Mbezi Beach A, Dar es Salaam
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Saad Mtambule, amewapa shime Viongozi na Wananchi wa Mtaa wa Mbezi Beach 'A', Kawe Jijini Dar es Salaam, kuendelea 'kukomaa' katika juhudi zao za kuhakikisha Ufukwe wa Mbezi Beach A (Rainbow), unakuwa nadhifu, huku akiahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha kutimiza azma hiyo.
DC Mtambule alisema na kutoa ahadi hiyo wakati akizungumza na viongozi na Wananchi wa mtaa huo, walioshiriki kufanya usafi kwenye ufukwe wa Bahari, eneo la Rainbow, Mtaa wa Mbezi Beach A, jana asubuhi, ambapo mapema kabla ya kuzungumza alikagua maeneo mbalimbali ya ufukwe huo.
Alisema, baada ya kukagua ameona madhara yanayosababisha ufukwe huo kuwa mchafu na kukosa mvuto, ikiwemo taka zinazoletwa na mito inayoungana kutoka maeneo mbalimbali ya nje, hivyo akaahidi kushirikiana na viongozi wa mtaa huo, kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti uchafuzi huo na kuweka vema maeneo yaliyoadhirika.
"Kinachonivutia ni kwamba tofauti na maeneo mengine katika wilaya hii ya Kinondoni, ni kwamba dhamira ya kufanya usafi kwenye fukwe, limedhamiriwa na Wananchi wenyewe, kwa hiyo kinachotakiwa ni kuungwa mkono juhudi zenu. kwa kweli ninyi mmekuwa mfano wa kuigwa na maeneo mengine", alisema DC Mtambule.
Akisoma risala, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Mbezi Beach ‘A’ (JMMBA) alisema, tangu Februari 7, 2026 Wananchi na viongozi wa Mbezi Beach A, wamekuwa wakifanya usafi wa ufukwe huo kila Jumamosi mfululizo bila kukosa na kwamba kwa wiki nne wamekusanya mifuko 217, 304, 291 na 88, jumla mifuko 900, ndani ya takribani mita 200 walizoweza kuzifanyia usafi kwenye awamu hii ya kwanza kati ya takriban mita mia tisa (900) za ufukwe huo wa Mbezi Beach A.
"Hatua muhimu tuliyoanza tangu Februari 28 ni kuhamia kwenye usafi unaoendeshwa kwa takwimu, si hisia pekee. Ndiyo maana, kwa msaada wa wataalam wa washirika wetu wa usafi wa fukwe, tumeanza kutumia WABA Methodology (Waste Assessment and Brand Audit). Huu ni mfumo wa kitaalamu unaotusaidia kuhesabu taka tunazokusanya, kupima uzito, na kurekodi taarifa kwa muundo unaoweza
kulinganishwa zoezi hadi zoezi.
Faida yake ni kwamba tunapata takwimu zinazotuwezesha kupanga vizuri mahitaji ya vifaa na nguvu kazi, na pia kutoa ushahidi unaoaminika kwa wadau wa kitaifa. Katika zoezi la tarehe 28 Februari 2026, tulipima kwa utaratibu na kupata wastani wa uzito wa kilo 11.61 kwa mfuko, tuseme kilo 12. Kwa kipimo hicho, mifuko 900 tuliyokusanya ndani ya wiki nne inawakilisha takribani tani 10 hadi
11 za taka ngumu tulizoondoa kwenye ufukwe ndani ya takribani mita 200 tulizoweza kuzifanyia usafi kwenye awamu hii ya kwanza kati ya mia tisa za ufukwe wetu huu wa Mbezi Beach A (Rainbow). Takwimu hizi zinakusudiwa pia kuingizwa kwenye mifumo ya kitaifa kama National Plastic Action Partnership (NPAP) ili kazi ya wananchi iwe na ushahidi wa kitaalamu na kusaidia upangaji wa hatua dhidi ya uchafu wa plastiki", alisea Mwenyekiti huyo.
Alisema changamoto yao kubwa ni uondoaji taka baada ya kukusanya na kwamba kwa maelezo waliyopata, mkandarasi wa taka za majumbani anafanya kazi chini ya utaratibu unaolipiwa kupitia makusanyo ya kaya, hivyo taka za ufukwe haziingii moja kwa moja kwenye huduma hiyo bila mwongozo maalum wa Manispaa.
"Tumeelezwa pia kuwa huduma kama hii inapohitajika hutazamwa kama safari maalum yenye gharama ya ziada, Kwa mantiki hiyo, tunaomba Manispaa iweke utaratibu rasmi, ikiwemo afisa anayehusika moja kwa moja na jambo hili, ili jamii inapokuwa na mazoezi ya usafi wa kijamii kama hili pawepo njia ya haraka, ya wazi na ya moja kwa moja ya kuratibu uondoaji wa taka zilizokusanywa", alisema Mwenyekiti huyo.
Baadhi ya viongozi waliosimamia zoezi la kufanya usafi huo, jana, walikuwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mbezi Beach A, Mtendaji Kata ya Kawe na Diwani wa kata hiyo.
Chini ni Matukio mbalimbali wakati Wananchi wa Mbezi Beach A, Kawe Dar es Salaam, wakifanya usafi kwenye Ufukwe wa Mbezi Beach A (Rainbow), jana.👇
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269