Breaking News

Your Ad Spot

Feb 25, 2011

KUTOKA MAREKANI

UNACHANGAMOTO KUBWA YA KUTAFSIRI KWA VITENDO SERA NA MIPANGO INAYOHUSU JINSIA- NAIBU WAZIRI
NA MWANDISHI MAALUM, NEW YORK
Pamoja na ukweli kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuingiza masuala ya jinsi katika sera, mikakati na mipango yake, bado inakabiliwa na changamoto za kuzitafrisiri kwa vitendo, sera, mipango na mikakati hiyo.  Hayo yameelezwa Naibu Waziri, Wizara ya Maendeleo ya Jamii , jinsia na Watoto, Mhe. Ummi Alli Mwalimu (pichani), wakati alipokuwa akichangia majadiliano kuhusu fursa na ushiriki wa wanawake na watoto wa kike katika elimu, mafunzo, sayansi na teknolojia pamoja na fursa sawa katika ajira.
       Naibu Waziri Ummi Mwalimu , anaongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika Mkutano wa 55 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake unaoendelea hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa. Ujumbe huo pia unajumuisha washiriki kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
        Anazitaja changamoto hizo kuwa ni katika kufanya uchambuzi wa masuala ya jinsia na ufinyu wa takwimu za jinsia ambazo zingeweza kutoa ushawishi katika maandalizi na utekelezaji wa sera na mipango.
        Naibu Waziri Ummi Mwalimu amewaeleza washiriki wa mkutano huo, kwamba changamoto nyingine ni katika kubadilisha mawazo na mitizamo ya jamii kuhusu suala zima la maendeleo na ushiriki wa wanawake.
       Hata hivyo anasema pamoja na changamoto hizo, serikali inaendelea na kazi ya kuzikabili na kuzifanyia kazi kwa kuwa imejiweka misingi madhabuti. Na kubwa zaidi ni utashi mkubwa wa kisiasa ulioonyeshwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete na serikali zima katika kuwapatia fursa sawa wanawake katika ngazi za maamuzi.
       Akizungumzia kuhusu ushiriki wa wasichana katika masomo ya Sayansi, Naibu Waziri anasema idadi ya wasichana wanaojiunga na Masomo ya Sayansi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam imeongezeka maradufu.
        Anasema mafanikio hayo yametokana na uamuzi wa Serikali wa kuweka mpango mahsusi wa kuwasaidia wasichana kwa kuwapatia mafunzo ya awali yanayowaweza kujiandaa na kufanya vizuri katika mitihani ya usaili kabla ya kujiunga na masomo ya sayansi.
       Akaeleza kuwa kupitia utaratibu huo idadi ya wanafunzi wasichana wanaochukua masomo ya Sayani imepanda kutoka asilimia 7 mwaka 2003-2004 hadi kufikia asilimia 27 mwaka 2007-2008. Aidha idadi ya wasichana wanaojiunga na elimu ya juu imeongezeka kutoka asilimia 32.2 hadi kufikia asilimia 35.5.
      Kuhusu ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi, Mhe. Ummi Mwalimu anasema, Baada ya kutambua tatizo la ushii mdogo wa wanawake katika ngazi za maamu, iliamua kwa makusudi kupitia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kutoa mwanya wa kuongeza ushiriki wa wanawake katika Bunge na mabaraza ya Serikali za Mitaa.
        Kutokana na marekebisho hayo, idadi ya wabunge wanawake ni asilimia 35 ya viti vyote kukiwa na ongezeko la wabunge wanawake kutoka 63 mwaka 2004 hadi 125 huku nafasi ya Spika wa bunge ikishikiliwa na mwamamke. Kwa upande wa Baraza la Wawakilishi uwiano wa wanake katika baraza hilo ni asilima 30
       Kwa upande wa vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto wa kike, Naibu Waziri anasema kuwa serikali imepitisha sheria mbalimbali dhidi ya wale wanaokiuka haki za wanawake na watoto wa kike.
“tumejitahidi kutimiza wajibu wetu kwa kuendana na matakwa ya kimataifa kuhusu maendeleo, ulinzi na usawa wa wanawake. Aidha Serikali imeingia, imesaini au imeridhia mikataba ya kimataifa inayohusiana na maendeleo na ulinzi wa wanawake” anasisitiza Naibu Waziri Ummi Mwalimu.
       Ameihakikishia kamisheni hiyo ya Hali ya Wanawake kwamba Tanzania inaendelea na jukumu la kuhakikisha inaondoa mifumo yote inayomkandamiza mwanamke kwa kuzingatia malengo na maudhui ya mikataba na matamko ya kimataifa.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages