.

MIAKA 47 YA MUUNGANO: BAN KI MOON AMTUMIA SALAMU ZA PONGEZI RAIS JAKAYA KIKWETE NA WATANZANIA

Apr 25, 2011


Rais Jakaya Kikwente na Ban Ki Moon

NA MWANDISHI MAALUM, NEW YORK
Wakati watanzania wakiadhimisha hapo kesho miaka 47 ya  Muungano.Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon amemtumia salamu  za pongezi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya  Mrisho Kikwete, Serikali na watanzania wote.
Katika salamu zake ambazo nakala yake ilitumwa katika Ubalozi wa Tanzania  Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon anasema , wakati huu kuliko ilivyokuwa wakati mwingine wowote, dunia inakabiliwa na changamoto nyingi.
Amesema  changamoto hizo ambazo zimevaa sura tofauti na uzito tofauti, zinavuka mipaka  kutoka taifa moja hadi lingine.  Na  kwamba kuzitafutia ufumbuzi kunataka utulivu, umakini, mshikamano na ushirikiano wa kimataifa  .
Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa, amemwelezea Rais Jakaya Kikwete kwamba, yeye binafsi amedhamiria katika kuhakikisha  kuwa  Umoja wa Mataifa, unakwenda sambamba na kasi ya mabadiliko yanayotokea hivi sasa duniani. Na kuhakikisha kwamba Umoja wa Mataifa unasimamia na kutoa matarajio yenye kuridhisha  na halisi katika kazi zake tatu kuu  za msingi ambazo ni maendeleo, amani na usalama  na haki za binadamu.
Ameeleza kuwa  anafarijika na kutiwa moyo sana na uongozi unaojituma wa   Jamhuri ya Muungano wa Tanzania . Na kwamba anaihesabu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama mshirika  mkubwa katika  kuifanya dunia kuwa endelevu na  salama kwa watu wote.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ª