HOTUBA YA MHESHIMIWA DK. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA 33 WA JUMUIYA YA
TAWALA ZA MITAA TANZANIA (ALAT), KATIKA UKUMBI WA MWALIMU JULIUS
NYERERE, DAR ES SALAAM, TAREHE 03 OKTOBA, 2017
Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu
wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Gulamhafeez Mukadamu, Mwenyekiti wa ALAT
na Mstahiki Meya wa Manispaa ya
Shinyanga,
Mheshimiwa Stephen Peter Mhapa, Makamu Mwenyekiti
wa ALAT
na Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Wilaya ya Iringa,
Mheshimiwa Seleman Jafo, Naibu Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais-TAMISEMI;
Mheshimiwa Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam;
Waheshimiwa
Wabunge mliopo hapa;
Wastahiki Mameya wa Majiji na Manispaa pamoja na
Waheshimiwa Wenyeviti wa
Halmashauri za Miji na Wilaya;
Waheshimiwa
Madiwani wa Dar es Salaam, mkiongozwa
na Mstaiki
Meya Isaya Mwita;
Mstahiki Meya wa Zanzibar pamoja na Viongozi
mbalimbali
kutoka Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar;
Mhandisi Mussa
Iyombe, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI;
Prof. Faustin
Kamuzora, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais;
Bwana Abdallah
Ngodu, Kaimu Katibu Mkuu wa ALAT;
Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa, Miji
na Halmashauri za Wilaya;
Wawakilishi wa
Jumuiya za Serikali za Mitaa kutoka
Nchi za Afrika
Mashariki mliopo;
Wawakilishi wa
Wadhamini kutoka Makampuni
na Mashirika
ya Serikali na Yasiyo ya Kiserikali,
Wawakilishi wa
Vikundi vya Wajasiriamali;
Ndugu Waandishi wa Habari;
Wageni
Waalikwa, Mabibi na Mabwana:
Napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wetu, ambaye ametupa
uhai na kutuwezesha kukutana hapa. Aidha, nakushukuru sana Mwenyekiti wa Jumuiya
ya Tawala za Serikali za Mitaa Tanzania (Association of Local Government Authorities
of Tanzania – ALAT), Mheshimiwa Mukadamu, kwa kunialika kufungua Mkutano huu Mkuu wa 33 wa
ALAT. Nasema Ahsante sana.
Natambua baadhi yenu hapa mmesafiri umbali mrefu kuja kuhudhuria
Mkutano huu, ambao awali ulipangwa kufanyika Jijini Mbeya, lakini siku za
mwishoni ukalazimika kuhamishiwa hapa Dar es Salaam. Hivyo basi, kwanza,
napenda kuwapa pole kwa uchovu wa safari. Lakini pili, kama mnavyofamu, mimi
pamoja na kuwa na majukumu ya Urais, nina dhamana kwenye Wizara ya TAMISEMI;
hivyo basi, napenda niwakaribishe wajumbe wote hapa Dar es Salaam na katika
Mkutano huu wa 33 wa ALAT. Karibuni sana ndugu wajumbe.
Napenda pia hapa mwanzoni kabisa nimshukuru Mwenyekiti wa ALAT Taifa
kwa salamu za pongezi alizozitoa kwangu, hususan kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa
Awamu ya Tano wa nchi yetu. Namshukuru pia kwa pongezi zake kuhusu utendaji
kazi wa Serikali ya Awamu ya Tano. Nasema ahsante sana. Mmezidi kutupa moyo wa
kuendelea kufanya kazi kwa bidii. Lakini nami ningependa kutumia fursa hii kuwapongeza,
wewe Mheshimiwa Mwenyekiti na Makamu wako, Wastahiki Mameya wa Majiji na
Manispaa pamoja na Wenyeviti wa Halmashauri zote nchini kwa kuchaguliwa kwenu.
Napenda niwaahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itashirikiana nanyi kwa karibu
katika kuhakikisha tunaleta maendeleo kwa wananchi na nchi yetu kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ndugu Wajumbe, Mabibi
na Mabwana;
Kwangu mimi, Mkutano huu ni muhimu sana. Ni muhimu kwa sababu, kama
mnavyofahamu, ALAT ni chombo kinachounganisha pamoja mamlaka na wadau
mbalimbali wanaohusika na masuala ya Serikali za Mitaa hapa nchini. Na sote
hapa tunatambua kuwa Serikali za Mitaa ni mamlaka ambazo zipo karibu zaidi na
wananchi. Kwa sababu hiyo, binafsi naona kuwa hii ni fursa nzuri kwangu
kuzungumza kwa kina na Watanzania wenzangu; na hasa kwa kuzingatia kuwa hii ni
mara yangu ya kwanza kuhudhuria Mkutano huu wa ALAT, tangu nimechaguliwa kuwa
Rais wa Awamu ya Tano wa nchi yetu. Hivyo basi, nina imani Mheshimiwa
Mwenyekiti pamoja na ndugu wajumbe mtaniruhusu, kabla ya kuzungumzia masuala
yaliyotuleta hapa, kueleza hatua mbalimbali ambazo tumechukua tangu tumeingia
madarakani pamoja na mipango na mikakati tuliyonayo ya kuleta maendeleo kwa
nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti
na Ndugu Wajumbe;
Tangu tumeingia madarakani, takriban miezi 23 iliyopita, tumefanya
mambo mengi ya kuleta maendeleo kwa nchi yetu. Mtakumbuka, tulianza kwanza
kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kudhibiti ubadhirifu wa mali za umma.
Tulibana mianya ya ukwepaji kodi na hivyo kutuwezesha kuongeza ukusanyaji wa
mapato kutoka wastani wa shilingi
bilioni 850 kwa mwezi hadi kufikia shilingi
trilioni 1.3. Sambamba na kuongeza ukusanyaji mapato, tuliamua kudhibiti ubadhirifu
wa mali za umma. Tumezuia safari za nje, warsha na semina zisizo na tija. Hivi
majuzi tu mmesikia kuwa ujumbe wetu kwenye Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
ulikuwa na watu watatu tu na
walituwakilisha vyema.
Kutokana na kuongeza mapato na kubana matumizi, hivi sasa tunawalipa
mishahara ya watumishi wetu kwa wakati. Aidha, tumeweza kulipa madai mbalimbali
ya watumishi, ikiwa ni pamoja na michango yao kwenye mifuko ya hifadhi ya
jamii. Zaidi ya hayo, tumeweza kuongeza bajeti yetu ya maendeleo kutoka wastani
wa asilimia 26 hadi kufikia wastani
wa asilimia 40 hivi sasa.
Hii ndiyo imetuwezesha kupanua wigo na kuboresha huduma mbalimbali za jamii,
hususan elimu, afya na maji. Kama mnavyofahamu, kwenye elimu, baada ya kuingia
madarakani, tulianza kutoa elimu bila malipo kuanzia shule ya msingi hadi
sekondari, ambapo mwanzoni tulikuwa tukitenga kila mwezi shilingi bilioni 18.77. Mwezi Julai 2016, kiasi hicho kiliongezwa
hadi kufikia shilingi bilioni 23.868,
na hivyo kufanya hadi mwezi Agosti mwaka huu, kuwa tumetumia kiasi cha shilingi bilioni 465.6 kugharamia elimu
bila malipo. Matokeo yake, bila shaka, nyote hapa mnafahamu. Idadi ya wanafunzi
wanaoanza darasa la kwanza na kidato cha kwanza imeongezeka maradufu; darasa la
kwanza kwa takriban asilimia 90 na
kidato cha kwanza takriban asilimia 25.
Tumeongeza pia idadi ya wanafunzi wa elimu ya juu wanaopata mikopo kutoka
98,300, wakati tunaingia madarakani,
hadi kufikia takriban 125,000. Hii imewezekana baada ya kuongeza bajeti
ya mikopo kutoka shilingi bilioni 365
hadi kufikia shilingi bilioni 483.
Kwenye afya, nako tumeimarisha na
kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo. Tumeongeza bajeti ya kununua madawa
kutoka shilingi bilioni 31 wakati
tunaingia madarakani hadi kufikia shilingi
bilioni 269, mwaka huu wa fedha. Hii imeongeza sana upatikanaji wa madawa
kwenye hospitali zetu, na hasa baada ya Serikali kuanza utaratibu wa kununua dawa
moja kwa moja kutoka kwenye viwanda zinakozalishwa. Aidha, Serikali imegawa katika kila halmashauri vifaa tiba, ikiwemo
vitanda ya kawaida, vitanda vya kujifungulia, magodoro na mashuka, ambavyo thamani
yake kwa ujumla ni shilingi bilioni 3.58.
Halikadhalika, katika kuboresha Huduma za Afya ya Mama na Mtoto, Serikali
ilipata fedha jumla ya shilinigi bilioni 161.9 kutoka Benki ya Dunia pamoja
na wadau wengine wanaosaidia sekta ya afya kwenye Mfuko wa Pamoja (Busket Fund).
Fedha hizo zimepangwa kutumika kuboresha vituo vya afya 170 ili kuviwezesha kutoa huduma za uzazi za dharura kwa lengo la
kuokoa maisha ya mama na mtoto; na zinatumwa moja kwa moja katika vituo vya
afya husika katika mwaka huu wa fedha.
Kuhusu
sekta ya maji, miradi mingi ya maji hivi sasa inatekelezwa sehemu mbalimbali
nchini. Karibu kwenye mikoa yote kuna miradi mikubwa ya maji inatekelezwa. Mathalan,
mwezi Machi 2017, nilikuwa Mkoa wa Lindi ambapo nilitoa maelekezo ya kukamilishwa
kwa haraka mradi wa maji wa Ng’apa wenye thamani ya shilingi bilioni 32, ambao
nimeambiwa unaendelea kukamilika. Mwezi Juni mwaka huu, nilizindua Mradi wa
Maji wa Ruvu Juu pale Mlandizi kwa ajili ya kuhudumia Jiji hili la Dar es
Salaam na sehemu za Mkoa wa Pwani. Aidha, mwezi Julai, nilizindua mradi mkubwa
wa maji pale Sengerema wenye thamani ya shilingi
bilioni 22.4. Mwezi Julai pia niliweka Mawe ya Msingi kwenye mradi wa maji
wa Kigoma wenye thamani ya shilingi
bilioni 42 na Mradi Mkubwa wa Maji kutoka Ziwa Victoria kwenda miji ya
Nzega, Tabora na Igunga wenye thamani ya shilingi ya shilingi
bilioni 550. Juzi
mmeshuhudia Mheshimiwa Waziri Mkuu akizindua mradi wa maji kule Longido wenye
thamani ya shilingi bilioni 16;
lakini nafahamu pia mradi wa maji wa Musoma umekamilika na unasubiri
kuzinduliwa. Halikadhalika, nafahamu kuwa kuna mradi mkubwa wa maji
unatekelezwa katika jiji la Arusha wenye thamani ya shilingi bilioni 476, na wakati wowote tutaanza utekelezaji wa
mradi mwingine mkubwa wenye thamani ya shilingi bilioni 250 kwa ajili ya miji ya Bariadi, Legangabilili, Maswa, Meatu na Busega. Kama hiyo
haitoshi, mwezi Julai mwaka huu, Serikali ya India ilitupatia mkopo wa masharti
nafuu wenye thamani ya Dola za Marekani
milioni 500, sawa na takriban shilingi
trilioni 1.2, kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji kwenye miji 17, ikiwemo Zanzibar. Kwa ujumla, miradi
mingi inatekelezwa sehemu mbalimbali nchini. Hivyo basi, nina imani kuwa baada
ya muda mfupi, tutakuwa tumepunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la maji nchini.
Nitoe wito kwenu viongozi wa Serikali za Mitaa kuendelea kuwahamasisha wananchi
kutunza mazingira pamoja na vyanzo vya maji. Bila kufanya hivyo, itafika wakati
tutakuwa na miundombinu mizuri isiyotoa maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti
na Ndugu Wajumbe;
Mbali na kuboresha huduma za jamii,
tumeweza kuimarisha miundombinu ya kiuchumi, hususan usafiri na nishati. Tumeanza
ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa kutoka Dar es Salaam hadi
Mwanza na Kigoma na kisha nchi za Burundi na Rwanda, kwa fedha zetu wenyewe.
Ujenzi wa kipande cha kilometa 300 kutoka
Dar es Salaam hadi Morogoro tayari umeanza, ambapo kiasi cha shilingi trilioni 2.74 kitatumika. Na hivi majuzi (ijumaa), tumesaini mkataba wa
kuanza ujenzi wa kipande cha kilometa 412
kutoka Morogoro hadi Dodoma (Makutopora) kwa thamani ya shilingi trilioni 4.328; na hivyo gharama za ujenzi kutoka Dar es
Salaam hadi Dodoma kufikia shilingi
trilioni 7.062.
Tunafanya upanuzi wa Bandari zetu za
Mtwara na Dar es Salaam. Mwezi Machi mwaka huu, niliweka Jiwe la Msingi la Upanuzi
wa Bandari ya Mtwara kwa thamani ya shilingi
bilioni 130. Aidha, mwezi Julai mwaka huu, niliweka Jiwe la Msingi la Upanuzi
wa Bandari ya Dar es Salaam, ambao thamani yake ni shilingi bilioni 926.2. Kama
hiyo haitoshi, wakati nikiwa Tanga katika sherehe za kuweka Jiwe la Msingi la
Mradi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga,
nilimwagiza Waziri wa Ujenzi kuanza taratibu za kutafuta mkandarasi wa kupanua
Bandari ya Tanga kwa thamani ya shilingi bilioni 16. Vilevile,
tumetengeneza meli mbili za Mv. Iringa na Mv. Ruvuma, ambazo zinatoa huduma
katika Ziwa Nyasa. Aidha, tupo katika hatua za mwisho za kupata wakandarasi kwa
ajili ya ukarabati wa meli mbili za Mv. Victoria na Butiama pamoja na ununuzi
wa meli mpya kwa ajili ya Ziwa Victoria.
Sambamba na hayo, tunakamilisha
upanuzi wa Viwanja Vikubwa vya Ndege vya Mwalimu Julius Nyerere kwa gharama ya shilingi bilioni 560 na Kilimajaro kwa
thamani ya shilingi bilioni 91.
Aidha, tunaendelea na ukarabati wa viwanja takriban 11 vya ndege sehemu mbalimbali nchini, ikiwemo Mwanza (shilingi bilioni 90); Mtwara (shilingi bilioni 46); Shinyanga (shilingi bilioni 49.2); Sumbawanga (shilingi bilioni 55.9); Musoma (shilingi bilioni 21), Songea (shilingi bilioni 21) na Iringa (shilingi bilioni 39). Tumenunua ndege
mpya sita, mbili tayari zimewasili na kuanza kazi, kwa ajili ya kutoa huduma ya
usafiri na kukuza sekta ya utalii. Kama mnavyofahamu, ukuaji na ustawi wa sekta
ya utalii kwa kiasi kikubwa unategemea uwepo na ubora wa usafiri wa anga katika
nchi. Vilevile, ujenzi wa barabara unaendelea vizuri. Tangu tumeingia
madarakani tumeshajenga takriban kilometa
1,500 za lami kwa thamani ya shilingi
trilioni 1.8. Na nyingi bado tunaendelea kuzijenga. Nikianza kuzitaja
tunaweza kumaliza kesho. Lakini kwa kuwa leo tupo hapa Dar es Salaam, niseme tu
kuwa, moja ya barabara tunayotarajia kuanza kujenga hivi karibuni ni barabara
ya njia sita kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze. Aidha, tunaendelea na ujenzi
wa barabara za juu pale TAZARA (shilingi
bilioni 94.031) na Ubungo (shilingi
bilioni 177.424); na muda si mrefu tutaanza ujenzi wa Awamu ya II, III na
III za miundombinu ya magari ya mwendokasi kwa thamani ya shilingi bilioni 891.
Tunajenga miundombinu hii ili kupunguza tatizo la msongamano wa magari katika
Jiji hili.
Kuhusu umeme, nako tunaendelea vizuri.
Lakini tunafahamu kuwa mahitaji ya umeme nchini bado ni makubwa. Hivyo, tunaendelea
na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kuzalisha umeme, ikiwemo Kinyerezi I na II,
ambayo kwa pamoja inatarajiwa kuzalisha Megawati
565, kwa kutumia gesi yetu asilia. Miradi hii kwa ujumla ina thamani ya shilingi trilioni 1.2. Aidha, maandalizi
kwa ajili ya miradi ya Kinyerezi III na IV, ambayo itazalisha takriban Megawati 600, inaendelea vizuri. Tumeanza
pia maandalizi ya ujenzi wa mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa maji pale Stiglier’s Gorge, ambao utazalisha Megawati 2,100. Tunataka, hadi kufikia
mwaka 2020, nchi yetu iwe na angalau Megawati
5,000 kutoka Megawati 1,460 za
sasa. Sambamba na hilo, tunaendelea na jitihada za kupeleleka umeme vijijini.
Mpaka sasa, tumeshapeleka umeme kwenye vijiji zaidi ya 4,000. Aidha, mwaka huu tumeanza Awamu ya Tatu ya Mpango wa Umeme
vijijini. Lengo letu ni kufikisha miundombinu ya umeme kwenye vijiji vipatavyo 7,873 ifikapo mwaka 2020/21. Katika bajeti ya mwaka huu, tumetenga shilingi bilioni 469.09 kuanza
kutekeleza mradi huo. Tunataka dhana ya viwanda inasambae hadi vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti
na Ndugu Wajumbe;
Mbali na kuongeza ukusanyaji mapato na
kudhibiti matumizi, tumeimarisha nidhamu na kurejesha heshima kwenye utumishi
wa umma. Tumewachukulia hatua za kinidhamu baadhi ya watumishi wazembe na wala
rushwa. Zaidi ya hapo, tumewaondoa takriban watumishi hewa wapatao 20,000, ambao walikuwa wakiigharimu
Serikali takriban shilingi bilioni
19.848 kwa mwezi; na kwa mwaka shilingi
bilioni 238.176. Vilevile, tumewaondoa watumishi wenye vyeti feki wapatao 12,000,
ambao kwa mwaka waligharimu Serikali shilingi bilioni 142.9. Tumefanya hivyo
ili kurudisha nidhamu na kuenzi elimu na ueledi katika utumishi wa umma.
Mtakubaliana nami kuwa, uwepo wa watumishi hewa na wenye vyeti feki ulikuwa
ukizorotesha na kupunguza ufanisi katika utoaji huduma kwenye taasisi za umma.
Aidha, uwepo wa watumishi wenye vyeti feki ulikuwa unapunguza heshima na hadhi ya
elimu na ujuzi, na hivyo, kushusha ari na morali miongoni mwa watumishi wenye
sifa.
Sambamba na hilo, tumejitahidi kuondoa
kero mbalimbali, ambazo zilikuwa zikiwasumbua wananachi. Mathalan, tumeondoa
kero za utitiri wa kodi kwa wakulima, wafugaji na wavuvi. Tumefuta tozo 80
kwa wakulima, tozo 7 kwa
wafugaji na tozo 5 kwa wavuvi.
Tumepiga marufuku kutoza kodi mazao yanayosafirishwa kutoka Halmashauri moja
kwenda nyingine, ambayo uzito wake hauzidi tani
moja. Na kwa kuwa tozo hizi nyingi tulizozifuta zilikuwa zikisimamiwa na
ninyi watu wa Serikali za Mitaa, niwaombe kupitia vikao vyenu, mkafanye
taratibu za kuzifuta kama bado hamfanya hivyo. Lakini, kama
hiyo haitoshi, kwa wakulima pia, kufuatia uamuzi wa Serikali wa kuanzisha
utaratibu wa kununua mbolea kwa pamoja (Bulk Procurement System – BPS),
tumeweza kupunguza bei ya mbolea ya kupandia na kukuzia kuanzia mwezi uliopita
(Septemba). Mathalan, Mkoani Lindi, bei ya mfuko mmoja wa mbolea ya kupandia imeshuka
kutoka shilingi 100,000 hadi kufikia
shilingi 51,000. Mikoa mingine bei
zimepungua kutegemeana na gharama za usafirishaji. Na huu ni mwanzo tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti
na Ndugu Wajumbe;
Baada ya
kuchukua hatua za kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kudhibiti matumizi;
kuboresha huduma za jamii; kuimarisha miundombinu ya uchumi; kurejesha heshima
ya utumishi wa umma na kushughulikia baadhi ya kero zinazowakabili wananchi
wetu; ambazo kimsingi, bado tunaendelea nazo, sasa tumeanzisha vita ya uchumi. Kama
mnavyofahamu, nchi yetu ni tajiri. Tuna rasilimali za kila aina. Tunayo madini
misitu, rasilimali za misitu na majini, n.k. Aidha, nchi yetu inashika nafasi
ya pili kwa vivutio vya utalii duniani baada ya Brazil. Lakini pamoja na kuwa
na rasilimali nyingi kiasi hicho, bado hazijatunufaisha. Wanaonufaika ni watu
wengine.
Kutokana
na hali hiyo, tumeamua kuchukua hatua za makusudi kulinda rasimali zetu. Mlisikia
kuwa tuliunda Tume za kuchunguza biashara ya madini na vito vya thamani.
Matokea yake, kila mmoja wetu hapa amesikia.
Lakini kwa kifupi, tulikuwa tunaibiwa sana. Kwa sababu hiyo, mwezi Julai
2017 tulipitisha Sheria za kulinda rasilimali zetu, hususan madini. Aidha, kwa
lengo hilo hilo la kulinda rasilimali zetu, hivi majuzi nikiwa Mererani
niliagiza kuanza mara moja kwa ujenzi wa uzio kuzunguka eneo lenye rasilimali
nyingi ya madini ya Tanzanite, ili
kudhibiti vitendo vya wizi. Nafurahi ujenzi huo tayari umeanza. Lakini niseme tu
kuwa huu ni mwanzo tu. Hatutaishia kwenye madini pekee. Tutaenda pia kwenye
rasilimali zetu nyingine, ikiwemo za utalii, misitu na za majini. Tunataka
kuona, rasilimali za nchi yetu, zinatunufaisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti
na Ndugu Wajumbe;
Katika
kuchukua hatua hizi, ni dhahiri kuwa wapo watu walioathirika na kuumia. Na
natambua kuwa wapo watu wanalalamika. Lakini kwangu mimi, hili ni jambo la
kawaida, kama kweli tunahitaji maendeleo. Maendeleo hayaji kirahisi. Maendeleo sio
lelemama. Maendeleo ni mapambano. Hivyo basi, niwaombe Watanzania wenzangu
tujidhatiti katika harakati za kuleta maendeleo kwa nchi yetu. Waingereza wana usemi
wao usemao “No Pain, No Gain” au “No sweet without sweat”. Lakini ningependa kusema tu kuwa watu wengi
wanaolalamika hivi sasa ni wale waliokuwa wakinufaika na mfumo ulikuwepo zamani. Huwezi kutegemea mmiliki wa benki iliyokuwa
ikinufaika kwa kufanya biashara na Serikali afurahie hatua tunazozichukua; Haiwezekani
mtu aliyekuwa akilipwa mishahara na posho za watumishi hewa afurahie hatua
tunazochukua; Huwezi kutegemea mtu aliyekuwa akikwepa kodi afurahie hatua
tunazozichukua; Huwezi kutegemea mtu aliyezoea kusafiri nje kila wiki afurahie
hatua tunazozichukua; huwezi kutegemea mtu aliyepata ajira kwa kutumia cheti
feki alichokinunua Kariakoo afurahie hatua tunazozichukua. Lakini pia huwezi
kutegemea mtu aliyekuwa akinufaika na fedha za pembejeo hewa (ambapo katika Halmashauri 140 zilizofanyiwa
uchunguzi, imebainika kuwa zilitolewa pembejeo hewa zenye thamani ya shilingi
bilioni 57.963) na kaya masikini hewa (56,000) kupitia TASAF, afurahie
hatua tunazozichukua. Ni dhahiri kuwa
watu waliokuwa wakinufaika, watalalamika.
Hivyo
basi, binafsi sishitushwi sana na malalamiko yanayotolewa na baadhi ya watu. Natambua,
ukitumbua mtu jipu ni lazima atalalamika. Sana sana tu, kelele zinazopigwa hivi
sasa zinatuongezea nguvu zaidi ya kuendelea na jitihada tulizozianza, ambazo
kwa hakika kabisa, naweza kusema sio tu zinaungwa mkono na wananchi walio wengi
bali pia zimeanza kuleta matokeo chanya ya kiuchumi kwa nchi yetu. Kama
mnavyofahamu, nchi yetu ni miongoni mwa nchi zinaongoza kwa ukuaji uchumi
Barani Afrika hivi sasa, ambapo mwaka huu uchumi wetu unatarajiwa kukua kwa asilimia
7.1. Hii inafanya nchi yetu kushika nafasi ya tatu. Sambamba na hilo, tumeweza
kudhibiti mfumko wa bei. Mathalan, mwezi
Julai, mfumko wa bei ulikuwa asilimia
5.2, lakini mwezi Agosti ulishuka hadi kufikia asilimia 5.0. Hii ni dalili njema. Lakini zaidi ya hapo, kinyume na
baadhi ya watu wanavyosema, nchi yetu imeendelea kung’ara katika kuwavutia
wawekezaji wengi. Hivi majuzi mmemsikia Mkurugenzi Mkuu wa Kituo Cha Uwekezaji
(Tanzania Investment Centre – TIC) akieleza kuwa mwaka uliopita nchi yetu iliongoza
kwa kuvutia wawekezaji wengi kwenye Ukanda wetu wa Afrika Mashariki. Tathmini
hii inaenda sambamba na Ripoti ya African
Economic Outlook Toleo la 16 iliyotolewa kwa pamoja na Benki ya Maendeleo
ya Afrika (AfDB) na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), ambayo inataja
nchi yetu kuwa miongoni mwa nchi kumi bora Barani Afrika kwa kuvutia wawekezaji
mwaka 2016. Na hiki ni kielezo kuwa hatua tunazochukua ni nzuri na mwelekeo
wetu ni mzuri. Na huenda hii ndio sababu viongozi wengi wa nje wanatembelea
nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ndugu Wajumbe, Mabibi
na Mabwana;
Niliona
nianze na hayo ili kuwapa taswira halisi ya hali ilivyo hapa nchini. Na kwa
kuwa ninyi mko karibu zaidi na wananchi na mnashirikiana nao kwenye mambo mengi,
nina uhakika kuwa mtaenda kuwafafanuliwa kuhusu hatua hizi tunazozichukua. Baada
ya kusema hayo, sasa naomba nizungumzie masuala yanayohusu Mkutano huu wa leo.
Kwanza
kabisa, napenda kuipongeza ALAT pamoja na mamlaka za Serikali za Mitaa kote
nchini kwa kazi kubwa mnazofanya katika kuleta maendeleo kwa nchi yetu.
Mafanikio mengi ya Serikali niliyoyataja hapo awali, yamepatikana kutokana na
jitihada mnazozifanya ninyi lakini pia ushirikiano mnaotupa sisi wa Serikali
Kuu. Kwa kutumia vyanzo vyenu vya mapato, mmeweza kutekeleza miradi mingi ya
maendeleo, ikiwemo ujenzi wa shule, hospitali, vituo vya afya, zahanati, miradi
ya maji pamoja na barabara. Aidha, mara nyingi, ninyi ndio mmekuwa wasimamizi
wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali Kuu kwenye maeneo yenu. Kwa sababu hiyo, sina budi, kuwapongeza.
Lakini
pamoja na pongezi hizo, hampaswi kuridhika na mafanikio yaliyopatikana. Kama
mnavyofahamu, nchi yetu bado ina safari ndefu ya kufikia kule tunakotamani.
Mathalan, nimeeleza hapo awali kuwa Serikali hivi sasa inatekeleza elimu bila
malipo, lakini ukiachilia mbali tatizo la uhaba wa madawati ambalo
tumelipunguza kwa kiwango kikubwa, bado tuna upungufu wa madarasa, maabara,
vyoo, nyumba za walimu, n.k. Hivyo basi,
Mamlaka za Serikali za Mitaa, hazina budi, kubuni mikakati ya kushughulikia
matatizo hayo. Aidha, kwa kuwa mko karibu na wananchi, mnao wajibu wa kuwahimiza
wananchi kupeleke watoto wao mashuleni ili wanufaike na fursa iliyotolewa na
Serikali ya kutoa elimu bila malipo.
Kwenye
afya pia, bado kuna upungufu mkubwa ya miundombinu, ikiwemo hospitali, vituo
vya afya, zahanati, nyumba za watumishi, n.k. Huko nako hamna budi kubuni
mikakati ya kushughulikia matatizo hayo. Aidha, kwa kuwa hivi sasa Serikali
imeongeza upatikanaji wa madawa kwenye hospitali zetu, niwaombe waheshimiwa
Madiwani na Wakurugenzi mwendelee kuhamasisha wananchi kujiunga na mifuko ya
bima za afya ili kupata matibabu bila vikwazo. Vilevile, hakikisheni mnasimamia
vyema fedha na matumizi ya dawa, ikiwemo kuanzisha mifuko ya dawa (Drug Revolving
Fund) kwa kila Halmashari, ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa fedha za
dawa.
Sambamba
na hayo, ili kuhakikisha mnakuwa na uwezo wa kutosha wa kuboresha huduma za
jamii nilizozitaja na kutekeleza miradi ya maendeleo, hamna budi kuimarisha
ukusanyaji wa mapato. Nafahamu hii ni changamoto kubwa inayozikabili mamlaka za
Serikali za Mitaa. Na kimsingi, nionavyo mimi, tatizo sio kwamba hakuna vyanzo
vya mapato. Hapana. Hali hii inatokana na sababu kubwa mbili. Kwanza, fedha
nyingi zinazokusanywa hupotelea kwenye mifuko ya “wajanja” wachache. Pili,
watendaji wengi wanakosa ubunifu katika kubuni vyanzo endelevu vya mapato. Ndio
maana kila siku utaona wanaongeza tozo kwenye mazao ya wakulima, wavuvi au
wafugaji. Hivyo basi, nitoe wito kwenu kuhakikisha mnatengeneza mifumo
madhubuti ya ukusanyaji mapato, hususan ukusanyaji mapato kwa njia ya
kielektroniki. Na katika hili,
ningependa kuwasisitiza kutumia Wakala wa Serikali Mtandao katika
kutengeneza mifumo yenu ya ukusanyaji kodi. Aidha, nawahimizeni kubuni vyanzo
endelevu vya mapato.
