.

WANAOTUHUMIWA KULA NJAMA ZA KUTAKA KUMUUA CHEGENI WATINGA KIZIMBANI

Apr 21, 2011

WATU wanne wakiwemo wanawake wawili ndugu, kati ya sita waliokuwa wakituhumiwa kula njama za kumuua aliyekuwa Mbunge wa zamani wa jimbo la Busega, Raphael Chegeni, wamepandishwa kizimbani.

Walisomewa mashitaka jana mchana, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Angelous Lumisha wa Mahakama ya Hakimu mkazi mkoa wa Mwanza bila kuulizwa wala kutakiwa kujibu lolote. Washitakiwa hao wa kesi ya jinai namba 113 ya mwaka 2011, hawakutakiwa kujibu lolote kutokana na mkanganyiko wa kisheria ambao ulipelekea kuahirishwa kwa kesi hiyo hadi leo na washitakiwa kwenda rumande Gerezani.

Mkanganyiko huo ni kutokana na kesi hiyo kusikilizwa aidha na Mahakama Kuu au na Mahakama ya hakimu Mkazi wa mkoa wa Mwanza.

Washitakiwa hao ni Dismas Zacharia (47) mfanyabiashara na mkazi wa Ramadi wilayani Magu, Erasto Casmir (48) ambaye ni pia mfanyabiashara wa jijini Mwanza.

Wengine ni wanawake wawili Helen Bogohe (54) mkazi wa Kisesa wilayani Magu na nduguye Queen Bogohe (37) ambaye ni mkazi wa barabara ya Kenyatta jijini hapa ambao kwa pmaoja wanatetewa na wanasheria wa kujitegemea Bernard Kabone na Mathew Nkanda.

Mwanasheria wa Serikali Paschal Marungu alidai Mahakamani hapo kuwa, wote kwa pamoja walitenda kosa la kula njama za kumuua Raphael Chegeni kinyume cha kifungu cha Sheria namba 215 ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 iliyorekebishwa mwaka 2002.

Marungu aliieleza Mahakama hiyo kwamba, aliieleza mahakama hiyo kwamba, washitakiwa hao walitenda kosa hilo tarehe tofauti kati ya mwezi Februari na Aprili 13 mwaka huu mkoani hapa na sehemu nyingine za Tanzania .

“Kwakuwa hatujajua kama shitaka hili litasikilzwa na mahakama Kuu au mahakama hii, leo sitawauliza na hawatajibu chochote washitakiwa.” Alisema Hakimu Lumisha.

Upande wa mashitaka ulidai kwakuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika washitakiwa wasipewe dhamana ili wasivuruge upelelezi kwa kuwa mazingira ya upelelezi wake yanahusiha uhalifu wa mtandao.

Kwa upande wa utetezi ukiongozwa na Kabonde, ulidai kuwa tangu wakamatwe na kupewa dhamana na polisi hakujawa na kuingilia upelelezi wowote.

Aliongeza kuwa “Suala la woga wa kuvuruga kesi liliondolewa na polisi wenyewe ambao ndio wapelelezi  hivyo naiomba Mahakama hii iwape dhamana hadi kesho (leo) mkanganyiko wa kisheria utakapokuwa umepatiwa ufumbuzi.”

Ndipo Hakimu Lumisha alipoieleza Mahakama hiyo kwamba hataweza kutoa maamzi yoyote hadi leo kutokana na muda wa kazi kupita na kwamba washitakiwa hao kuendelea kukaa chini ya ulinzi wa polisi.

“Sasa ni saa 9:59 inaingia saa 10:00, nilitakiwa kufunga kazi saa 9:30 hivyo sitaweza kutoa maamzi hadi kesho, muda wa kazi umeisha, washitakiwa watakaa chini ya ulinzi wa polisi.”

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช