HOTUBA KAMILI YA MHE. JAKAYA KIKWETE, MWENYEKITI WA CHAMA CHA MPAINDUZI NA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWA WANACHAMA WAPENZI NA WAKEREKETWA WA CCM KWENYE UZINDUZI WA MPANGO WA UCHANGIAJI WA FEDHA ZA KAMPENI KWA KUTUMIA SIMU ZA MKONONI
Ndugu Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Bara;
Ndugu katibu Mkuu;
Ndugu Wajumbe wa Kamati Kuu na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa;
Ndugu Wenyeviti wa CCM na Makatibu wa CCM wa Wilaya ;
Ndugu Viongozi wengine wa CCM ;
Ndugu wageni waalikwa, mabibi na mabwana.
Nakushukuru sana Ndugu Amos Makalla, Katibu wa Fedha na Uchumi wa Chama chetu, kwa maelezo mazuri ya utangulizi. Tumekusanyika jioni hii kuzindua shughuli za uchangiaji wa Mfuko wa CCM wa Kugharamia Kampeni ya CCM kwa Uchaguzi Mkuu wa 2010.
Ndugu Viongozi na Ndugu WanaCCM;
Huu ni mwaka wa uchaguzi, na uchaguzi una gharama zake. Na, kwa Chama kikubwa kama chetu, gharama ni kubwa. Ndugu Makala amefafanua kwa kina mahitaji ya zana na hivyo pesa zinazohitajika kugharamia uchaguzi. Kimsingi hili ni jukumu la wanachama pamoja na wapenzi wa CCM. Lakini pia ni jukumu la la mwananchi yoyote mwenye mapenzi na CCM au anayeona au kuamini kuwa Tanzania inafaa kuendelea kuongozwa na Chama cha Mapinduzi.
Chama chetu kimetafakari na kubuni njia mbalimbali za kupatia fedha. Katika kufanya hivyo, tumezingatia matakwa ya Sheria mpya ya Gharama za Uchaguzi inayotaka tutumie njia zilizo halali na utaratibu ulio wazi. Mweka Hazina wa Chama chetu, kama tulivyozoea kumuiita, ameeleza uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa katika kikao chake cha tarehe ........hadi.......2010 kuwa tutafute fedha kwa njia kuu tatu, yaani:
(a) Michango ya hiari ya wanachama: kwamba zaidi ya kulipa ada, wanachama watoe michango ya hiari kuwezesha kupata ushindi. Kiasi cha kutoa ni hiari ya mwanachama lakini tungependa kila mwanachama achangie sio chini ya shilingi 1,000 kwa mwezi kuanzia sasa mpaka uchaguzi. CCM itakuwa imepata shilingi bilioni 20.
(b) Njia ya pili ni harambee ambapo tutawaomba wanachama na wapenzi wa CCM wanaopenda na wanaoweza kuchangia wachangie. Tumekusudia kufanya Harambee tatu kati ya sasa na mwezi Julai. Tumefungua akaunti maalum kwa ajili hiyo ambayo mwanachama na mtu yoyote anayetaka kuchangia anaweza kutuma fedha. Hivyo si lazima mtu ashiriki kwenye hafla ya harambee yenyewe lakini anaweza kutuma moja kwa moja. Aidha, anaweza kufika Ofisi Ndogo Lumumba au Afisi Kuu Zanzibar na kuwasilisha mchango wake.
Ndugu Washiriki,
Aina nyingine ya uchangiaji ni mpya kabisa ya kutumia simu za mikononi. Hii ni njia ya kisasa ambayo maelezo yake yataelezwa na wahusika. Kwa kutumia njia hii, wachangiaji watatakiwa kuchanga kwa viwango vya shilingi 300, shilingi 500 na shilingi 1,000, kwa uamuzi wake mtu.
