Mkurugenzi wa Oparesheni wa Jeshi la Polisi, Kamishna Paul Chagonja (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na maofisa watatu wa Jeshi la Polisi waliokabidhiwa tiketi na fedha za kujikimu ili kuweza kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa wa Maofisa wa Polisi utakao fanyika Oktoba 22-28 mwaka huu katika mji wa Oralndo , Florida nchini Marekani.Wengine kutoka kushoto ni SACP.Jamal Rwambow, ACP, Renatus Mbushi,ASP.Emmanuel Mkilia na Mkurugenzi wa Mahusiano wa Kampuni ya Sigara Tanzania, Paul Makanza aliyekabidhi udhamini huo. TCC imekuwa ikiwadhamini maafisa mbalimbali wa Jeshi la Polisi kuhudhuria mkutano huu tangu mwaka 2001.( Picha na Executive Solutions.)
===============================
Na Mwandishi Spesho
Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) imefadhili maofisa watatu waandamizi wa polisi kuhudhuria Mkutano wa Taasisi ya Kimataifa ya Wakuu wa Polisi (IACP) unaofanyika mwezi huu nchini Marekani. Akizungumza jana, wakati wa kukabidhi udhamini huo kwa washiriki, Mkurugenzi wa Mahusiano TCC, Paul Makanza, alisema walianza kuisaidia Polisi tangu 2001, kampuni yake ilipodhamini jeshi hilo kuhudhuria Mkutano wa IACP nchini Marekani.
“Kila mwaka tumekuwa tukilisaidia Jeshi la Polisi kuhudhuria mikutano hii muhimu. Tangu 2001 hadi leo wajumbe 40 kutoka Jeshi la Polisi wamehudhuria mikutano hii chini ya udhamini wa TCC, na mwaka huu tutadhamini wajumbe wengine watatu,” alisema Makanza.
Wajumbe watakaohudhuria mkutano uliopangwa kufanyika Orlando, Florida kuanzia Oktoba 23 hadi 27 ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Jamal Rwambo ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Maabara ya Uchunguzi ya Jeshi la Polisi Makao Makuu ya Jeshi; Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Renatus Mbushi ambaye ni Kamanda wa Chuo cha Polisi Moshi na Kamishna Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Emmanuel ambaye ni Meneja wa Teknolojia ya Mawasiliano.
Mkurugenzi Makanza alisema kwamba mikutano ya aina hiyo hufumbua macho kwa wasimamizi wa sheria, kwani hutoa fursa kwa wanaohudhuria kujiongezea weledi katika utawala, teknolojia na operesheni kwa kuchota yaliyo mazuri zaidi kutoka kwa wenzao.
“Tukiwa wafadhili wakuu kwa wajumbe wa Tanzania, tunafurahia kuona kwamba elimu waliyopata wajumbe wa Tanzania kwa kweli inawekwa katika vitendo hapa nyumbani,” akaongeza.
Makanza alimwambia Mkuu wa Mafunzo na Operesheni wa Jeshi la Polisi, Kamishna Paul Chagonja: “Usalama wa umma ni muhimu kwa biashara kustawi, likiwa ni shirika linalowajibika, TCC inapenda kulisaidia Jeshi la Polisi kutekeleza kazi zake.”
Wakati huo huo, Makanza alikabidhi kompyuta zenye thamani ya Sh milioni 10 kwa Kamishna Chagonja, aliyezipokea kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC)wa Dodoma, Zelothe Stephen, baada ya RPC huyo kuomba msaada huo siku zilizopita.
Kwa upande wake, Chagonja aliishukuru TCC kwa kulisaidia Jeshi la Polisi katika programu yake ya kwenda na wakati. Alisema Jeshi la Polisi linatambua mchango mkubwa wa TCC, mashirika mengine kama hayo na jamii kwa ujumla.
“TCC inatambua changamoto nyingi zinazolikabili Jeshi la Polisi katika kulinda amani na usalama na linashukuru kwa huduma zinazotolewa na Jeshi la Polisi kuhakikisha usalama wa bidhaa, mali na watu,” akasema kamishna huyo.
Aliishukuru kampuni hiyo kwa kuwadhamini wajumbe wa Jeshi kwenda IACP mwaka huu na kuwapa changamoto wanaokwenda kuhakikisha wanarejea na kitu kipya na wanakuwa na uwezo wa kukitekeleza.
Kamishna Chagonja pia alishukuru TCC kwa mchango wake katika kazi zake za kuchunguza na kuainisha mikakati ya kihalifu kuhusu bidhaa bandia kwenye biashara na uchumi wa nchi.
“Kwa niaba ya Inspekta Jenerali wa Polisi, napenda kusema kwamba Jeshi la Polisi Tanzania litaendelea kuwa mstari wa mbele kutekeleza hatua mbalimbali katika kukabiliana na uhalifu na masuala yanayohusiana nayo, kuhakikisha kwamba mazingira ya biashara yanakuwa mazuri,” akasema Chagonja.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269