Na Mwandishi wetu ,Iringa
ASKOFU Boazi Sollo (pichani) amewataka viongozi wa dini kuendelea kuombea amani Taifa na kumwombea Rais Jakaya Kikwete aendelee kuliongoza vema Taifa badala ya kushabikia watu wanaotaka kuvuruga amani ya Tanzania
Askofu Sollo ambaye ni mkurugenzi wa kituo cha maombi cha Overcomers mkoani Iringa aliwataka viongozi wa madhehebu ya dini kuepuka kutumia nyumba za Mungu kuendesha ibada zenye kujenga chuki dhidi ya serikali ya Rais Jakaya Kikwete na badala yake kutumia nyumba za Ibada kuhubiria amani ya Taifa na kuwaombea viongozi wote.
Akihubiri katika ibada ya Pasaka kwenye ukumbi wa IDYDC leo askofu Sollo alisema kuwa watanzania wameendelea kuyumbishwa na kikombe cha babu wa Loliondo na kuziacha tiba sahihi ambazo zilikuwa zikitolewa katika Hospital na vituo vya afya na huduma za maombezi ambazo zinafanywa na watumishi wa Mungu.
Askofu Solloa alisema kuwa neno la Mungu ni zaidi ya kikombe cha babu wa Loliondo na kuwa uzima ni zaidi ya uponyaji hivyo ni vizuri watanzania kukimbilia kutafuta uzima kuliko uponyaji.
Hata hivyo alisema kuwa wapo watu ambao wamepokea neno la Mungu hajapata kuugua ugonjwa wa Maralia kwa zaidi ya miaka 15 kama yeye hivyo inadhihirisha ni kiasi gani neno la Mungu lilivyo na nguvu kuliko uponyaji .
"Watumishi wa Mungu wanatoa uzima na uponyaji bila kutumia kikombe kama anavyofanya babu wa Loliondo na kuwa kinachofanwa na babu huyo ambaye amekuwa akitibu kwa kisingizio cha kutumwa na Mungu huku anakusanya fedha za wagonjwa ni sawa na kuwadanganya wagonjwa na kutumia mwavuli wa dini kujipatia fedha...kama kweli ni huduma asinge weka kiwango cha shilingi 500 kwa wagonjwa angetibu bure ili mgonjwa mwenyewe aweze kutoa sadaka bila kupangiwa kiwango"
Alisema kuwa katika kudhihirisha kuwa neno la Mungu lina nguvu kuliko shetani hivi sasa vifo zaidi vimeendelea kuripotiwa kutoka kwa babu wa Loliondo hali ambayo serikali kama haitachukua hatua kikombe hicho kinaweza kuleta madhara zaidi kwa jamii .
Sollo alisema kuwa kwa upande wake hawashauri wagonjwa kuondoka katika tiba za Hospitali na kwenda Loliondo kutumia fedha nyingi kwa dawa isiyo na uhakika tofauti na kwenda mapema Hospitali na kutibiwa na wataalam ambao wamesomea kwa fani hiyo.
Alisema ni kumkosea Mungu kwa kumchanganya Mungu na shetani na kuwa hata Bibilia inatamka wazi kuwa ya Mungu mpe Mungu na ya Kaisali apewa kaisali hivyo kutibu kwa mitishamba na maombi ni sawa na kuchanganya mambo mawili kwa wakati mmoja.
Wakati huo huo askofu Sollo amewataka viongozi wa dini na watanzania wote kuendelea kuliombea Taifa na viongozi wake badala ya kuendelea kuwashabikia wale wote ambao wanachochea vurugu ambazo zitasababisha maafa kwa Taifa.
Alisema kuwa viongozi wa dini wanalo jukumu kubwa la kulinusuru Taifa na machafuko kwa kutotumia nyumba za ibada kuwasema vibaya viongozi wa nchi kama Rais na wengine na badala yake viongozi hao wanapaswa kutumia vizuri nyumba hizo za ibada kwa kuhamasisha amani na upendo kwa watanzania wote
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269