*Asema ruksa kuwekeza na kufanya
biashara Tanzania
*Lakini ruksa hiyo ni kwa biashara halali
Na Mwandishi Maalum,
Rais Mstaafu wa awamu ya pili Mzee Ali Hassan Mwinyi akizungumza na wanachama na wajumbe bodi ya taasisi ya The Turkish-American Business Improvement and Development Council ( TABID) ya Jijini New York, Marekani. piicha zaid mwisho wa stori |
New York
Rais mstaafu wa awamu ya pili Mhe. Ali Hassan Mwinyi amewataka wafanyabishara wa kimarekani na kituruki kuja kuwekeza nchini Tanzania na kwamba kwa kufanya hivyo hawatajutia mitaji yao.
Akizungumza na wanachama na wajumbe wa bodi ya taasisi isiyo ya kiserikali ijulikanayo kama Turkish-American business improvement and development council ( TABID) ya jijini New York, Marekani.Rais Mwinyi alitumia fursa hiyo kuitangaza Tanzania kwa kuelezea fursa na maeneo ya uwekezaji yaliyopo nchini.
Katika mazungumo yake na wanachama hao,Rais huyo mstaafu ambaye amefuatana na mkewe Mama Sitti Mwinyi, amesema, zipo fursa nyingi na maeneo mbalimbali ya uwekezaji ilimradi uwekezaji huo uwe ni halali. “Njooni Tanzania, njooni mjionee nini Tanzania inaweza kuwapa, kuna msemo usemao kuona ni kuamini, licha ya haya ninayowaeleza njooni mjionee wenyewe. Kuna kila fursa ya kuwekeza, ili mradi biashara hiyo iwe halali, nina wahakikishieni hamtajutia uamuzi wenu wala mitaji yenu”.Akasisitiza.
Akasema kwa kuanzia wafanyabiashara na wawekezaji hao wanaweza kuja kushiriki maonesho ya Kimataifa ya Biashara ambayo hufanyika kila tarehe saba ya kila mwezi wa saba maarufu kama Saba-Saba
“Ninawakaribisha mje na mshiriki kwenye maonesho haya, hili ni eneo moja la kujionea fursa za uwekezaji na biashara, mtakutana na kubadilishana mawazo na wafanyabiashara wa ndani na nje, njooni tunaihitaji mitaji yenu na teknolijia zenu” akasihi Rais Mstaafu.
Akasema inasikitisha kuwa licha ya Tanzania na Marekani kuwa na uhusiano na ushirikiano mzuri lakini kumekuwapo na pengo kubwa katika ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji.
Amesema kasoro hiyo inatokana na matumizi ya watu wa kati na mawakala ambao kwa namna moja ama nyingine wameshindwa kuendeleza na kuvutia ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.
Baadhi ya maeneo ambayo Rais Mwinyi ameyataja kuwa yanahitaji uwekezaji ni pamoja na kilimo.
Akizungumzia eneo hilo, rais mstafu amesema Tanzania inayo hazina kubwa ya ekari 88 milioni ambazo zinafaa kwa kilimo lakini kati ya hizo ni ekari milioni 13 tu ambazo zinatumika kikamilifu
Kuhusu kilimo cha umwagiliaji amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na mito na maziwa ambayo maji yake yanafaa kwa kilimo cha umwagiliaji, huku kukiwa na zaidi ya ekari milioni moja ambazo zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji ingawa ni ekari 160.000 ambazo zinatumia kilimo hicho
Akasema Tanzania hivi sasa imejiwekea na inatekeleza sera na mipango inayolenga kuleta mageuzi ya kilimo kupitia mpango wake ujulikanao kama Kilimo Kwanza.
Hata hivyo amesisitiza kuwa pamoja na mipango mizuri ya kukifanyia mageuzi makubwa kilimo, mageuzi hayo yanaweza yasifanikiwe sana kama hapatakuwapo na uwekezaji katika kilimo cha kisasa na kinachotumia teknolijia za kisasa.
“ Hili ni eneo ambalo wamerakani na waturuki mnayo fursa kubwa ya kuwekeza, tunahitaji zana na teknolojia za kisasa, tunahitaji viwanda vya zana za kilimo na usindikaji za mazao yatokanayo na kilimo, tunauhitaji utaalamu wenu njooni tunayo ardhi kubwa na ya kumtosha kila mmoja wetu” akasititiza Rais Mstaafu.
Aidha ameyataja maeneo mengine ambayo yanafaa kwa uwekezani kuwa ni katika eneo la viwanda vikubwa na vya kati, ukanda maalum wauwekezaji maarufu kama EPZ na SEZ,madini, utalii, ujenzi wa miundombinu na uhamishaji wa teknolojia za kisasa na mitaji.
Akielezea zaidi ni kwa nini anawashawishi wamarekani na waturiki kuwekeza nchini Tanzania, Rais Mwinyi anasema Tanzania kupitia serikali yake imeweka sera, sheria na mazingira mazuri ya kufanya biashara zikiwamo sheria za kumlida mwekezaji, mali zake na mitaji yake bila ya kubagua kama mwekezaji huyo ni wa ndani au kutoka nje.
Aidha kama hiyo haitoshi anasema Tanzania ni kitovu kikuu cha uwekezaji kwa kuwa inapakana na nchi kadhaa ambazo wawekezaji watanufaika kwa kuuza bidhaa zao katika nchi hizo.
Kwa mfano anasema kuwa Tanzania ni mwanchama wa Jumuia ya Afrika Mashariki(EAC) na Jumuia ya Maendeleo ya Nchi za Kusini (SADC) huku kukiwa na jumla yatu milioni 300 ambao ni mtaji tosha kwa biashara.
Na kubwa zaidi anasema Tanzania ni nchi ya amani, utulivu na salama.
Rais Mstafu kwa kushirikiana na Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Ombeni Sefue pia alijibu maswali mbalimbali kutoka kwa watu waliokuwa wakimsikiliza.
Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi akionesha zawadi aliyokabidhiwa na wenyeji wake
Baadhi wa wanachama na wajumbe wa Bodi ya TABID wakimsikiliza Rais Mstaafu Mwinyi hayupo pichani. Aliyekaa mbele mstari wa kwanza kutoka kushoto
ni Mke wa Rais Mama Sitti Mwinyi
Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe Ombeni Sefue, Rais Mstaafu Ali Hassan
Mwinyi na Rais wa TABID Bw. Gokhan Ozkok wakijiandaa kujibu maswali mara baada ya Rais Mstaafu kumaliza mazungumzo yake ya kuitangaza Tanzania na vivutio vyake katika maeneo ya biashara na uwekezaji.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269