Halikadhalika, kuhakikisheni mnasimamia vizuri fedha mnazokusanya na
zile zinazotolewa na Serikali Kuu kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Natambua hivi sasa suala la hati chafu limepungua kwenye halmashauri nyingi. Lakini
hii haimanishi kuwa ubadhirifu na wizi umekwisha kwenye Halmashauri zetu. Ubadhirifu
bado upo. Imethibitika kuwa mara nyingi taarifa za vitabuni hazifanani na hali
halisi ya utekelezaji wa miradi na kazi (value for money). Kwa maneno mengine,
kazi inayofanyika hailingani na thamani halisi ya fedha inayotumika. Hivyo
basi, nawaomba ndugu wajumbe mlipe suala hili la usimamizi wa fedha za Serikali
kipaumbele kinachostahili. Miradi inayotekelezwa ni lazima iendane na thamani
ya fedha zinazotolewa. Na katika hili, msisite kuwachukuliwa hatua za kinidhamu
au kuwatumbua wale wote wakatakaojihusisha na ubadhirifu wa fedha zinazotolewa
kwa ajili ya maendeleo ya wananchi. Lakini niwaombe na ninyi kuacha mtindo wa
kutoa zabuni kwenye makampuni yenu au ya washirika wenu, ambayo hayana uwezo wa
kutekeleza miradi husika.
Masuala mengine
ambayo ningetamani sana kuona mnayapa kipaumbele kwenye maeneo yenu ni kudhibiti
migogoro na makundi kwenye halmashauri zetu. Haipendezi kuona, kwenye
Halmashauri, kuna kundi la Meya na Naibu Meya; ama kundi la Mwenyekiti na Mkurugenzi.
Hali hii inazorotesha utendaji na kupunguza kasi ya kuwapelekea maendeleo wananchi.
Nawasihi pia muendelee kushughulikia kero mbalimbali zinazowakabili wananchi,
hasa wananchi wa kipato cha chini, ikiwemo, kama nilivyosema awali, utitiri wa
kodi kwa wakulima, wafugaji na wavuvi; na halikadhalika ukosefu wa maeneo ya
biashara kwa wafanyabiashara wadogo. Vilevile, nawasihi muendelee kuwahimiza
wananchi kuhusu umuhimu wa kudumisha amani na umoja wetu, kulipa kodi na
kuchapa kazi kwa bidii. Nina imani, sote tukifanya haya, nchi yetu itapata
maendeleo, tena kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika risala yako
umeeleza kuhusu mipango yenu mbalimbali na kuwasilisha baadhi ya maombi. Kwa
ujumla, niseme tu kuwa nimeyapokea maombi yenu yote. Lakini nakiri kuwa
nimefarijika sana kusikia azma yenu ya kuhamishia Makao Makuu yenu kutoka hapa
Dar es Salaam kwenda Dodoma, Makao Makuu ya nchi yetu. Nawapongezi sana kwa
kuunga mkono dhamira ya Serikali ya kuhamia Dodoma. Na napenda kutumia fursa
hii kuwahakikishia kuwa, kama nilivyoahidi kwenye hotuba yangu ya kupokea
wadhifa wa kuwa Mwenyekiti wa CCM mwezi Julai mwaka jana, hadi kufikia mwaka
2020, Serikali yote itakuwa imehamia Dodoma. Kama mnavyofahamu, tayari Waziri
Mkuu, Mawaziri, Makatibu Wakuu na baadhi ya watendaji wa Wizara wameshahamia
Dodoma. Makamu wa Rais anatarajia kuhamia mwaka huu. Na mimi natarajia kuhamia
mwakani. Hivyo basi, narudia tena, kuwashukuru kwa uamuzi wenu wa busara wa
kuhamia Dodoma. Na kuhusu jengo mnalotaka kujenga Dodoma kwa ajili ya ofisi na
kitega uchumi, wakati ukifika, Serikali kulingana na uwezo wake wa kifedha,
itaangalia uwezekano wa kuwaunga mkono.
Kwenye Risala yako
pia umeeleza suala la ucheleweshaji wa fedha za maendeleo kutoka Serikali Kuu,
suala la uhaba wa watumishi wa Serikali za Mitaa na pia posho za Waheshimiwa
Madiwani. Serikali inatambua masuala hayo yote. Tutaendelea kuhimiza HAZINA
kutoa fedha za maendeleo kwa haraka. Kama mnavyofahamu, tangu tumeingia
madarakani, tumejitahidi sana kuhakikisha fedha zinatolewa kwa wakati.