Ndugu Viongozi na Ndugu WanaCCM;
Mpango tunaouzindua jioni hii, unawawezesha wale walio na simu za mkononi kutumia njia hii kuchangia shughuli za kampeni za Chama chetu. Aidha, kwa wale ambao hawana simu za mkononi wanaweza pia kutumia njia hii kuchangia mfuko wetu wa kampeni kwa kununua vocha na kumwomba mwanachama mwenye simu amtumie. Mpango huu utarahisisha sana uchangiaji na utapunguza usumbufu uliotokana na utaratibu wa zamani wa mtu kusafiri kwenda kwenye ofisi za CCM kutoa mchango wake ambako wakati mwingine mchangiaji alikuwa anaweza kufika ofisini asiwakute watu kwa sababu kadhaa. Kwa utaratibu huu mpya, mtu anaweza kuchangia toka mahali popote alipo bora tu awe na simu.
Pamoja na kukichangia Chama chetu kupitia simu za mikononi, ni makusudio yetu kuutumia mfumo huu wa kisasa kwa mawasiliano kati ya Chama chetu na wanachama wake. Aidha, itakapofika wakati wa uchaguzi, tutautumia kuwasiliana na wapiga kura kwa ujumla. Kuanzia sasa, katika kampeni hii, tumeweka mfumo wa kisasa wa mawasiliano, ambapo Makao Makuu ya CCM, Makao Makuu ya Kampeni yetu Kitaifa, wataweza kuwasiliana kwa urahisi zaidi na Ofisi za CCM za Mikoa, Wilaya na Kata. Namba za simu za viongozi wa Chama katika ngazi hizo zinaendelea kuingizwa kwenye mfumo wa mawasiliano ambapo viongozi hao wataweza kuwasiliana na Makao Makuu, au baina yao, katika kutoa na kupata taarifa mbalimbali bila gharama yoyote kwao na watajibiwa kwa haraka zaidi.
Baada ya uzinduzi huu, kuanzia sasa, tutawaomba Watanzania wengi kadri iwezekanavyo kujiunga na mtandao wa CCM bila gharama yoyote ili wawe wanapata taarifa mbalimbali za CCM katika maeneo yao husika. Kama nilivyokwidokeza, wakati wa kampeni, tutatumia njia ya simu za mikononi kuwasiliana na wapiga kura na kuwapa taarifa kuhusu Chama chetu, sera zetu na mipango yetu. Pia tutautumia kujibu hoja na propaganda za wapinzani.
Vilevile, tunaendelea na kazi ya kukusanya namba za simu za wanachama wetu wote wa CCM, kwa wale ambao wana simu, ili tuwe na uwezo wa kuwasiliana nao siku za usoni pale itakapohitajika. Katika mchakato utakaoanza mwezi Julai wa kuhakiki regista ya wanachama wa CCM kwenye matawi kwa ajili ya kura za maoni, tunayo nia ya kutengeneza daftari kuu la wanachama wa CCM kwa nchi nzima na kuliweka kwenye mfumo wa kompyuta. Daftari hili litakuwa linaboreshwa kila mwaka na kutupa idadi halisi ya wanachama wa CCM na kiwango cha ulipaji ada. Juu ya hili, wanachama wa CCM sasa wataweza kulipa ada zao kwa kutumia simu zao za mkononi, ambapo watatumiwa namba za risiti kutoka kwenye electronic receipt book.
Ndugu zangu,
Mpango wa uchangiaji kupitia njia hii ya wazi ya simu za mikononi sio tu unatokana na msukumo wa zama na mazingira, bali pia ni hatua muhimu ya utekelezaji wa dhamira yangu niliyoieleza katika hotuba yangu ya kuzindua Bunge tarehe 30 Desemba, 2005, ya kuwa na “utaratibu halali, ulio wazi, wa chama au mgombea kutafuta fedha za uchaguzi; na utaratibu halali ulio wazi, wa chama au mgombea kutumia fedha hizo.” Dhamira hii ilidhihirika kisheria kwa Bunge letu kutunga sheria ya Gharama za Uchaguzi hivi karibuni. Leo tunaidhihirisha dhamira hiyo kwa matendo. Matumizi ya simu za mkononi katika kuchangia kampeni za uchaguzi za Chama Chetu ni moja ya utaratibu halali, ulio wazi, wa chama chetu kutafuta fedha za uchaguzi. Tuliahidi tumetimiza tena kwa vitendo.
Ndugu Viongozi na Ndugu WanaCCM;
Natoa wito kwa viongozi, wanachama, wapenzi na wakereketwa wa CCM kukichangia Chama chetu ili kukipa uwezo wa kushiriki kwa ukamilifu katika uchaguzi wa mwaka huu na kupata ushindi wa kishindo. Changieni na wahamasisheni ndugu, jamaa na marafiki nao wachangie. Sio lazima kuchangia kiasi kikubwa kwa mara moja. Unaweza kuchangia kidogo kidogo kwa kadri unavyoweza. Ningependa kila mmoja wetu ajiwekee lengo la kuchangia walau shilingi 1,000 kuanzia sasa hadi wakati wa kampeni, lakini wenye uwezo watoe zaidi. Unaweza kutoa zote 1,000 kwa mara moja au ukatoa kidogo kidogo.
Ndugu zangu viongozi wa Wilaya na Mikoa,
Pamoja na kuanza kwa mpango huu wa kuchangia kwa kutumia njia ya simu za mikononi, bado njia zetu za zamani za kuchangia zipo pale pale. Vilevile, haina maana kwamba ukishachangia kwa SMS basi usichangie kwa njia nyingine. La hasha! Wenye uwezo wa kutoa vifaa na michango ya aina nyingine wanaruhusiwa kufanya hivyo. Hii ni njia mojawapo tu ya kuchangia kwa urahisi.
Nawasihi kwamba, tukitoka hapa na kurudi majumbani mwetu, tuhakikishe kwamba tunahimiza wananchi kuchangia Chama chetu ili kiweze kumudu gharama za uchaguzi na kupata ushindi mnono. Tutaendelea kutoa elimu na maelekezo kwa umma kuhusu namna ya kuchangia. Tukifanya hivyo, naamini tutafikia lengo la kukusanya fedha zitakazokidhi bajeti yetu ya kampeni.
Chama cha Mapinduzi kimeifanyia mema mengi nchi yetu. Nchi yetu na watu wake ni wamoja na nchi yetu ni tulivu.
Tuchangie CCM, Pamoja Tutashinda!
Kidumu Chama cha Mapinduzi.
HABARI KATIKA PICHA
MWENYEKITI wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akitoa hotuba ya uzinduzi wa mtandao huo, jana jioni katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaa. Kulia ni Katibu wa NEC-CCM, Uchumi na Fedha, Amos Makalla.KATIBU Mkuu wa CCM Yussuf Makamba akimpogheza Kikwete kwa hotuba nzuri ya ufunguzi huo. Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Pius Msekwa.Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete akizindua rasmi mtandao huo.JK akishangilia baada ya kuzinduaJK na Makamba wakitazama katika simu zao mtandao huo unavyofanya kazi muda mfupi baada ya kuzinduliwa.Waalikwa wakishangulia baada ya kuona mtandao huo unafanyakazi katika simu zao walipojaribu kuchangia baada ya kuzinduliwa.Abdulrahman Kinana akibofya simu yake kuona mtandao unavyofanya kazi.
Waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa na Katibu Mkuu wa UVCCM nao wakijaribu mtandao. Waziri Mkuu mstaafu Dk Salim Ahmed Salim, Waziri Kiongozi, Dk Mohamed Ghalib Bilal na waziri Mkuu Mstaafu Cleopa Msuya waakijaribu simu kuona mtandao huo. Mwenyekiti mstaafu wa CCM (Bara) John Malecela na mkewe Anne Kilango Malecela wakijaribu pia mtandao huo katika simu. Kushoto ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na watoto, Magareth SittaWaziri Mkuu MizengoPinda na Waziri kiongozi Shamsi Vuai Nahodha na Mama Salma Kikwete pia hawakauwa nyuma kujaribu simuWaalikwa akifuatilia hafla nzima ilivyokuwa ikiendaVicko Kamata na mwenzake nao wakijaribu kuchangia kwa njia ya simu baada ya mtandao kuzinduliwa na JKWANAMUZIKI wa bendi ya Vijana Jazz wakitumbuiza katika hafla hiyo. Kina mama wakijimwayamwaya ukumbini kwa furaha ya kuzinduliwa mtandao huo.Vicl kamata akitumbuiza wakati wa uzindiuzi wa mtandao huoMwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete akiangana na Mzee Malecela na Dk. Salim mwishono mwa hafla.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269