Breaking News

Your Ad Spot

Oct 8, 2010

TUTASHIRIKIANA NA JIRANI ZETU KUUKABILI UGAIDI –TANZANIA

Wakili Mkuu wa serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Donald Chidowu (katikati), akifuatilia mjadala kuhusu mkakati wa Jumuia ya Kimataifa  wa kukabiliana na ugaidi. Mkutano huo ambao ameandaliwa na Kamati ya sita inayohusika na sheria za Kimataifa katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN), umeakutanisha wataalamu wa masuala ya sheria kutoka mataifa wanachama wa umoja huo na unafanyika makao makuu ya UN mjini New York, Marekani. (Picha kwa Hisani ya  UN).
================================================
HABARI KAMILI
NA MWANDISHI MAALUM

NEW YORK-Tanzania imesisitiza kwamba inayo nia na dhamira ya dhati ya kushirikiana na jirani zake na jumuia ya kimataifa, katika kupambana na vitendo vya ugaidi ikiwa ni pamoja na kuwakamata watuhumiwa wanajiohusisha vitendo hivyo.

Msisitizo huo umetolewa na Wakili Mkuu wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Bw. Donald Chidowu, wakati wataalam wa sheria wa Kamati ya Sita ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, walipokuwa wakijadili juhudi na mikakati ya Jumuia ya Kimataifa na kitaifa katika kukabiliana na kupambana na ugaidi.

“Kama nchi ambayo imeoja ukatili wa matukio ya kigaidi, dhamira na nia yetu iko wazi kabisa nayo ni kushirikiana na jumuia ya kimataifa na majirani zetu dhidi ya ugaidi”.

Bw. Chodowu anayeongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo, akasema Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine inalaani kwa nguvu zote tukio la kigaidi lililotokea jijini kampala, Uganda mwezi julai. na kwamba inaugana na serikali ya Uganda katika kuwatafuta na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria yeyote atakayepatikana kuhusika na tukio hilo.

Akasema ugaidi hauna rangi, dini, haujali mipaka na wala hauchagui nchi. Na akaongeza.” Kila mtu ni mhanga wa ugaidi, hakuna mwenyewe uhakika wa kutoguswa na matukio au tukio la kigaidi. Na kwa sababu ya unyeti wa matukio yenyewe, ni ukweli usiopingika kwamba tunahitajika kama jumuia ya kimataifa, kuunganisha nguvu zetu na mikakati ya pamoja kuukabili ”.

Akabainisha kuwa wakati jumuia ya kimataifa ikiendelea kuvutana na kubishana juu ya tafsiri ya ugaidi, ucheleweshaji wa ukamilishwaji wa rasmu kuhusu mkataba wa ugaidi, ndivyo ugaidi unavyojikita na kuibuka na mbinu na mikakati ya hali ya juu.

Akatoa wito wa jumuia ya kimataifa kumaliza tofauti zao, kuonyesha utashi wa kisiasa na ushirikiano ili rasmu hiyo iweze kukamilika.

Kuhusu juhudi zinazofanywa na serikali ya Tanzania katika kukabiliana na kudhibiti ugaidi, pamoja na mambo mengine, Wakili Mkuu wa serikali ameuleza mkutano huo kwamba, Tanzania kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za kimataifa imekuwa ikiandaa mafuzo kwa maafisa wa ngazi za juu kutoka mamlaka za utekelezaji wa sheria.

Akasema mafunzo wanayopewa yanahusu namna ya kuukabili ugaidi na uhalifu wa kimataifa .

Aidha akasema Tanzania katika kuunga mkono mkakati wa kimataifa wa kupambana na ugaidi, inaandaa mkakati wa kitaifa na akatumia nafasi hiyo kuziomba jumuia ya kimataifa kuipatia Tanzania msaada wa kiufundi ili kusaidia mpango wa utekelezaji.

Karibu kila mjumbe aliyezungumza katika mkutano huo, alitoa wito wa kutaka kumalizwa kwa mkanganyiko kuhusu tafsiri sahihi ya ugaidi na kusisitiza kwamba rasmi inayoandaliwa lazima ije na tafsiri itakayokubalika.

Aidha licha ya kila mjumbe kueleza nchi yake inafanya nini katika kukabiliana na ugaidi, baadhi ya wajumbe wamesisitiza kwamba juhudi za kukabiliana na ugaidi lazima ziheshimu haki za binadamu na mipaka ya nchi nyingine na kwamba kinyume na hayo, juhudi hizo zitakuwa kazi bure.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages