamiaji,
binafsi ningepinga vikali kuruhusiwa rais Trump kutoa hotuba katika
ukumbi wa Westminster. Baada ya kuwekwa kwa marufuku ya uhamiaji na rais
Trump, ninapinga hata vikali zaidi hotuba ya rais Trump katika ukumbi
wa Westminster," alisema Bercow bungeni siku ya Jumatatu.
Matamshi
ya Bercow hayakuwa ya kawaida kwa sababu maspika wa bunge la Uingereza
wanatarajiwa kutoegemea upande wowote wa kisiasa. Ni mmoja wa maafisa wa
bunge ambao wangekubali kumualika mgeni wa nje kuwahutubia wabunge.
Viongozi
wa dunia waliowahi kupewa heshima ya kutoa hotuba kwa mabaraza yote ya
bunge ni pamoja na Nelson Mandela, na mtangulizi wa Trump Barack Obama.
Bercow
alishangiliwa na wabunge pale aliposema kwamba, inagwa Uingereza
inathamini uhusiano wake na Marekani, "upinzani wetu dhidi ya ubaguzi wa
rangi na kijinsia, na uungwaji wetu wa usawa mbele ya sheria na
mahakama huru, ni mambo yenye umuhimu mkubwa zaidi.
Trump atazuru
Uingereza kama mgeni wa Malkia, ziara iliotangazwa na waziri mkuu
Theresa may alipomtembelea Trump mjini Washington mwezi uliopita.
Lakini
baadhi ya raia wameonyesha mashaka na uharaka wa serikali kuwa karibu
na rais huyo mwenye kuchochea mgawanyiko. waraka wa mtandaoni unaopinga
ziara ya Trump umesainiwa na zaidi ya watu milioni 1.8, na utajadiliwa
bungeni Februari 20.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269