Breaking News

Your Ad Spot

May 20, 2011

MARTHA MLATA AANZISHA MPANGO WA KUKUZA TAALUMA KATIKA SEKONDARI ZA KATA

MBUNGE wa Viti Maalumu mkoa wa Singida, Martha Mlata (CCM), ameanzisha mpango wa kukuza taaluma katika sekondari za kata.

Martha, ambaye amekuwa mstari wa mbele kusaidia jamii nchini, ametoa msaada wa vifaa mbalimbali vya elimu vyenye thamani ya sh. milioni 16.5 kwa Sekondari Kata ya Ndago wilayani Iramba, Singida.

Msaada huo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati huo, ambao utazifikia sekondari mbalimbali mkoani hapa.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo hivi karibuni, Martha alisema fedha hizo zimetumika kununua magodoro 42, mashuka jozi 42, unga wa sembe kilo 500, maharage kilo 100, mchele kilo 200 na magunia 10 ya mahindi.

Pia, alisema zitatumika kuweka umeme wa jua (Solar) shuleni hapo huku kiasi cha sh. milioni 1.1. zitatumika kulipia wanafunzi mitihani.

Martha alisema kuwa mpango wake huo umelenga katika kusaidia harakati za serikali kuboresha elimu nchini.

Alisema ameanza na sekondari hiyo kwa kuwa uongozi wa shule uliwasilisha ombi la msaada huo kutokana na kukabiliwa na changamoto nyingi.

“Nitaendelea kusaidia kwa hali na mali sekondari hii ili kuboresha taaluma kwa wanafunzi. Hapo nyuma niliipatia mifuko ya saruji iliyosaidia kupatikana kwa matofali 2,058 kwa ajili ya ujenzi wa hosteli pamoja na mabati 108,” alisema Martha ambaye amekuwa mbunge anayejitolea kusaidia maendeleo mara kwa mara.

Hata hivyo, amesema kuwa azma yake ni kuona wanafunzi hasa wa kike wakisoma kwa bidii na kuwaepusha na mafataki wa mitaani.

Alitumia fursa hiyo kuwaasa wazazi kufuatilia kwa karibu maendeleo ya wanafunzi shuleni ikiwa ni pamoja na kuchangia gharama za elimu

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages