Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa,lilipokutana kujadili athari za mabadiliko ya tabia nchi na tishio lake kwa amani na usalama wa kimataifa |
Wakati tishio la mabadiliko ya tabia nchi likiwa Dhahiri kwa hatima ya mataifa mbalimbali yakiwamo yale ambayo ni visiwa. Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wamepinga kwa mara nyingine, juhudi za Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa za kushinikiza kupewa dhamana ya kuratibu athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Kwa siku nzima ya jumanne, Baraza hilo ambalo liko chini ya Uraisi wa Ujerumani kwa mwezi huu wa Saba, lilikuwa na mjadala wa wazi kuhusu Udumishaji wa amani na usalama wa kimataifa; madhara ya mabadiliko ya tabia nchi.
Lengo la majadiliano hayo pamoja na mambo mengine,yalikuwa ni kwa Baraza hilo kushinikiza liwe na uwezo wa kuratibu na kushughulikia uwezekano wa ukosefu wa amani na usalama utakaosababishwa na madhara ya yatokanayo na mabadiliko ya tabia nchi.
Karibu kila Balozi anayeiwakilisha nchi yake katika UM ,wakiwamo baadhi ambao nchi zao ni wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama maarufu kama P5, waliochangia majadialiano hayo, walisema ingawa wana kubali ukweli kwamba madhara ya mabadiliko ya tabia nchi, yanatishia usalama na amani ya jumuia ya kimataifa, bado Baraza hilo haliwezi kuwa na dhamana ya kulijadili , kulitolea maamuzi au maelekezo suala hilo.
Baadhi ya hoja zilizotolewa na wazungumzaji hao ni kwamba, ikiwa Baraza Kuu la Usalama litapewa dhamana hiyo. Siyo tu kwamba ,halina wataalam katika eneo hilo, lakini litakuwa linaingilia majukumu, dhamana na wajibu wa vyombo vingine vya UM ambavyo hasa ndivyo vilivyokasimiwa kulishughulikia tatizo hilo. Na kusisitiza kuwa viachwe vyombo hivyo vifanye kazi yake
Majadiliano hayo yalifunguliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ambaye pamoja na kuwasilisha taarifa yake kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, lakini pia alisema, athari za mabadiliko hayo zipo wazi kabisa na wala hazina mjadala.
Hata hivyo akasema, yeye anadhani kutokana na tishio la kiusalama, na ustawi wa maendeleo na uhai wa mataifa mbalimbali na watu wake. Baraza Kuu la Usalama, linapashwa pia kupewa dhamana ya kuratibu athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Akichangia majadiliano hayo, mwakilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika UM, Balozi Ombeni Sefue, alisema , Serikali ya Tanzania inatambua kwamba kuna kipengele cha usalama katika mabadiliko ya tabia nchi, kipengele ambacho pia kiko karibu katika kila jambo katika dunia hii.
“ Hata hivyo hatujayaleta hayo mengine kujadiliwa katika Baraza Kuu la Usalama la UM kama tunavyotaka kufanya kwa hili. Ujumbe wangu unaamini kwamba, mabadiliko ya tabia nchi yanashughulikiwa kwa ukamilifu na vyombo vya msingi vya UM. Vyombo ambayo vimepewa dhamana ya kushughulikia suala la Maendeleo Endelevu ” akasema Balozi Sefue.
Na kuongeza. “Mwaka 2007 tulikuwa na majadiliano kama haya, na maoni ya wajumbe wengi waliochangia majadiliano yale yalikuwa, Baraza la Usalama lijiepushe kuingilia dhamana za taasisi nyingine za UM kama vile Mfumo wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi (UNFCCC ) na Baraza la Uchumi na Mandeleo ya Jamii ( ECOSOC).
Aidha Balozi Sefue amasema, Tanzania kama ilivyo kwa mataifa mengine inatambua ukubwa wa athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa visiwa vilivyoko katika bahari ya Pasifiki.
Lakini akasema , tishio la kutoweka kwa nchi hizo, tishio ambalo pia linaweza kuzalisha wakimbizi ,haliko kwa visiwa hivyo tu. Bali ni tishio hata kwa Tanzania n ambayo nayo ina visiwa ambavyo vimo hatarini kutoweka.
Kwa hiyo akasema , ndiyo maana Tanzania imekuwa ikisisitiza na kusimamia kwamba majadiliano kuhusu tatizo la mabadiliko ya tabia nchi na athari zake lijadiliwe zaidi katika ngazi ya kimataifa kupitia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ili kupata ufumbuzi wa kudumu.
Akasisitiza kuwa, kwa kutenga tatizo la mabadiliko ya tabia nchi na kuliingiza katika Baraza Kuu la Usalama, kunaweza kufifisha jitihada zote ambazo zimekwisha kufanyika na hivyo kutokamilisha majadiliano yanayo simamiwa na UNFCCC.
Halikadhalika , mwakilishi huyo wa Tanzania amerejea wito uliotolewa na wajumbe wengine wa kutaka nchi maskini kama Tanzania na zile ambazo zimo katika hatari kubwa ya kutoweka, na zile ambazo zimeonyesha nia thabiti ya kudhibiti hewa ukaa na uhifadhi wa mazingira kwa kupanda miti ya ziada. Zisaidiwe kwa hali na mali na mataifa yaliyoendelea ambayo hasa ndiyo chanzo kikubwa cha mabadiliko ya tabia nchi.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269