Mathalan, katika Bajeti ya mwaka 2014/2015 fedha za maendeleo zilizotengwa
kwenda kwenye halmashauri (Serikali za Mitaa) ni shilingi bilioni 339.8 lakini zilizotoka zilikuwa shilingi bilioni 250.2 sawa na asilimia 62; mwaka 2015/16 zilitengwa shilingi bilioni 296.3, zikatolewa shilingi bilioni 168.8 sawa na asilimia 57; mwaka 2016/17 zilitengwa shilingi bilioni 256.7, zilizotolewa ni
shilingi 251.5 sawa na asilimia 98. Na katika mwaka huu wa fedha, tumetenga shilingi bilioni 308.6, na napenda
niwahakikishie fedha zote zitatolewa. Sambamba na hilo, mwaka huu, tumeanzisha
Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), ambayo imetengewa shilingi bilioni 246, ukiachilia mbali
fedha zilizoahidiwa na wafadhili mbalimbali, ikiwemo Benki ya Dunia. Hivyo
basi, sina shaka, tatizo la fedha za maendeleo litazidi kupungua.
Kuhusu tatizo la
uhaba wa watumishi baada ya kuwaondoa watumishi wenye vyeti feki, Serikali
mwaka huu imepanga kuajiri watumishi wapya wapatao 52,000, wakiwemo watumishi wa afya, walimu na watumishi wa kada
nyingine. Hivyo basi, nina imani kuwa hii itapunguza uhaba wa watumishi kwenye
Serikali za Mitaa. Ombi langu tu msiajiri watumishi wasio na sifa. Lakini niwe
mkweli ombi lenu la kuongeza posho kwa madiwani, kidogo litaiwia Serikali vigumu
kulitekeleza kwa wakati huu. Kama nilivyosema hapo awali, kwa sasa, Serikali
imeelekeza nguvu zake katika kuboresha huduma za jamii na kujenga miundombinu
ya kiuchumi. Hivyo basi, niwaombe Waheshimiwa Madiwani mtuelewe katika hili.
Aidha, nawaombeni mzidi kuwahamisha Watanzania kuchapa kazi kwa bidii na kulipa
kodi ili kuongeza uwezo wetu wa kifedha. Uwezo wetu ukiimarika, Serikali kamwe
haitasita kuboresha maslahi sio tu yenu ninyi Waheshimiwa Madiwani bali pia
watumishi wote wa umma.
Umeeleza pia kuhusu ombi
la kutaka kuridhiwa kwa Mkataba wa Umoja wa Afrika kuhusu Ugatuaji Madaraka (The African Union Charter on Principles and
Values on Decentralization, Local Governance and Local Development) pamoja
na ombi la kutaka nchi yetu kuwa Makao Makuu ya Jumuiya ya Tawala za Serikali
ya Mitaa kwa Kanda ya Afrika. Maombi haya nayo tumeyapokea. Nitaziagiza taasisi
husika kupitia Mkataba huo na endapo haukinzani na Katiba na Sheria zetu, uweze
kuridhiwa na Bunge letu. Na kuhusu ombi la nchi yetu kuwa Makao Makuu, natambua
faida za kuwa mwenyeji wa Taasisi hiyo. Hata hivyo, kabla ya kukubali kuipokea
taasisi hiyo, ni vyema tathmini ikafanyika kuhusu mahitaji ya fedha yanayotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Siwezi kuhitimisha
hotuba yangu bila kugusia kaulimbiu ya Mkutano huu, ambayo inasema “Ardhi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa
ni chachu ya Maendeleo, Halmashauri zitenge ardhi kwa ajili ya Uwekezaji wa
Viwanda Vidogo na Vikubwa”. Kama mnavyofahamu, kipaumbele kikubwa cha
Serikali ya Awamu ya Tano ni ujenzi wa Viwanda. Na ili kujenga viwanda,
unahitaji ardhi. Hivyo, kaulimbiu hii ni nzuri na imekuja kwa wakati muafaka. Kwenye
ziara zangu maeneo mengi nchini, nimekuwa nikihimiza wakurugenzi, Wakuu wa
Wilaya na Mikoa kutenga maeneo na kuweka miundombinu rafiki ili kuwavutia
wawekezaji kujenga viwanda. Hivyo basi, kwa mara nyingine napenda kurudia tena
wito huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Mheshimiwa Naibu
Waziri wa TAMISEMI;
Ndugu Wajumbe, Mabibi
na Mabwana;
Nimezungumza mengi. Napenda kuhitimisha hotuba
yangu kwa kukushukuru tena Mwenyekiti wa ALAT kwa kunialika kufungua Mkutano
huu. Napenda kuwahakikishia tena kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ipo pamoja
nanyi. Nitafuatilia Mkutano huu, na yote mtakayokubaliana, nawaahidi kuwa
Serikali itayazingatia na kuyatekeleza. Wito wangu kwenu, mjadiliane kwa amani
na uwazi.
Baada ya kusema hayo,
sasa natamka kuwa Mkutano wa 33 wa Jumuiya ya Tawala za Serikali za Mitaa
(ALAT) umefunguliwa rasmi.
Mungu Ibariki ALAT!
Mungu Zibariki Mamlaka zote za Serikali za Mitaa
Nchini!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269