Breaking News

Your Ad Spot

Jul 18, 2011

RAIS AENDA AFRIKA KUSINI LEO

Rais Jakaya Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatatu, Julai 18, 2011, anaanza Ziara ya kihistoria ya Kidola (State Visit) katika Afrika Kusini, ikiwa ziara ya kwanza ya aina yake kufanywa na Rais wa Tanzania katika nchi hiyo.
Rais Kikwete anafanya ziara hiyo kwa mwaliko wa Rais wa Afrika Kusini, Mheshimiwa Jacob Zuma ambaye utawala wake umekuwa karibu na kuwa na uhusiano mzuri na Tanzania tokea aliposhika madaraka ya kuongoza taifa hilo kubwa kiuchumi kuliko mengine yote katika Afrika.
Rais Kikwete na ujumbe wake ambao ni pamoja na Mama Salma Kikwete umeondoka nchini mchana wa leo kwenda Pretoria tayari kuanza ziara hiyo ya siku nne.
Pamoja na kwamba marais wa Tanzania waliomtangulia Rais Kikwete wametembelea Afrika Kusini mara nyingi kwa shughuli mbalimbali, lakini hakuna Rais wa Tanzania amepata kualikwa kufanya ziara rasmi, ya Kiserikali ama ya Kidola, tokea nchi hiyo kuingia katika mfumo wa demokrasia mwaka 1994.
Kwa mujibu wa ratiba ya ziara hiyo, Mheshimiwa Rais Kikwete, Mama Salma Kikwete na ujumbe wa Tanzania watapokelewa rasmi kesho asubuhi kwenye Jumba la Serikali mjini Pretoria na Rais Zuma na mkewe tayari kwa sherehe ya makaribisho ambazo zitafuatiwa na mazungumzo rasmi ya Kiserikali kati ya Tanzania na Afrika Kusini.
 Baada ya mazungumzo rasmi ambayo yatafuatiwa na utiaji saini wa mikataba na makubaliano katika Nyanja mbalimbali kati ya nchi hizo, viongozi hao wawili watahutubia mkutano wa waandishi wa habari. Baadaye, Rais Kikwete atatembelea Uwanja wa Uhuru akiandamana na Rais Zuma.
Mchana viongozi hao wawili watahudhuria chakula cha mchana cha wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika Kusini ambako watazungumza kuelezea umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.
Jioni, Rais Zuma ataandaa dhima ya kitaifa kwa ajili ya Rais Kikwete na ujumbe wake kwenye Nyumba ya Wageni ya Rais ya Afrika Kusini ambako Rais Kikwete atafikia wakati wa ziara hiyo.
Keshokutwa, Rais Kikwete na ujumbe wake watakwenda Cape Town ambako miongoni mwa mambo mengine ujumbe huo utatembelea Kisiwa cha Robben ambako wapigania uhuru maarufu wa Afrika Kusini, akiwamo Rais Mstaafu Nelson Mandela, walifungwa kwa miaka mingi na makaburu. Rais Kikwete atarejea nyumbani Alhamisi, Julai 21, 2011 asubuhi.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

18 Julai, 2011

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages