Breaking News

Your Ad Spot

Sep 13, 2011

WASIRA AMSHAWISHI MGOMBEA WA CHADEMA KUMPIGIA KURA DK. KAFUMU

Wasira akimnadi Dk. Kafumu Igunga leo
NA NKOROMO DAILY, IGUNGA
MGOMBEA wa ubunge wa CHADEMA  Joseph Kashinye ametakiwa kumpigia kura ya ndiyo mgombea wa CCM Dk. Dalaly Peter Kafumu kuonyesha kuwa anamheshimu kitaaluma.

Hayo yamesemwa leo Mjumbe  wa Kamati Kuu ya CCM, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Uratibu na Mahusiano, Steven Wasira wakati akihutubia kwa nyakati tofauti mikutano ya kampeni za CCM kata kadhaa jimboni hapa.

"Kashindye alikuwa mwalimu wa upe, na mnatambua wazi kuwa mwalimu wa upe ni wa kiwango gani cha elimu, hawezi kufikia hata kwa asilimia 99 kiwango cha elimu ya mgombea wa CCM, Dk. Dalaly Peter Kafumu, hivyo basi kwa kuwa wanataaluma huheshimiana namshauri Kashindye ampigie kura Dk. Kafum", alisema Wasira.

Alisema, wananchi wa Igunga watafanya kosa ambalo hawataweza kusamehewa na Mungu kama wanamchagua Kashindye wakamwacha Dk. Kafumu kwa kuwa Kafumu anamzidi Kashindye kwa kila sifa zinazostahili kumpatia mtu uongozi.

Wasira alisema, Dk. Kafumu ni mwanataaluma aliyebobea  na amekuwa mtumishi wa umma kwa muda mrefu katika ngazi ya juu serikalini na ni mzaliwa na mkazi wa Igunga hivyo ataweza kutatua kwa wepesi zaidi shida walizo nazo wananchi kuliko Kashindye.

"Huyu ni msomi ambaye katika kazi zake ndani na nje ya nchi amekutana na watu wengi , hivyo ni rahisi kwake kuonana ana kwa ana na wananchi wa Igunga na kisha akapeleka shida zao  moja kwa moja kwa ngazi husika hata kwa rais bila kuhitaji wakala kuliko Kashindye", alisema.

Alisema, moja ya sababu za wepesi wa Dk. Kafumu kufikisha matatizo ya wananchi kwa Rais ni kwa kuwa uchaguzi mdogo jimbo la Igunga unafanyika kukiwa tayari kuna rais ambaye ni kutoka CCM na kwa hivyo ilani inayotekelezwa kwa sasa ni ya CCM.

"Sasa kama ilani inayotekelezwa ni ya CCM wewe mwananchi wa Igunga unadanganywa eti umchague mbunge wa upinzani ndiye akatekeleze ilani hiyo, hii si sawa kabisa ni sawa na Yesu kama angemtuma shetani kuhubiri injili", alisema.

Wasira alisema, mbali ya ubora wa mgombea wake CCM yenyewe inazo sera zinazoeleweka na zoinazotekelezeka, kuliko vyama kama CHADEMA ambacho alidai kazi zake ni tatu tu, fujo, kudanyanya wananchi na kupinga kila kitu.

Alisema, wakati CCM ni chama chenye mtandao na uongozi unaoeleweka kila mahala vyama vingine kama CHADEMA ni vyama vya kwenye magari ambapo chama huonekana kuwa imara pale viongozi wake wa ngazi ya kitaifa wanapofika na magari eneo husika wanapoondoka wanakwenda na chama chao.

Uchaguzi mdogo wa jimbo la Igunga utafanyika Oktoba 2, mwaka huu, baada ya kampeni zilizoanza Septemba 7, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages