Breaking News

Your Ad Spot

May 23, 2011

DC KANGOYE AWAASA TARIME KUSHIKAMANA

Na mwandishi wetu

Kangoye
 MKUU wa Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, Christopher Kangoye, amewaasa wananchi wa Tarime kuwa na mshimamano na wasikubali kuyumbishwa.

Pia, amesema ameguswa na tukio la kuuawa kwa wananchi watano waliopigwa na risasi walipovamia mgodi wa dhahabu wa North Mara, uliopo Nyamongo, Tarime.

Kangoye aliyasema hayo juzi kwa njia ya simu wakati alipotakiwa kutoa maoni yake juu ya  tukio hilo, ambapo alisema ameshtushwa na mauaji hayo ya wananchi.

Hata hivyo, alishauri vyombo vya usalama kuangalia utaratibu wa kuwadhibiti wananchi badala ya kuharakisha matumizi ya silaha za moto, ambazo mara nyingi husababisha maafa.

Pia, amewataka watanzania hasa wakazi wa Tarime kufuata taratibu na kuheshimu maonyo yanayotolewa na vyombo vya dola ili kudumisha amani kwenye maeneo yao.

“Mimi kama Kangoye nimeshtushwa na tukio hilo kwani, watu waleopoteza maisha ni wengi. Nitoe rai kwa wananchi kufuata sheria na taratibu za nchi na vyombo vya usalama kuangalia njia muafaka kudhibiti wananchi,” alisema Kangoye, ambaye aliwahi kuwania ubunge katika jimbo hilo.

Kuhusu baadhi ya wanasiasa wa upinzani kudaiwa kushawishi na kuwatumia wananchi kisiasa, Kangoye alisema si jambo jema na kutaka wananchi waachwe waamue mambo yao ikiwa ni pamoja na kushiriki shughuli za maendeleo.

Alisema tabia ya baadhi ya wanasiasa kuwatumia wananchi hasa vijana kama mtaji wa kujipatia umaarufu kisiasa, imekuwa ikishamiri hivyo ni vyema wananchi wakawa makini.

“Kuna wanasiasa wanawatumia wananchi ili kujipatia umaarufu na mambo yanapoharibika wanawakimbia.
“Ni lazima wana-Tarime tushikamane na kuwaepuka wanasiasa wa aina hiyo kwani, wanaweza kutuangamiza,” aliongeza Kangoye.

Mei 17, mwaka huu, zaidi ya watu 800 walivamia mgodi wa North Mara kwa lengo la kupora dhahabu, ambapo polisi waliokuwa na silaha za moto walipambana na wananchi hao na kuwaua watano kati ya waliovamia.

Tayari serikali imechukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kugharamia maziko na kuunda tume kuchunguza mauaji hayo.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages