Breaking News

Your Ad Spot

Jan 16, 2011

BAN KI MOON ATAJA VIPAUMBELE VYA 2011

• AFRIKA KUPEWA UMUHIMU
• ATAHADHARISHA KUWA MWAKA MGUMU

Na Mwandishi Maalum
New York-Kutokana na changamoto mbalimbali zinazoendelea kulikabili Bara la Afrika, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, anasema bara hilo litaendelea kuwa moja ya kipaumbele chake katika mwaka huu wa 2011.

Ban Ki Moon ameyasema hayo wakati alipokuwa akivitaja vipaumbele vyake vya mwaka huu wa 2011 huku akitahadharisha kwamba kama ilivyokuwa katika mwaka uliopita mwaka huu pia utakuwa na changamoto zake.

“ Afrika bado itaendelea kuwa sehemu muhimu katika vipaumbele vyangu na vipaumbele vya Umoja wa Mataifa kwa mwaka huu, hasa kutokana na changamoto mbalimbali zinazolikabili bara hili” akasema Katibu Mkuu.

Akivitaja vipaumbele hivyo mbele ya Mabalozi 192 wanaoziwakilisha nchi zao katika Umoja huo, Ban Ki Moon akiwa na Naibu wake Dkt. Asha-Rose Migiro anasema. “ Kama mwaka 2010 ulikuwa ni mwaka uliokuwa na changamoto nyingi kwa Umoja wa Mataifa, basi mwaka 2011 utakuwa zaidi”

Akaeleza kuwa kazi ya kukabiliana na changamoto hizo si ya mtu mmoja mmoja bali ni kazi inayowakabili watu wote katika ujumla wao

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, anakitaja kipaumbele cha kwanza kuwa ni juhudi mjumuisho za kukabiliana na suala zima la maendeleo endelevu katika dunia yenye kukabiliwa na mkwamo wa uchumi

Anasema kutokana na mkwamo wa uchumi bado watu wanahofu kubwa kuhusu ajira zao, kuhusu usalama wao na kuhusu maisha ya baadaye ya watoto wao. akaunganisha kipaumbele hicho na mkutano wa nchi maskini kuliko zote duniani utakaofanyika mwezi mei huko Uturuki.

Anasema mkutano huo pamoja na mambo mengine utalenga katika kutangaza mpango wa utekelezaji wa miaka kumi utakaoboresha hali ya usalama wa chakula, ajira, kupunguza matukio hatarishi, kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na matumizi ya nishati mbadala na salama kwaajili ya nchi zinazoendelea.

Aidha suala zima la mabadiliko ya tabia nchi, ni kipaumbele cha pili kwa Katibu Mkuu huyo. Akisisitiza kwamba pamoja na mafanikio yaliyopatika katika mkutano uliofanyika Cancun, Mexico, bado kuna kazi kubwa mbele.

Uwezeshaji wa wanawake ni kipaumbele cha tatu, katika kipaumbele hicho, Ban Ki Moon anaahidi ushiriki na fursa sawa za kijinsia, kupinga vitendo vya kikatili dhidi ya wanawake na kuongeza idadi ya wanawake katika nafasi za juu za uongonzi ndani ya Umoja wa mataifa.

Akisisitiza kuhusu nafasi ya wanawake, Ban Ki Moona anabainisha kwa kusema. “ Chukua jambo lolote lile, kuanzia mabadiliko ya tabia nchi, maendeleo, amani na usalama. Pale ambapo wanawake wanakuwa ni sehemu ya utekelezaji wa masuala hayo, basi dunia hushuhudia matokeo yanayoridhisha”.

Kuifanya dunia kuwa mahali salama ni kipaumbele cha nne, anakifafanua kipaumbele hicho kwa kuelezea pamoja na mambo mengine,juhudi za UN katika kuhakikisha demokrasia inachukua mkondo wake huko Ivory Cost, juhudi za kuleta amani ya kudumu katika Sudan pamoja na kura ya maoni ya Sudani ya Kusini.

Kwa upande wa kipaumbele cha Tano na cha Sita, Ban Ki Moon anavitaja kuwa ni kuboresha haki za binadamu pamoja na uharaka wa kushughulikia misaada ya kibinadamu kwa kujifunza kwa majanga yaliyotokea Haiti na Pakistani mwaka uliopita.

Akasema kuwa Umoja wa mataifa unaendelea na mikakati ya kujipanga vizuri katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na kuunganisha nguvu , uratibu na matumizi ya raslimali zilizopo ili Umoja wa Mataifa uweze kushughulikia kwa haraka na kwa ufanisi mara tu pale majanga yanapotokea.

Kuhusu upunguzaji wa silaha zikiwamo silaha kali na za maangamizi, ambacho ni kipaumbele cha saba, Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa, anasema kuwa jitihada zitaendelea za kukabiliana na changamoto hizo, huku akielezea kuridhishwa kwake na hatua ya hivi karibuni ambapo Marekani na Urusi zilifikia maridhiano ya kupunguza malimbikizo ya silaha za nyukilia.

“Umoja wa Mataifa utahakikisha kwamba unaendelea na kazi kubwa ya kuhakikisha mkataba wa kupiga marukufu kabisa majaribio ya silaha za kinyukila unafanyika, na tutaongeza jitihada za kukabliana na tishio la usalama wa nyukilia na ugaidi wa kinyukilia.

Akitaja kipaumbele cha nane, Katibu Mkuu anakieleza kuwa ni mwendelezo wa mchakato wa kujisafisha, kujipanga na kuboresha mfumo wa kiutendaji, utoaji wa maamumi, uwazi, uwajibikaji zaidi ndani ya sekretarieti ya chombo hicho cha kimataifa.

Anasema kutokana na dunia kukabiliwa na changamoto nyingi na ngumu, mafanikio hayaji mara moja, lakini jambo la msingi ni kuendelea mbele kwa kujituma na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.

Akazitaka nchi hizo 192 kuwa na imani naye na kwamba hapana shaka dunia inauhitaji Umoja wa Mataifa wenye nvugu na kuwajibika zaidi.

KATIBU  MKUU WA UMOJA WA MATAIFA, BAN KI MOON AKIVITAJA VIPAUMBELE VYAKE NANE  VYA MWAKA 2011 MBELE YA MABALOZI 192 WANAOZIWAKILISHA NCHI ZAO KATIKA UMOJA WA MATAIFA. KUSHOTO KWAKE NI NAIBU KATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA DKT. ASHA-ROSE  MIGIRO NA KULIA NA RAIS WA BARAZA KUU LA  65 LA UMOJA WA MATAIFA, BW. JOSEPH DEISS

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages