Na Mwandishi wa Jeshi la Polisi –Zanzibar
Viongozi sita wa madhehebu ya dini wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya nchini, wamejitokeza mbele ya Kamati ya Maadili ya Viongozi wa Dini na Haki za Jamii na kukiri kujihusisha na biashara hiyo kwa muda mrefu sasa.
Afisa Uhusiano wa Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina, amesema kuwa baada ya kuhojiwa, Viongozi hao waliiomba Kamati hiyo kutowataja hadharani majina ama madhehebu yao kwa kuhofia kubezwa kwa madhehebu wanayoyaongoza.
Akizungumza mwishoni mwa ziara yao Visiwani humo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mchungaji William Mwamalanga wa Kanisa la Pentekosti Tanzania, amesema kuwa orodha hiyo na nyingine ya watu 18 wakiwemo wafanyabiashara wakubwa na Wanasiasa wanaojihusisha na biashara hiyo haramu zote zitafikishwa kwa Mkuu wa kitengo cha Polisi cha Kupambana na dawa za Kulevya nchi.
Mchungaji Mwamalanga amesema kuwa, tatizo la ongezeko la dawa za kulevya pia inazihusu nchi mbalimbali duniani na kwamba kamati hiyo itakutana na kamati nyingine kama hizo za nchi za Maziwa Makuu kwa maana ya Afrika ya Mashariki kuzungumzia ufumbuzi wa suala hilo.
Amesema mkutano huo pia utapendekeza kwa mabunge ya nchi hizo na Bunge la Afrika ya Mashariki kutunga sheria za kuwafilisi wale wote waliojilimbikizia mali kutokana na biasha za dawa za kulevya kwa nchi wanachama.
Hata hivyo Kamati hiyo ya Maadili ya Viongozi wa Dini na Haki za Jamii ikiwa hapa Visiwani, imesifu na kupongeza juhudi za Jeshi la Polisi kwa hatua zao za kukabiliana na ongezeko la dawa za kulevya.
Akizungumzia kero ya dawa za kulevya visiwani hapa, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar ACP Aziz Juma Mohammed, amesema kuwa Jeshi hilo limekuwa likiwakamata wengi wa wafanyabiashara na watumiaji wa dawa za kulevya na kuwafikisha mahakamani.
Hata hivyo, kamanda Aziz ametoa wito kwa wananchi na wadau mbalimbali wa usalama kuendelea kusaidiana na Jeshi hilo kwa kutoa taarifa za wale wote wanaojihusisha na mtandao wa dawa hizo.
Kamanda Aziz amesema kama kila mwananchi atatoa taarifa za siri Polisi za kuwepo kwa mtu ama kundi la watu wanaojihusisha na biashara hiyo ama uhalifu mwingine wowote, ni wazi kabisa kuwa Polisi iyawatia mbaroni.
Wiki iliyopita watu wawili wakazi wa Jijini Dar es Salaam, wamekamatwa kwenye uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar kwa nyakati tofauti wakitokea nchini Brazil ambapo kila mmoja alipatikana na kiasi kikubwa cha madawa ya Kulevya aina ya Cocaine.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269