Na Mwandishi Maalum, New York
Majanga ya asili pamoja na mageuzi ya kisiasa yanayoendelea katika baadhi ya mataifa ni sehemu ya changamoto zinazoitaka Jumuia ya Kimataifa kuitafakari upya na katika mapana yake dhana ya Usalama wa Binadamu.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa , Asha-Rose Migiro (pichani) wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipokutana kujadili na kubadilishana mawazo kuhusu dhana ya usalama wa binadamu.
Migiro anasema majanga ya asili kama vile tsunami na tetemeko la ardhi yaliyotokea nchini Japani, au mfululizo wa machafuko ya kisiasa yanayoendelea katika Mashariki ya kati, ni kielelezo tosha kwamba Jumuia ya Kimataifa inatakiwa kujipanga upya.
“Matukio yanayoendelea hivi sasa ni kielelezo dhahiri kwamba hakuna nchi iliyo salama iwe imeendelea au inayoendelea, maskini au tajiri, wote hatuko salama. Anasisitiza Migiro
Na kuongeza. “ Na ndio sababu kwa kweli tunahitaji kupanua wigo wa dhana nzima ya usalama, wigo utakaohusisha pia mambo mengi zaidi yanayotishia usalama , maisha uhai na utu wa kila mmoja wetu” anafafanua Migiro.
Akabainisha kuwa hatari kwa usalama wa binadamu inaweza kuwa vya ghafla kama vile majanga ya aina ya tsunami, lakini pia inaweza kuwa ni ile inayotokana na mrundikano wa mambo mengi na kwa muda mrefu kama yale ya utawala wa kimabavu.
Katika majadiliano hayo ambayo watoa mada kadhaa akiwamo Rais Mstaafu wa Nigeria Olusegun Obasanjo, nchi wanachama pamoja na wanazuoni walibadilishana mawazo ya namna bora na sahihi ya kuitafsiri dhana ya usalama wa binadamu.
Dhana hiyo ya usalama wa binadamu ilipitishwa mwaka 2005na wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, na kila mwaka kwa nyakati tofauti imekuwa ikijadiliwa kwa lengo la kupata muafaka wa tafsiri sahihi ya usalama wa binadamu.
Akichangia mawazo yake kuhusu dhana hiyo, Rais mstaafu wa Nigeria Olusegun Obasanjo, yeye amesema kuwa ingawa anakubaliana na misingi ya dhana ya usalama wa binadamu ambayo ni uhuru wa mtu kuishi bila hofu, uhuru wa kutaka na uhuru wa kuishi kwa heshima. Lakini anadhani suala kubwa na la msingi wa yote hayo ni uhakika wa kuishi.
“ Uhakika wa mtu kuishi kwangu mimi la msingi zaidi na linatakiwa liwe la kwanza halafu ndiyo hayo matatu” anasema Rais huyo Mstaafu ambaye alijitambulisha kama mkulima.
Obasanjo anasema kuwa kila mtu anaowajibu wa kwanza kuhusu maisha yake, na wajibu huo unaanzia katika ngazi ya familia, jumuia anayoishi na kupanda katika ngazi ya taifa na kuishia kimataifa.
“Wajibu wa kwanza wa kuhakikisha kuwa unaishi ni wako wewe kama mtu binafsi, lakini pia unawajibika katika jumuia unayoishi, serikali au taifa linatakiwa kuhakikisha kwamba unaishi kwa kukuwekea mazingira na misingi ya wewe kuishi lakini wajibu wa kwanza ni wako kama mtu binafsi”.
Rais huyo mstaafu anasema uwajibikaji wa mtu mmoja mmoja katika familia au jumuia ni jambao ambalo halipashwi kupuuzwa au kuweka kando.
Aidha anasema kuwa kutowajibika kwa wadau mbalimbali zikiwamo serikali, katika utekelezaji wa sera mbalimbali kunaweza kuwa kichocheko au chimbuko la kutokuwapop kwa usalama wa binadamu.
Akatoa pendekezo kwamba kila nchi inatakiwa kuwa na orodha ya mambo ambayo inadhani kama hayatatekelezwa ipasavyo yanaweza kupelekea kutokuwapo kwa usalama wa binadamu.
Anasema kwa kuipitia orodha hiyo mara kwa mara basi serikali inaweza kujua wapi inafanya vizuri wapi inalegalega na hivyo kuchukua hatua za tahadhari na kusisitiza kuwa hilo linawezekana.
Awali akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu kufungua majadiliano hayo, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Bw, Joseph Diess aliwaambisha washiriki wa majadiliano hayo kwamba, tafsiri yoyote kuhusu dhana ya usalama wa binadamu lazima izingatie misingi mitatu muhimu ambayo ni usalama, maendeleo na haki za binadamu.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269