Maafisa wawili wa ngazi ya juu wa Umoja wa
Mataifa wamesema kuwa, zaidi ya Waislamu 1000 wa kabila la Rohingya
wameuawa katika operesheni za jeshi la Myanmar kaskazini mwa nchi hiyo.
Maafisa hao wa UN ambao wanafuatilia wimbi la Waislamu
wanaokimbia kutokana na ukatili unaoendelea dhidi yao nchini Myanmar
wamesema kuwa, takwimu za uharibifu unaotokana na operesheni za jeshi la
nchi hiyo, ni zaidi ya kiwango kilichotajwa awali na serikali hiyo. Hii
ni katika hali ambayo viongozi wa serikali wamedai kuwa, tangu
kulipotekelezwa operesheni hizo katika mkoa wa Rakhine mwaka jana, watu
wasiofikia 100 ndio waliouawa.
Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Haki za
Binaadamu, sanjari na kutoa ripoti inayohusiana na ukatili wa kutisha wa
askari wa Myanmar dhidi ya Waislamu imesema kuwa, askari hao walihusika
na mauaji dhidi ya watoto wachanga, watoto wadogo, wanawake, wazee
pamoja na kuwanajisi wanawake. Kabla ya hapo serikali ya Myanmar
ilikadhibisha tuhuma hizo na kutaka ufanyike uchunguzi kuhusiana na
suala hilo. Hata hivyo maafisa wa serikali hawakuziruhusu timu za
uchunguzi kufika eneo la tukio kwa khofu ya kufichuliwa ukatili huo.
Wakati huo huo Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani amelaani jinai
wanazofanyiwa Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar. Papa
Francis, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani ameyasema hayo jana na
kuongeza kuwa, Waislamu wa Myanmar wananyanyaswa kwa miaka mingi sasa na
wanauawa na kuteswa kinyama kwa sababu tu ya kutaka waishi kwa mujibu
wa utamaduni na mafundisho ya dini yao.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269