.

LEO NI KARUME DAY

Apr 7, 2011

Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, akipokea matembezi ya
kumbu kumbu ya miaka 39 ya kumuenzi muasis wa Mapinduzi ya Zanzibar,
hayati Abeid Amani Karume,katika viwanja vya CCM Afisi kuu Kisiwandui leo


Watanzania leo wanaadhimisha Siku ya Karume, kukumbuka ambayo taifa la Tanzania lilimpoteza mmoja wa waasisi wake, na muasisi wa Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964, Hayati Abeid Amani Karume, aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Rais Karume aliuawa kwa kupigwa risasi jioni ya Aprili 7, 1972, na wapinga Mapinduzi na maendeleo ya Zanzibar na Tanzania, akiwa makao makuu ya Chama cha Afro Shirazi, Kisiwandui mjini Zanzibar, pamoja na viongozi waandamizi wa Chama hicho ambacho mwaka 1977 kiliungana na Chama cha TANU na kuunda Chama Cha Mapinduzi.
Watanzania wana kila sababu ya kumkumbuka kiongozi wao huyo, ambaye ametoa mchango mkubwa katika kuasisiwa kwa Jamhuri ya Muungano, pamoja na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Hayati Rais Karume ana sababu ya kukumbukwa na kuenziwa, kwa sababu alikuwa kiongozi ambaye wakati wote aliweka maslahi ya taifa mbele, badala ya kufikiria maslahi au hatima yake binafsi. Hakuwa mbinafsi wa kufikiria katika kutenda au kuamua suala lolote la kitaifa, yeye atanufaika vipi.
Ndio sababu, Karume alijitoa kuhakikisha Wazanzibari wanaishi maisha mazuri kwa kuwawekea mazingira ya kuondokana na umasikini na unyonge, vitu ambavyo alikuwa akivieleza wazi kuwa binadamu hawezi kuwa huru na mwenye uzalendo akiwa anakabiliwa na mambo hayo mawili.
Ili kuondokana na hali hiyo, aliamua kutumia rasmlimali za nchi kuhakikisha anawajengea Wazanzibari nyumba bora na kisasa za kuishi, alitoa matibabu na elimu bila malipo kwa kila mwananchi, awe mwenye uwezo au asiye na uwezo, aliamua kutoa huduma za maji safi na salama bila wananchi wake kuilipia, ili kila mwananchi awe na hakika ya afya yake.
Kubwa zaidi, nyumba alizowajengea wananchi alizigawa bure na kuhakikisha wazee wasiojiweza na watoto yatima na waliotelekezwa na wazazi wao wanatunzwa na serikali hadi wazee watakapomaliza uhai wao, na watoto watakapofikia umri wa kujitegemea.
Tunamkumbuka Hayati Rais Karume, si kwa jina lake, bali kwa mambo aliyoyafanya kwa nchi kwa kutumia raslimali za umma kwa manufaa ya anaowaongoza.
Viongozi wa sasa wana mambo mengi ya kujifunza kutoka kwake likiwemo hilo la kuhakikisha raslimali za umma zinatumika kwa faida ya wananchi wote na siyo kufujwa na wajanja wachache waliopewa dhamana ya kuzisimamia.


Wakati tukiadhimisha miaka 39 ya kifo cha shujaa huyo wa Zanzibar na Tanzania, ni wajibu wa viongozi waliopo kujitolea zaidi kuwatumikia wananchi kwa moyo wa uzalendo, na hata watakapokuwa hawapo madarakani waweze kukumbukwa kutokana na alama watakazokuwa wameziacha kama alivyoacha Hayati Abeid Amani Karume, ambayo ndio mema aliyotenda na ambayo yanatusukuma kumuenzi.
 Haya ni Maoni yaliyochapishwa leo katika gazeti la Uhuru linalochapishwa na kampuni ya Uhuru Publications Ltd

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ª