.

KADA WA CCM AMVAA ZITTO KABWE KIGOMA KASKAZINI

Apr 2, 2010

OMARI  NKWARULO
MBUNGE wa Jimbo la Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe, amedaiwa kuwatelekeza wapigakura wake kwa kutotembelea maeneo kadhaa yenye kero, kiasi cha wengi wa wapigakura hao kutomfahamu kwa dhahiri zaidi ya kumuona kupitia televisheni.
    Pia amedaiwa kuwadharau kwa kuamua kutangaza hivi karubuni kwamba anafanya uchunguzi kuona ni jimbo gani analokubalika zaidi kugombea badala ya jimbo lake la sasa.
  Madai hayo yalitolewa jana mjini Dar es Salaam, na mkazi wa kijiji cha Mkigo, kigoma Vijijini, Omari Nkwarulo wakati akitangaza kuwania kumvaa Zitto, kwa kugombea ubunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya CCM.
   Nkwarulo aliyetangaza nia hiyo mbele ya waandishi wa habari katika hoteli ya Travetine, Magomeni, alisema, zitto hakupaswa kutangaza kutafuta jimbo lingine wakati bado ni mbunge halali wa Kigoma Kaskazini na kwamba kufanya hivyo amewaona wapigakura wa jimbo hilo kuwa hawana manufaa kwake.
 " hatua ile ya kutangaza kuwa anawatuma wataalamu kufanya utafiti jimbo gani analokubalika zaidi ni ili agombee ni usaliti kwa sisi wananchi wa jimbo lile la Kigoma Kaskazini kama vile mchezaji wa Yanga kutangaza kutangaza waziwazi kuwa atahamia timu ya Simba kabla ya msimu wa ligi kuisha", alisema Nkwarulo.
   Nkwarulo alidai hatua ya Ziotto kutafuta maoni ya wapi anakubalika ili agombee ni 'janja' ya kutafuta moja ya majimbo yenye machimbo ya madini. Alidai, tangu Zitto apate jimbo la Kigoma Kaskazini amekuwa akijishughulisha zaidi na hoja za kitaifa na hivyo kuwa kama mbunge wa kuteuliwa huku akiacha jimboni kukiwa na kero mbalimbali zinazowakabili wapigakura.
   Nkwarulo alisema kutokana na hali hiyo ndiyo sababu ameamua kutangaza nia yake ya kutaka kuwania ubunge wa jimbo hilo la Kigoma Kaskazini ili kuwezesha kuwepo mipango madhubuti katika kusimamia mipango ya utatuzi wa kero ambazo zimedumu kwa muda mrefu sasa.
  Alisema, pia nia yake ni kutaka jimbo hilo lirejee mikoni kwa CCM kwa kuwa kuwa chini ya upinzani kunasababisha kudhoofisha maendeleo kwa jumla kutokana na kutokuwa viongozi kutokuwa na malengo ya pamoja katika kutekeleza ilan ya uchaguzi.
   Nkwarulo ni msomi ambaye amehitimu ya Chuo Kukuu katika masuala ya Biashara na ni Mkurugenzi wa shule ya sekondari ya Lake Tanganyika iuliyopo Kigoma.
   Kwa mujibu wa maelezo yake, ni mwanachama wa TANU tangu mwaka 1971 na baadaye CCM ambapo alipata kadi mpya ya uanachama mwaka 1991.
    Kwarulo amekuwa mwananchi wa kwanza kutoka Kigoma Vijijini kutangaza kuwania Ubunge Kigoma Kaskazini, jimbo ambalo kwa sasa linashikiliwa na Zitto.
MKAZI wa Kigoma Vijijini, Omari Nkwarulo akitangaza nia yake ya kugombea ubunge jimbo la Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya CCM, jana kwenye hoteli ya Travetine, Dar es Salaam. Mbunge wa jimbo hilo kwa sasa ni Zitto Kabwe (Chadema). Kushoto ni Charles Sabini ambaye ni Makamu Mkuu wa shule ya Sekondari ya Lake Tangyika.
  

2 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ª