Benki ya ABC imeendelea kupanua wingo wake kwa kufungua tawi lake jipya eneo la Tegeta jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuhudumia ongezeko la idadi ya wateja katika eneo hilo, hatua ambayo inaifanya sasa Benki hiyo kuwa na jumla ya matawi matano hapa nchini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa tawi hilo, Waziri wa Fedha na Mipango Philip Mpango alisema ni uamuzi mzuri kwa kupeleka huduma za kibenki kwenye maeneo ya nje ya jiji la Dar es Salaam kwa kuwa huduma nyingi za kibenki zinapatikana kati kati ya jiji la Dar es Salaam. ‘Nachukua fursa hii kuwapongeza uongozi wa benki ya ABC kwa kuja na mbinu hii ya kufungua tawi lenu hapa Tegeta. Ni vizuri kufahamu ya kwamba maeneo kama haya ndio yenye Watanzania wengi ambao wanahitaji huduma za kibenki na hivyo inakuwa ni rahisi kuwafikia wale ambao bado hawana huduma hizo,’ alisema Mpango.
Akiongea kuhusu huduma zitolewazo na benki hiyo, Waziri Mpango alionyesha kuridhishwa kwake kwamba benki hiyo inatoa huduma kwa zaidi ya wafanyakazi 60,000 wa serikali kwa kuwapa mikopo pamoja fursa ya kuwekeza. ‘Kwa jinsi mnavyohudumia wafanyakazi wa serikali, fanyeni hivyo hivyo kwa sekta binafsi na watawaamini na kutumia huduma zenu’, aliongeza Mpango.
Mpango alitoa wito kwa Watanzania kujiwekea utaratibu wa kujiwekea akiba kwani ndio njia pekee kwa mtu kuweza kutimiza malengo yake. ‘Kuweka akiba kuna faida nyingi zikiwemo kufikia malengo lakini pia inajenga imani kwa benki pale mtu atapohitaji kupata mkopo. Waziri Mpango pia alitoa wito kwa benki ya ABC pamoja na taasisi zingine za fedha kufikiria kupunguza riba ya mikopo kwani ni Watanzania wengi ambao wamekuwa na nia ya kukopa lakini riba kubwa kwenye mikopo hiyo imekuwa ikiwakatisha tamaa.
Aliwaomba Watanzania pia kujijengea utaratibu wa kulipa mkopo kwa wakati pale wanapokopa kwani kwa kufanya hivyo kunazidi kujiongezea imani na pia inatoa fursa kwa wengine kukopa.
Akiongea kwenye uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya ABC Dana Botha alisema kufungua tawi la Tegeta ni hatua kubwa ya kuleta huduma za kibenki karibu na wananchi. Hii ni hatua kubwa kwetu benki ya ABC kufungua tawi hapa Tegeta kwani kunaendana na malengo yetu ya kuwafikia wananchi kwa karibu na kuwa moja ya benki zenye mafanikio katika nchi ambazo tunafanya biashara, alisema Botha.
Botha aliwaomba wakazi wa Tegeta pamoja na maeneo ya karibu kuchukua fursa ya benki kuwa karibu nao na kupata huduma zote za kibenki. ‘Sisi kama taasisi tumekuwa tukifanya kazi kwa bidii kufanikisha malengo yetu. Hii ndio sababu tunaendelea kukua na kwa mwaka 2017 benki yetu imeshinda 2017 Banker Afrika, Southern Africa Awards as the Best Emerging Bank – Southern Africa. Ushindi wetu utatokana na kura ambazo zitapingwa na wateja pamoja na wale wote wote waliojisajili. Hii imekuwa moja ya malengo yetu kuendelea kushinda tuzo nyingi zaidi kwa ubora wa huduma zetu, alisema Botha.
Benki ya ABC pia ina malengo ya kujitanua zaidi kwa kufungua matawi mengine mawili kwenye mikoa ya Dodoma na Mwanza kwa mwaka huu.
Waziri wa Fedha na Mipango Philip Mpango akimpongeza Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya ABC Tanzania Jonas Kapolo, baada ya kuzindua tawi la benki hiyo Tegeta, Dar es Salaam, jana. Wapili kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Dana Botha.
Uzinduzi ukiendelea
Uzinduzi ukiendelea
Waziri wa Fedha na Mipango Philip Mpango akipokea maelezo ya jinsi ya kufungua akaunti kutoka kwa Meneja Huduma kwa wateja wa benki ya ABC ya kufungua tawi jipya la Tegeta la benki hiyo jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269