Breaking News

Your Ad Spot

Aug 10, 2011

DK. MIGIRO AFUNGUA SEMINA YA KITAIFA YA UHAKIKI WA RIPOTI YA NCHI

Dk. Asha -Rose Migoro akifungua semina hiyo leo. Kushhoto ni
Mwenyekitiwa  NGC, Prof Hasa Mlawa na Kushoto ni Katibu wa NGC,
 Rehema Twalib na Naibu Waziri wa Mamabo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadh Juma
DAR ES SALAAM
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Dk. Asha-Rose Migiro, amesema mfumo wa kujitathimini katika utawala bora kwa nchi za Afrika utapunguza kwa kiasi kikubwa mianya ya rushwa.
       Dk. Asha-Rose alisema hayo Dar es Salaam leo, alipokuwa akizindua ripoti mpya iliyohuishwa ya Mpango wa Bara la Afrika Kujithimini Kiutawala Bora (APRM), ambayo itaonyesha Hali ya Utawala Bora nchini kwa mujibu wa maoni ya wananchi na wataalamu mbambali.
     Alisema nchi nyingi za Afrika zimekithiri kwa vitendo vya rushwa kutokana na masuala ya utawala bora katika baadhi ya nchi hizo kutopewa nguvu hatua ambayo haitoi fursa kwa wananchi wa kawaida kupata stahiki zao za kiraia.
        Dk. Asha-Rose aliipongeza serikali ya Tanzania kwa kuyapa kipaumbele masuala ya utawala bora na kuongeza kuwa ripoti hiyo inastahili kupigiwa mfano na baadhi ya nchi za Afrika zinazopinga utawala bora na kuwa mwanzo na kichocheo cha kuhatarisha amani.
        "Zipo baadhi ya nchi hazipendi masuala ya utawala bora, Tanzania ni nchi ya kupigiwa mfano na ripoti hii imeonyesha wazi kwamba tupo makini na tuna lengo la kutoa fursa sawa kwa kila Mtanzania," alisema Dk. Migiro.
       Alisema kujitathimini huko kunaangazia maeneo ambayo serikali inaweza kufanya vizuri akitolea mfano wa kutatua migogoro ya ardhi, mivutano kutokana na imani tofauti za kijamii na kiimani na kuepuka misuguano inayoibuka ndani ya vyama vya siasa iliyopo baina ya vyama hivyo.
       Aliongeza kuwa baadhi ya nchi zinazopinga utawala bora haziwezi kufanikiwa kwa kuwa kampeni ya kujenga utawala bora una nguvu kubwa duniani na UN unawaunga mkono watu wenye nia thabiti ya kujenga jamii zenye kutathimini utu, haki na fursa kwa wote.
        Alisema nchi zinazofuata kikamilifu misingi ya demokrasia mara nyingi zinafanikiwa katika kuepusha migogoro na mapigano na hupata fursa nzuri ya kuleta utulivu na maendeleo yenye kuzingatia masilahi ya watu wote katika jamii.
        "Migogoro mingi ya wafugaji na wakulima au msuguano wa ardhi unachangiwa kwa kiasi kikubwa na misingi mibovu ya utawala bora, ningependa kuona wananchi wanapata fursa sawa kuanzia ngazi za serikali za mtaa ambapo viongozi wetu wanakutana ana kwa ana wananchi," aliongeza Dk. Migiro.
        Aliipongeza Tanzania kufanya kazi kubwa kupitia mchakato wa Mfumo wa Uhakiki wa Kujitathimini Barani Afrika licha ya kukabiliwa na changamoto ya kupata fedha za kutosha.
        Ripoti hiyo imehuisha ile ya awali ya mwaka 2009 kwa nia ya kuongeza takwimu mpya kutokana na mabadiliko mbalimbali yaliyokwishajitokeza katika kipindi cha Julai mwaka huo hadi sasa. Ripoti hiyo pia itakuwa na Mpangokazi wa namna ya kuziondoa changamoto zilizobainishwa.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages