Breaking News

Your Ad Spot

Jul 20, 2011

MISS ILALA WAPIMA UKIMWI

NA MWANDISHI WETU, DSJ
Washiriki wa shindano la ulimbwende Kanda ya Ilala,wamepima kwa hiari ukimwi kuhamasisha jamii kujitokeza bila woga kupima ugonjwa huo ili kujua afya zao.
    Upimaji huo ulifanyika jana, katika Kituo cha Shirika la Huduma za Afya na Utafiti Afrika (AMREF), Upanga mjini Dar es Salaleo ambapo jumla ya warembo 17 walijitokeza na kupima afya zao.
      Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Kambi wa Miss Ilala, Regina Joseph alisema, wamechukua uamuzi wa kwenda na warembo hao kupima ukimwi ili kuhamasisha jamii kujitokeza kupimwa ugonjwa huo.
       Alisema, ipo haja ya wananchi kuendelea kuhamasishwa kwa njia mbalimbali kupima afya zao kwa kuwa bado wapo ambao bado wanaogopa au kuona aibu kwenda kupimwa ukimwi kutokana na sababu mbalimbali.
     "Hatua ya kujitokeza kupimwa itakuwa hamasa kubwa kwa watu wengine na pia itasaidia warembo wenyewe kutambua afya zao na hivyo kuchagua kwa usahihi aina ya maisha watakayoishi katika kupambana na ukimwi", alisema Regina.
       Akiwapa nasaha warembo hao, Meneja Mradi wa Angaza zaidi wa AMREF, Dk. Beati Mboya aliwapongeza kwa uamuzi wao lakini akawapa changamoto kwamba hatua waliyofanya itakuwa na manufaa zaidi kama watawapeleka wenzi wao nao wapimwe.
       "Mmefanya jambo zuri, lakini bila shaka kila mmoja wenu hapa ana mwenzi wake, kwa hiyo jitahidini nao waje kupima kwa kuwa kufanya hivyo kutawafanya muishi maisha yenye raha na kujiamini zaidi" alisema.
Shindano la Miss Ilala linatarajiwa kufanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, Julai 29, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages