Breaking News

Your Ad Spot

May 9, 2010

KINONDONI NA IRINGA ZATOANA JASHO BAO 1-1




TIMU za Kinondoni Kombaini na Ruaha Boyz ya Iringa, jana zilishindwa kutambiana baada ya kulazimishana sare ya bao 1-1 katika mechi ya makundi ya Kili Taifa Cup,  waliyocheza katika uwanja wa Samora mjini Iringa.

Katika mechi hiyo ambayo timu ya Iringa chini ya Kocha wake Freddy Felix Minziro ilionekana kupania kuibuka na ushindi, zilimalizika dakika 45 za kipindi cha kwanza  bila timu hizo kufungana.

Ni katika kipindi cha pili ndiyo timu zilionekana kuchachamaa kwa nia ya kupata bao, na hatimaye  katika dakika ya 62 ya kipindi hicho, Kinondoni walipata bao safi kupitia kwa mshambuliaji wake Sunday Frank.

Kupatikana kwa bao hilo, kuliwafanya Iringa kucheza mchezo wa kufa na kupona ambao ulizua rafu za hapa na pale, lakini wakapata bao  la kusawazisha katika dakika ya 65 na kuwafanya angalau kupata ahueni.

Mpambano uliendelea kuwa mkali huku kukwatuana kukiendelea kushamiri miongoni mwa wachezaji wa pande zote,  hatimaye mchezaji Frank kupewa kadi nyekundu na mwamuzi wa mechi hiyo kwa kudaiwa kumchezea vibaya mchezaji wa Iringa.

Kadi hiyo ilizua kizazaa na kusababisha rabsha kwa muda, mbele ya mkuu wa mkoa wa Iringa, Mohammed Abdulaziz  ambaye alifika kushuhudia kipute hicho, ambapo alilazimika kuingia kati kutuliza rabsha hizo.

Mapema kabla ya mechi hiyo, saa 8 mchana zilishuka dimbani timu za  Pinda Boyz ya Rukwa na Mbeya ambapo Mbeya ilitoka kidedea baada ya kuifunga Rukwa bao 1-0.


No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages