.

RAIA WA KENYA WAFUNGUA KESI YA MADAI DHIDI YA SERIKALI YA UINGEREZA KWA KUNYANYASWA WAKATI WA VITA YA MAU MAU

Apr 12, 2011

RAIA wanne wa Kenya wanaodai kuwa walinyanyaswa wakati kundi la Mau Mau lilipokuwa likikandamizwa na utawala wa ukoloni, wamefungua kesi dhidi ya serikali ya Uingereza.
Kundi hilo linalodai fidia kupitia Mahakama kuu, linasema kuwa walishambuliwa kati ya mwaka 952 na 1961 na maofisa wa utawala wa ukoloni wa Uingereza.
Wakili wa watu hao Martyn Day alisema: "Mateso yaliyowafika yaliwaacha wakiwa na madhara ya kudumu maisha yao yote."
Hata hivyo serikali ya Uingereza ilisema kuwa tangu mateso yanayodaiwa kufanyiwa watu hao ni muda mrefu, kwa hiyo haiwezi kuwajibishwa.
Kesi hii imewasilishwa na wanaume watatu na mwanamke mmoja, wote wakiwa na umri uliozidi miaka 70.
Wakili wao alisema kuwa watu hawa wanawakilisha jamii kubwa ya wenzao nchini Kenya alioteswa wakati wa harakati za kupigania Uhuru zilipoanza dhidi ya utawala wa kikoloni.
Taarifa zilisema wakoloni walikuwa wakiwafungia ndani ya kambi watuhumiwa waliopinga utawala wa kikoloni, na waliteswa kwa madai ya kushiriki matukio ya uasi.
Wakili wa walalamikaji hao, Day alisema kuwa wateja wake kipindi hicho walikabiliwa na vitendo visivyoelezeka kutoka kwa maofisa wa Uingereza katika miaka ya 1950 na 1960, ikiwa ni pamoja na kukatwa uume, ubakaji na kupigwa mara kwa mara.
Alisema kimsingi wanachokiomba ni kutambua yaliyowafika na kuwaomba radhi na msamaha. Na kwamba ni wajibu wa serikali ya Uingereza kuona kwamba watu hawa wanatazamwa kwa heshima na hadhi inayostahiki.
Kwa upande wake Tume ya Haki za Binadamu ya Kenya imesema kuwa wa Kenya 90,000 walinyongwa, kunyanyaswa na kujeruhiwa, huku wengine 160,000 kufungwa katika mazingira ya kutisha.
Ripoti rasmi iliyochapishwa mwaka 1961 ilibainisha kuwa zaidi ya Wafrika 11,000 wengi wao wakiwa ni raia pamoja na walowezi 32 wazungu waliuawa kipindi hicho.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช