Na Veronica Simba – Singida
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amewataka wananchi wote, hususan
wanaounganishiwa huduma ya umeme vijijini, kufanya malipo husika katika Ofisi za
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) peke yake na siyo kwa mtu mwingine yeyote.
Aliyasema
hayo hivi karibuni kijijini Mkwese, Wilaya ya Manyoni wakati akizindua Mradi
Kabambe wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) katika Mkoa wa
Singida.
Profesa
Muhongo alisema kuwa wananchi wengi wamekuwa wakitapeliwa na watu mbalimbali
kwa kuombwa rushwa ili waunganishiwe umeme au kulipishwa gharama zaidi ya zile
zinazostahili, na baada ya kufuatilia, imebainika kuwa wanaofanya utapeli ni
watu wasiohusika kabisa na uunganishaji umeme.
Ili
kuepuka utapeli huo, Waziri Muhongo amewataka wananchi kufahamu taratibu
zinazopaswa kufuatwa wakati wa kuunganishiwa umeme ikiwa ni pamoja na kujua
kiasi wanachopaswa kulipia na ni nani wa kumlipa.
Aidha,
aliitaka Tanesco kuhakikisha inaendelea na zoezi la kutoa elimu kwa umma kuhusu
huduma zote wanazotoa ili wananchi wawe na uelewa wa kutosha na hivyo kuepuka
kutapeliwa.
Alisema
kuwa, baadhi ya wananchi wanadhani kuwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ndiyo
wenye jukumu la kuchukua malipo kutoka kwa wananchi wanaounganishiwa umeme
vijijini.
“Anayepokea
malipo yote ya umeme ni Tanesco. Siyo REA wala Wizara. Wananchi mjue hilo.
Mwingine yeyote akidai malipo ya umeme, kataeni,” alisisitiza.
Waziri
Muhongo aliwataka Wakuu wa Wilaya mbalimbali kuhakikisha wanamkamata na kumweka
ndani mtu yeyote anayepita katika maeneo yao na kudai malipo ya umeme kutoka
kwa wananchi wakati siyo Ofisa wa Tanesco.
“Mambo
ya malipo yote yanafanywa Tanesco. Wala huyu Mkandarasi hakusanyi fedha. Kama ataomba
fedha za kuunganishia watu umeme au za nguzo, huo ni wizi na utapeli. Lazima
mumshtaki.”
Akielezea
kuhusu utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, Profesa Muhongo alisema kuwa
dhamira ya Serikali ni kuhakikisha inaundoa umaskini wa wananchi kwa kuwapatia
huduma muhimu ikiwemo umeme.
“Injini
mojawapo nzuri na muhimu ya kuondoa umaskini wetu ni kuhakikisha tunakuwa na
umeme wa uhakika, unaotabirika na wa bei nafuu.”
Alisema,
Serikali inatambua kuwa wananchi walio wengi wanaishi vijijini ndiyo maana Bajeti
ya Wizara ya Nishati na Madini ambayo inaishia mwezi wa sita mwaka huu, fedha
zake nyingi zilipelekwa kwenye miradi hususan ya umeme vijijini.
Profesa
Muhongo alisema kuwa, ili kuwapunguzia wananchi gharama ya kufuata huduma ya
kuunganishiwa umeme kwenye Ofisi za Tanesco ambazo ziko mbali, Serikali
imeagiza maafisa wa shirika hilo kutangaza tarehe watakapofika kugawa fomu za
kujiandikisha pamoja na vituo vitakavyotumika kufanyia malipo.
Alitoa
rai kwa Serikali za Vijiji kutoa ushirikiano kwa Tanesco, ikiwezekana kuwapatia
chumba au Ofisi ya kutolea huduma kwa siku watakazopanga kutoa huduma katika
vijiji husika.
Waziri
Muhongo alieleza kuwa, kwa Mkoa wa Singida, Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini
Awamu ya Tatu utatekelezwa kwa vipindi viwili tofauti ambapo sehemu ya kwanza
itahusisha upelekaji umeme katika vijiji 185 kwa gharama ya shilingi bilioni
47.36. Aliongeza kuwa utekelezaji wa sehemu hiyo ya kwanza umeanza mwezi
Februari mwka huu na unatarajiwa kukamilika ifikapo Machi 2019.
Alimtaja
Mkandarasi Nakuroi Investment Co. Ltd ambaye alimtambulisha pia kwa wananchi na
kumkabidhi kwa viongozi wa Serikali na Wabunge wa Singida, kuwa ni mmoja wa makandarasi
watakaoshiriki katika utekelezaji wa Mradi husika katika Mkoa huo.
Aidha,
Profesa Muhongo alieleza kuwa, sehemu ya pili ya mradi huo mkoani Singida,
itaanza kutekelezwa baada ya sehemu ya kwanza kukamilika mwaka 2019 ambapo
vijiji 82 vitapatiwa umeme na hivyo kufikisha umeme katika vijiji vyote vya
Mkoa wa Singida ifikapo Mwaka 2021.
Uzinduzi
wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu kwa Mkoa wa Singida
ulihudhuriwa na wananchi, viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na baadhi ya
wafadhili wa Mradi husika ambao ni Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Katarina
Rangnitly na Balozi wa Norway nchini, Hamme Hanie Kaarstad.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269