Na Daudi Manongi-MAELEZO.
Tanzania
inategemea kupata Megawati 400 za umeme kutoka Ethiopia ikiwa ni moja
ya makubaliano yaliyofikiwa baada ya ziara ya kikazi ya siku mbili ya
Waziri Mkuu wa Ethiopia Mhe.Haile Mariam Desalegn.
Hayo
yamesemwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt John Pombe
Magufuli alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari juu ya makubaliano
na mikataba ambayo nchi za Tanzania na Ethiopia wametiliana saini leo
Ikulu Jijini Dar es Salaam.
“Tukitaka
kujenga uchumi wa viwanda ni lazima tuwe na umeme wa kutosha,wenzetu
Ethiopia wametuonyesha njia na mimi nimemuomba Mhe.Waziri atusaidie
wataalamu kutoka nchini kwake ili waje tuwaonyeshe maeneo mbalimbali
watusaidie katika kupata umeme wa uhakika kwa kujenga mabwawa ya umeme
ambayo yamesaidia sana katika kupatikana kwa umeme wa kutosha nchini
kwao.”Aliongeza Rais Magufuli.
Aidha
amesema kuwa kupatikana kwa umeme huo kutasaidia kuleta changamoto kwa
shirika la umeme nchini katika kuwapatia wananchi bei ya chini na hivyo
kuleta ushindani katika upatikanaji wa umeme nchini.
Kwa
upande wake Waziri Mkuu wa Ethiopia Mhe.Haile Mariam Desalegn amesema
kuwa wana mengi ya kujifunza kutoka Tanzania kwani nchi hizi mbili zina
historia inayofanana na kuongeza kuwa hakuna haja ya wao kwenda nje ya
Afrika kupata uzoefu katika masuala mbalimbali.
Ameongeza
kuwa lengo kuu la kuja nchini ni kwa sababu anahamini nchi hizi mbili
zinaweza kuunganisha nguvu zake na kuwa nguzo kuu katika maendeleo
katika eneo la ukanda wa Afrika Mashariki na kati.
“Tanzania
na Ethiopia ni nchi ambazo zina ushirikiano mzuri sana,sisi sio
washindani bali tunasaidiana katika masuala mbalimbali kwani tumekuwa
katika hatua mbalimbali za kuwaondoa wananchi wetu katika umaskini
katika hatua zinazofanana,na huu ni wakati muafaka katika kuimarisha
ushirikiano wetu kwa faida ya watu wetu kwa ujumla”Alisisitiza
Mhe.Desalegn.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269