.

U20 ZA TANZANIA NA MALAWI KUUMANA LEO DAR

Apr 30, 2010

TIMU ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes inashuka dimbani leo kuivaa timu ya umri kama huo ya Malawi.
   Mechi hiyo ya marudiano ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Afrika kwa vijana wa umri huo, imepangwa kufanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
   Kwa ujumla mechi hiyo inatarajiwa kuwa ngumu kutokana na ukweli kwamba, katika mechi ya kwanza ya kinyanga'anyiro hicho iliyochezwa Malawi takriban wiki mbili zilizopita, Ngorongoro walilazimisha sare ya mabao 2 - 2.
  Hivyo ni wazi kuwa vijana wa Malawi nao watashuka uwanjani, lakini kikubwa kwenye pambano hilo watakuwa wamekuja kusaka ushindi ili waweze kusonga mbele na mzunguko wa pili wa michuano hiyo.
  Wakati Wamalawi hao wakidhani hivyo, naye Kocha Mkuu wa Ngorongoro, ambaye ni raia wa Brazil, Rodrigo Stockler atakuwa na jukumu linalofanana na lile la wapinzani.
  Jukumu hilo ni kucheza kwa kujituma, nidhamu na kwa ustadi mkubwa ili kuweza kuibuka na ushindi wa aina yoyote ile ili kusonga mbele.
   Bila shaka, Ngorongoro kama iliweza kutoka sare ugenini, na sasa inacheza kwenye dimba la nyumbani ina kila sababu ya kuibuka na ushindi kwenye mechi hiyo ambayo inatarajiwa kushuhudiwa na idadi kubwa ya mashabiki wa soka.
  Ili kuhakikisha kuwa Ngorongoro wanasonga mbele kwenye michuano hiyo, tayari Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) limeondoa viingilio kwa upande wa mzunguko wa uwanja wa Uhuru ili kutoa fursa kwa mashabiki wengi kujitokeza na kuishangilia timu hiyo.
  Akizungumzia maandalizi ya pambano hilo, Ofisa Habari wa TFF, Florian Kaijage alisema maandalizi yote yamekamilika ikiwemo kuwasili kwa Wamalawi na waamuzi wa mechi hiyo.
  "Uamuzi wa TFF kutoa ofa kwa mashabiki wa soka wa upande wote wa mzunguko kuingia bure, ili kutoa fursa kwa idadi kubwa ya mashabiki kujitokeza uwanjani na kuishangilia timu hiyo," alisema.
  Mechi hiyo ambayo itaamua timu itakayosonga mbele, itachezeshwa na mwamuzi na wasaidizi wake kutoka Elitrea. Aliwataja waamuzi hao ni Gebremichael Luelseged ambaye atasaidiana na Mohamed Berhane na Tesfagiorghis O'Michael, wakati mwamuzi wa akiba ni Ibada Ramadhan(Tanzania).
   Mshindi katika mechi hiyo anatarajiwa kuvaana na timu ngumu ya vijana ya Ivorycoast, ambapo kulingana na ratiba mechi hiyo itachezwa Juni, mwaka huu wakati fainali za michuano hiyo itachezwa Libya, mwakani.
  Viingililo vingine vvya mechi hiyo ni sh.10,000 kwa viti vya VIP, sh.5,000 kwa viti vya jukwa kuu, wakati sh.3,000 kwa viti vya jukwa la kijani.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ª