.

YANGA MABINGWA WAPYA WA SOKA TANZANIA BARA

Apr 10, 2011


Kikosi cha Yanga

Na Mwanadishi Maalum, Mwanza
Nderemo na vifijo vimetawala leo katika uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa baada ya Yanga kutawazwa kuwa mabigwa wapya wa soka Tanzania Bara, baada ya kuinyuka Toto Africa, mabao 3-0 katika mechi ya funda dimba la michuano ya Vodacom lililofanyika katika uwanja huo..
Kombe walilokuwa wapewe Simba kama wangeibuka
mabingwa likirudishwa ndani
Kufuatia ushindi huo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Abbas Kandoro alimkabidhi kombe la ushindi nahodha wa Yanga Shadrack Nsajigwa, na pia kupatiwa wachezaji wote medali za dhahabu.

Mara baada ya nahodha Nsajigwa kupokea kikombe hicho mamia ya washabiki walilipuka kwa shangwe na vifijo na kuwabeza wapinzani wao wa Simba kabla ya kuzunguka uwanjani na timu yao huku wakishangilia kwa ngoma ya Kidedea na ma Vuvuzela.

Kandoro aliyekuwa mgeni rasmi katika pambano hilo , aliwapa hongera wachezaji hao na kuwatakia uwakilishi mwema katika mashindano ya kimataifa itakayowakilisha Tanzania Bara.

Katika pambano hilo Toto walilianza kwa kugongeana kwa pasi za uhakika na kulifikia lango la Yanga, iwapo washambuliaji wake wangekuwa makini wangejipatia bao la kuongoza mapema.

Yanga walijibu mashambulizi dk 18, 26 na 30 lakini washambuliaji wake akiwemo Davis Mwape aliyepiga kichwa ufyongo akiwa yeye na mlinda malango wa Toto Wilbert Mweta, walishindwa kuweka mpira wavuni.

Kosakosa hizo ziliendelea kwa timu zote kushambuliana kwa zamu huku Yanga wakijipatia kona sita zisizozaa matunda na hadi timu hizo zikienda mapumziko zilikuwa suluhu.

Yanga walianza kipindi cha pili kwa kumtoa Kigi Makasi na kumuingiza Jerson Tegete, dk 47 Nurdin Bakari aliwanyanyua mashabiki wa Yanga alipoipatia timu yake bao la kwanza.

Bakari aliyepiga mpira wa adhabu, alifunga kwa shuti kali lililokwenda wavuni moja kwa moja baada ya Devi Mwape kuchezewa vibaya nje ya eneo la hatari.

Devi Mwape aliipatia timu hiyo bao la pili na la ushini katika dk 63 baada ya Shadrack Nsajigwa kuamba amba na mpir katika winga ya kulia na kuachia kross iliyomkuta Mwape na kutumbukiza mpira kwa kichwa.

Yanga walizidi kulisakama lango la Toto na dk ya 88 Nurdin Bakari aliyemalizia pasi ya Nsajigwa, aliiandikia Yanga bao la tatu lilioipa Ubingwa baada ya kumpiga dobo kipa Huseein Tade aliyeingia badala ya Mweta.

Yanga: Yew Berko, Shadrack Nsajigwa, Abuu Zuberi, Nadri Canavaro, Chacha Marwa, Juma Seif, Fred Mbuna, Nurdin Bakari, Davis Mwape, Idd Mbaga/Mega Seme na Kigi Makasi/Jerson Tegete.

Toto: Wilbert Mweta/Hussein Tade, John Bosco, Philemon Mwendasile, Laban Kambole, Ladslaus Mbogo, Malegesi Mwangwa, Jackob Masawe, Tete Kang’anga, Sammy Kessy, Emmanuel Swita na Mohamed

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ª